Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Dr. George Venance Lugomela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. DKT. GEORGE V. LUGOMELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipatia fursa hii ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maji. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uhai na nguvu na hivyo kuweza kutoa mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Rais wa nchi yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatua akina mama ndoo kichwani. Kusema kweli kazi hii ameianza tangu akiwa Makamu wa Rais. Tunampongeza sana kwa maono. Tumeona fedha nyingi ambazo ameweza kutoka katika kipindi chake katika Wizara hii ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Maji ndugu yangu Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya katika Wizara hii katika kutimiza maono ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Aweso kadiri anavyozidi kukaa kwenye hii Wizara ndivyo anavyokuja na matokeo makubwa zaidi, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, pia tunampongeza Naibu wake Engineer Kundo kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia kusimamia miradi na kufuatilia utekelezaji wa miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Katibu Mkuu wa Wizara hii, Engineer Mwajuma Waziri pamoja na watendaji wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha kwamba miradi ya maji inatekelezwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai na kila siku kukicha mahitaji ya maji yanaongezeka; kwa sababu watu tunazidi kuongezeka na kila mtu anahitaji maji na maji yanabaki kiasi kilekile. Wizara ya Maji imekuja na suluhisho kubwa na suluhisho hilo ni SGR ya maji, kwa maana ya National Water Grid. Niipongeze sana Wizara kwa kuanzisha mradi huu mkubwa wa National Water Grid. Kusema kweli utekelezaji umeanza. Mheshimiwa Waziri ametuambia kwenye hotuba yake kwamba tumeanza na ule Mradi wa KASHIWASA, kwa maana ya maji yanayokwenda Kahama – Shinyanga na sasa hivi yanaenda Tabora – Igunga – Nzega mpaka na wilaya zote za Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SGR au National Water Grid imeanza pia kutekelezwa katika Mkoa wa Simiyu kupitia ule mradi wa climate resilience. Mradi ule unachukua maji pale Nyashimo na kupeleka Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima kwa awamu ya kwanza. Tunaishukuru sana Serikali kwa hatua iliyofikia katika utekelezaji wa mradi huu. Mradi huu uko zaidi ya 50% na utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Wanasimiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na watendaji wote, awamu ya pili ya mradi huu itaenda Maswa na Meatu na hizi ndizo wilaya kame kabisa katika Mkoa wa Simiyu. Tuombe kwamba utekelezaji wa awamu ya kwanza uende kwa wakati ili tukamilishe awamu ya kwanza na tuanze awamu ya pili ambayo wananchi wa Maswa pamoja na Meatu wanasubiri kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mradi huu wa climate resilience tuna miradi midogo midogo ambayo inahitaji kukamilishwa wakati tunasubiri maji ya kutoka Ziwa Viktoria. Tuna mradi wa kuongeza mtandao wa maji Maswa Mjini; hapa tunahitaji tu milioni 257 ili kazi hii iweze kukamilika. Vilevile tuna mradi wa ununuzi wa dira za maji, 657,000,000 na mradi wa maji Sulu nao unahitaji 650,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, moyo usiyokuwa na shukrani ukausha yaliyo mema yote. Niishukuru Wizara kwa kazi kubwa waliyoifanya. Wameweza kutujengea mabwawa mawili katika mwaka huu wa fedha; Bwawa la Mwamashindike na Bwawa la Bugalama, jumla ya takribani 2,000,000,000. Wameweza kukamilisha ujenzi wa tenki la Induki la lita 2,000,000 kwa kutumia 2,000,000,000. Tenki hili limeboresha huduma ya maji katika Mji wa Maswa. Kuna mabwawa mengine mengi ambayo yamejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kazi ya ujenzi wa mabwawa pia iendelee katika Kata za Mwamanenge, Sangamwalugesha, Mwabaratulu, pamoja na Binza, Bwawa la Nyamasaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)