Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Edefonce Joackim Canoni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. EDIFONSI J. KANONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Wizara ya Maji. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali siku ya leo, lakini pia nimwombee Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan awe na afya njema, kwa sababu ninajua maombi ninayomwombea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyezi Mungu halali, huwa maombi yangu yanafika kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri mwenyewe, imani ni kubwa sana kwa Watanzania na hasa akina mama walipo vijijini. Anafanya kazi kubwa sana, nimpongeze sana, lakini pia ni kijana. Kwa hiyo, tuna imani kwamba atakimbia zaidi. Mheshimiwa Waziri aongeze speed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani ni kubwa na Wabunge wote wanaoweza kuchangia hapa wana imani kubwa na Waziri kwa jinsi ambavyo anasimamia miradi ya maji. Ndoa nyingi zimepungua, zilikuwa zinavunjika kwa sababu ya akina mama kufuata maji umbali mrefu, lakini sasa amejaribu kupunguza changamoto na akina mama wengi, asilimia kadhaa wanaendelea kupata maji katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Maji ambao tumeupokea katika Wilaya ya Kalambo Mji wa Matai ambao huu mradi ni ujenzi wa chujio la maji wa shilingi 1,623,000,000. Mheshimiwa Waziri, tunamshukuru sana kwa kupokea huu mradi, lakini pia katika huu mradi, nimwombe Mheshimiwa Waziri, atoe kibali kuweza kuongeza mtandao wa maji katika Mji wa Matai ambao unakuwa kwa kasi, katika vitongoji vya Kateka, Kasisiwe, na Keleni, ambavyo vipo katika Mji Mdogo huu wa Matai. Pia, katika Mji wetu wa Matai, tuko border kati ya Zambia na Congo. Tunapokea wageni wengi, tunahitaji kuwa na miundombinu ya maji ili kuboresha maisha ya Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi wa maji inayoendelea katika Wilaya ya Kalambo, hususan katika Kata ya Legezamwendo ambayo ina vijiji sita, katika Kijiji cha Mombo, Mkombo, Utengule, Mlenje pamoja na Kalembe. Mheshimiwa Waziri, huu mradi, mkandarasi anadai shilingi 803,000,000. Nimwombe Waziri katika bajeti tutakayopitisha, basi aangalie jinsi ya kuweza kukamilisha mradi huu, tuweze kunufaisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Maji Kisumba ambao ni Kijiji cha Kisumba, Kafukoka, Kisenga pamoja na Kasote. Huu mradi, mkandarasi anadai shilingi 537,000,000. Nimwombe kwa heshima, imani yangu ni kubwa, huu mradi uweze kukamilika ili unufaishe wananchi wa maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Maji katika Kata ya Mnamba ambao mkandarasi anadai shilingi milioni 165. Nimwombe nao asukume ili katika bajeti tutakayoitoa aweze kupita, wananchi waweze kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mradi wa Maji wa Mbuluma katika Kata ya Mbuluma ambao upo katika Kijiji cha Mbuluma, ambapo Kalemasha na Lolesha ni wanufaika wa mradi huu ambao mkandarasi anadai shilingi milioni 165. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imani yangu kwa Mheshimiwa Waziri, ni kubwa na sina mashaka na si mimi tu, hapo na Waheshimiwa Wabunge tutapitisha bajeti, kuhakikisha kwamba haya ambayo ametusomea katika bajeti yako yanapita ili utekelezaji wa miradi uende kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ambayo hayana maji kabisa, kuna Kijiji cha Kasusu, Sengakalonje, Mpanga, Chalatila, Kanyezi pamoja na Ilambila. Haya maeneo Mheshimiwa Waziri, hayana maji kabisa katika hivi vijiji katika Wilaya ya Kalambo. Nimwombe katika bajeti itakayopita waangalie kwa jicho lingine, akina mama kwa maeneo hayo wanapata shida sana kufuata maji kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshawasilisha katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Kata ya Mpombwe - Kijiji cha Kapozwa; na Kalambo, katika Kata ya Samazi - Kijiji cha Samazi na Kipanga; hivi vijiji havina maji. Tunaomba kwa bajeti itakayopita Mheshimiwa Waziri atujali na sisi tupate maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa mradi ambao sasa umewasilishwa katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri, kwamba sasa kunaenda kujengwa Mradi wa Gridi ya Maji ya Taifa. Nimwombe, huu mradi ni mkubwa, lakini utachochea uchumi sana, siyo kwa matumizi tu ya maji ya kuoga na kufua, lakini utachochea uchumi kwa maana wananchi watafanya kilimo kwa wakati wote wa kuanzia mwezi Januari mpaka Desemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi katika pointi ambazo alizitaja Mheshimiwa Waziri kutoka Kigoma, Katavi, Kalema, ukija Rukwa unaitaja Kalambo lakini pointi yake iko Samazi. Nina imani kubwa na Mheshimiwa Waziri, niko tayari kupitisha bajeti yake hii kuhakikisha kwamba yale ambayo ametusomea katika bajeti yake yanatimia ili tukamilishe miradi yetu wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)