Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni matumaini ya akina mama, ninamshukuru sana. Pia nimpongeze Meneja wetu wa RUWASA, Mkoa wa Simiyu pamoja na cabinet yake, wanafanya kazi nzuri sana. Niwapongeze pia Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri ni majembe, wanafanya kazi nzuri sana, Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais mama yetu kipenzi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia nzuri ya kuwatua akina mama ndoo kichwani. Tangu Mheshimiwa Rais aingie madarakani na hata akiwa Makamu wa Rais alikuwa na nia nzuri ya kumtua mama ndoo kichwani. Hongera sana kwa Mheshimiwa Rais na ni lazima tumpongeze, tusipompongeza sisi Wabunge, hakika mawe yatapiga kelele. Mwenyezi Mungu amlinde Mheshimiwa Rais. Wanaomwombea mabaya washindwe na walegee katika Jina la Yesu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuletea fedha nyingi za ujenzi wa miradi ya maji Mkoa wa Simiyu. Kutokana na kutoa fedha hizi hali ya upatikanaji wa maji vijijini imeongezeka kutoka 60.85% hadi 71% mwaka 2022. Upatikanaji wa maji Mjini Bariadi, Busega, Maswa na Mwanuzi umeongezeka kutoka 55.7% kufikia 67% mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia Mkoa wa Simiyu shilingi 440,000,000,000 kwa ajili ya Mradi wa Ziwa Victoria. Ujenzi wa Mradi wa Ziwa Victoria na wilaya zake unakuja Simiyu, Wilaya ya Busega, Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu. Ujenzi huo umekwishaanza na umefikia 55%. Mheshimiwa Rais, ahsante sana. Awamu ya kwanza unaenda katika wilaya tatu, ambazo ni Wilaya za Busega, Bariadi na Itilima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Maswa na Meatu ina ukame sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais ametupatia magari ya kuchimba visima, lakini katika wilaya hizo kuna baadhi ya maeneo hata visima vikichimbwa, maji hayapatikani na hata kama yakipatikana, yanakuwa na magadi hayafai katika matumizi ya binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali itafute fedha awamu ya pili mradi uweze kuanza kujengwa. Ninaendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha. Jumla ya miradi 97 yenye gharama ya shilingi bilioni 63.7 imetekelezwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 chini ya RUWASA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ujenzi wa Mradi wa Maji Kabita, Wilaya ya Busega, umegharimu shilingi bilioni 3.1; Mradi wa Maji Mkula umegharimu shilingi bilioni 2.7; Maswa, ujenzi wa Mradi wa Maji Ipililo, shilingi bilioni 1.3; Itilima, ujenzi wa Mradi wa Maji Vijiji vya Madilana na Kinang’Weli, shilingi bilioni 2.3; na Meatu, ujenzi wa Mradi wa Maji Inonelwa, shilingi bilioni 4.8; Bariadi - Ngulyati, shilingi bilioni 1.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka unaoendelea RUWASA, Simiyu itatekeleza miradi 27 yenye gharama ya shilingi bilioni 21.04. Mfano Bariadi, Mradi wa Ihusi shilingi bilioni 1.6; Meatu, Mradi wa Mbushi shilingi milioni 573; na Itilima, Mradi wa Habia shilingi milioni 931. Ninamshukuru Mheshimiwa Rais. Mimi ni nani nisimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miradi yote hii aliyotuletea? Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Maji Lagangabilili lakini pia, Wilaya ya Itilima. Ninaiomba Serikali visima vimekamilika, imebaki usambazaji. Ninaiomba Serikali iweze kusambaza maji, Lagangabilili. Pia kuna Mradi wa Nanga ambao haujakamilika, niiombe Serikali ituletee fedha tuweze kukamilisha hiyo miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Miradi ya Bariadi inayoendelea kujengwa. Mradi wa Ihusi unaendelea kujengwa, Nkindwabiye unaendelea kujengwa, Mwasubuya, Mwauchumu, Mradi wa Sapiwi na Mradi wa Itubukilo. Ninaiomba Serikali iweze kutuletea fedha ili tuweze kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jumaa Aweso ni mmoja tu, ukimtafuta Mheshimiwa Waziri wa Maji, huwezi kumpata popote pale tofauti na Jumaa Aweso. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na Mungu awabariki. (Makofi)