Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuwa mchangiaji katika hotuba hii ya Wizara ya Maji. Kipekee, kwa mara nyingine pia nishukuru, kwa sababu ya Mradi mkubwa wa Ziwa Victoria unaoletwa Biharamulo wenye thamani ya dola milioni 55.1, ambapo kwa exchange rate ya leo ya 2,650 unaongea shilingi 146,000,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mradi mkubwa wa kihistoria unaokuja kutua akina mama ndoo vichwani. Si akina mama wa Biharamulo tu, kwa sababu tunaongea habari ya gridi ya maji ya Taifa, ni kwamba tuna hakika, kwa sababu Ziwa Victoria ni chanzo cha uhakika na gridi ni vyanzo. Tuna uhakika mradi huu baada ya kufika Biharamulo, utahudumia watu wa Ngara, wanaweza kwenda Kakonko na maeneo mengine yote ya jirani pale ili watu waweze kupata maji safi na salama, lakini maji yanayotoka kwenye chanzo cha uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya moyo wangu, nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, Jumaa Aweso. Nimshukuru Naibu wako Mheshimiwa Engineer Kundo, lakini pia na Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Maji Engineer Mwajuma Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya. Wanafanya kazi kama timu, ninakumbuka mradi huu, hata ulipokuwa unaenda kufanya presentation huko nje ukiwa unatafuta fedha, ulikuwa unanitumia clip unanionesha. Mungu ambariki sana Waziri kwa niaba ya watu wa Biharamulo aendelee kuwa na afya njema, lakini mambo mazuri hayo yaje na jimboni kwake pia, asituletee sisi akasahau kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa, ninataka niongelee, kwa sababu Wabunge wengi wamekuwa wanaongea visima vimechimbwa, maji hamna, hiki kimechimbwa maji hamna. Ni kweli huwezi kupata mradi wa maji kama maji hamna, kwa sababu kiasili maji hayako kila sehemu. Ndiyo maana, tumeona Serikali imechukua hatua hii ya kutumia vyanzo vichache, lakini vikubwa vilivyopo kwenye hii nchi ili maji yaweze kwenda kila sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika baada ya miaka mitatu, minne, mitano, hatutakuwa tunakuja hapa tena kulia na masuala ya kisima kimechimbwa umeme hamna, kwa sababu kama maji yanatoka kwenye chanzo kimoja, tuna hakika maji yataweza kufika kila sehemu vijiji vitapata maji, lakini na maeneo mengine yatapata maji. Hii ndiyo ajenda kubwa tunayoongelea leo ya gridi ya maji ya Taifa. Kwa hiyo, tuendelee kuwa wavumilivu, jambo hili lipite, tulipitishe kwa kishindo na bajeti hii ipite hatimaye tuweze kuyaona haya ambayo tunayapigia kelele yakifanyika kwa uhakika zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, experience yangu kipindi cha nyuma, wote tunaelewa, hususan bajeti hii iliyopita, ni kama vile hatukufanya miradi mipya, kwa sababu kulikuwa na maelekezo ya kutekeleza miradi mingi ya zamani. Kwa hiyo, tulione hilo na ni vizuri, kwa sababu, unapokuwa na mradi umeishia katikati wananchi hawawezi kupata maji. Tunapomaliza miradi michache tuliyoianza kipindi cha nyuma, tukatoa fursa ya kuanzisha miradi mingine mipya, hatimaye tunakuwa na kitu cha kusema kwa wananchi, na wananchi wale wachache waliopata maji, wanaona na wanakuwa mashuhuda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa ajili ya plan hiyo nzuri, tuna hakika miradi hii ambayo imewekwa kwenye bajeti kwa sasa, itaenda kutekelezwa sawa na ambavyo imewekwa kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa, Wizara ya Maji kumekuwa na shida. Pesa zao nyingi hazitoki kwa wakati, especially pesa za Mfuko wa Maji. Mheshimiwa Aweso huyu, maeneo mengi wakandarasi wanafanya kazi kwa heshima yake tu, amekuwa mtu rahimu, akija ofisini, kila anapofuatwa. Kuna kipindi unamwangalia anataka akusaidie lakini pesa hana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaomba, ring fenced money ambazo zimepitishwa na Bunge, zisiguswe, zirudi zikafanye kazi huku. Huyu baba anahangaika na Katibu Mkuu, lakini kama hawawapelekei pesa, leo wanalaumiwa wao. This is not fair, kwa hiyo, tungeomba wasaidiwe kwa kupelekewa pesa, zilizopitishwa kwenye bajeti ya Bunge, ili tusaidie miradi hii hata tusipoongea na wananchi kule, wananchi wayaone haya matunda mazuri ambayo tunayaongelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya PIC. Tulipokuwa kwenye ziara tukitembelea miradi, tulipita DAWASA pale. DAWASA wana expansiyon kubwa ya chanzo cha maji cha Ruvu Chini, lakini wale watu wanahitaji only 38.7 million dollars. nadhani. Tungeomba tuwape hii pesa wamalizane kule. Unajua ni aibu mimi wa Biharamulo nalilia maji, nipewe pesa 1,000,000,000, DAWASA inayobeba nchi nzima nayo inalilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakishampa huyo wakamalizana naye, mwakani watupe sisi wadogo. Kuliko leo unampa 1,000,000,000 haimalizi, unampa 2,000,000,000 haimalizi, mimi kwangu unanipa 500,000,000 haimalizi. Amalizane naye afanye biashara, hizo hela nyingine mwakani watuletee sisi, tukawapelekee wananchi tuwape huduma. Hilo jambo tuliliona, tunaomba wasaidiwe hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuliliona, ni suala la kutoza VAT kwenye umeme na VAT kwenye maji. Maji tunajua, VAT anatozwa end user. End user kwenye maji hakuna VAT. Hizi mamlaka zinatozwa VAT. Saa nyingine zinakaa na madeni TANESCO haziwezi kulipa, zinadaiwa TRA. Tulione hili, basi tuwasaidie, kama hamna VAT kwa end user, why are we charging them VAT kwenye masuala ya umeme na huduma nyingine wanazozitoa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka mamlaka zisimame, zifanye biashara, zilete gawio Serikalini, kwa sababu Serikali imeweka mtaji kwenye hizi mamlaka. Sasa hazitaweza kufanya hivyo kama bado tunazibana. Kwa hiyo, ninaomba hilo lionekane, tuwasaidie, waweze kufanya kazi, ili na sisi wa vijijini tunaowawakilisha wananchi walio wengi, wanaohitaji huduma ya maji, kwa sababu bado wanakunywa maji kwenye sehemu nyingine. Tumeambiwa ni zaidi ya 70%, haijafika 90% wala haijafika 100%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba watusaidie, ili bajeti inayofuata, pesa nyingi zielekezwe vijijini zitusaidie sisi, kuliko kuendelea kupeleka pesa tunagawanya nusunusu, inakuwa haitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona mic imewashwa muda mrefu, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ninaunga mkono hoja, pesa ipelekwe, Mheshimiwa Aweso na watu wake wakafanye kazi, sisi tuko nyuma yao tunawa-support. Ahsante sana. (Makofi)