Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Kija Limbu Ntemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. KIJA L. NTEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kupata nafasi hii kuchangia katika Wizara ya Maji. Mheshimiwa Waziri Aweso, awali ya yote niipongeze sana ofisi kwa ujumla. Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu mmoja anasema, anaweza ukawa simba ukawa peke yako, lakini pia anaweza akawa simba akawa na wenzake wakafanya kazi vizuri. Mheshimiwa Aweso ni simba na ana simba wenzake wanaofanya kazi vizuri, niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, sitasoma sana mafungu na mimi ni msomaji wa mafungu, ataenda asome mwenyewe pamoja na Naibu wake. Watasoma Isaya 44:2, wakiusoma utawasaidia kwa ajili ya manufaa yao. Mheshimiwa Waziri, sisi kule kwetu Katoro, nadhani O-Kundo agomanile, okobhise Katoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ametuletea maji yenye gharama kubwa sana, kupitia Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitupatia maji nadhani hata yeye kwenye kampeni alikuja na wale watu wa Katoro tuliwaeleza kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameleta maji ya zaidi ya shilingi bilioni 6.3 pale Mji wa Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiwekeza lazima pia ujipange kuvuna ulichokiwekeza, umewekeza mradi mkubwa sana wa maji tunaomba, hoja yetu ni ndogo sana tunatamani watuletee mabomba ili tuweze kusambaza maji katika Mji wa Katoro maana maji yapo. Hadi sasa maji yanapampia kutoka Chankorongo nadhani ukipata muda utatembelea Katoro twende Chankorongo maji yapo yako mengi sana yanayosukumwa kwenye matenki ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, changamoto ukishayapampu unayapeleka wapi? Yanabaki kwenye matenki kwa sababu mabomba ya kusambaza maji ili wananchi wapate maji katika Mji wa Katoro na kata zake bado ni mdogo sana. Kwa hiyo, nimwombe, watu wanasema kushikilia shilingi, mimi sitaki nishikilie shilingi yake ila ninaomba anisaidie kupata mabomba ya kutosha ili watu wa Katoro waweze kusambaziwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ukishayasambaza haya maji wale idara ya maji wana uwezo wa kujiendesha kwa sababu watalipa madawa, watalipa watumishi watafanya, kwa sababu maji yamepata nafasi na maji yamesambazwa na wananchi wetu wamepata maji ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Waziri anapofanya hivyo anatuletea mabomba tukumbuke kwamba ili watu wetu waweze kupata huduma sasa maana siyo watu wote wanalingana kiuchumi, basi watupunguzie gharama za kuwasambazia watu hawa maji kwa sababu wanapokwenda kuwasambazia ikiwa gharama kubwa, watu watakaosambaziwa maji watakuwa ni wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe sana Waziri baada ya bajeti yake ajitahidi kutuhudumia, awasaidie wananchi wetu waweze kupata huduma ya kutosha ambayo itawasababisha wao kuamini kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alipopita katika Mji wa Katoro alitoa ahadi pamoja na kwamba kuna maji yanayokuja yenye mradi mkubwa kutoka Geita, alisema yatakuwepo maji ya kutosha katika Mkoa wa Geita kiujumla.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kabla ya huo Mkoa wa Geita kwa ujumla kwa kuwa Mheshimiwa Rais alishawekeza katika Jimbo la Katoro, basi ahakikishe anakwenda kusambaza hayo maji ili wananchi hawa waweze kupata huduma nzuri na Waziri tunamwamini na ndiyo maana tunatafuta nafasi sana ya kuzungumza, tumpongeze kwa kazi nzuri uliyoifanya. Miaka tisa yuko ndani ya hii Wizara na ameonekana kuwa simba jasiri anayeweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi wetu na katika Nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya haya machache, kubwa sana kwangu ninaweza nikazungumza mambo mengi sana, lakini hoja yetu sisi ni moja tu akatusambazie maji ya kutosha maana maji yalishayafika katika Mji wa Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, ninaunga mkono hoja, ninamwombea heri Mungu ambariki, achape kazi, asonge mbele pamoja na Mheshimiwa Naibu wake Mheshimiwa Injinia Kundo, wachape kazi, Mama amewaamini kwa moyo wa hali ya juu sana, waende wakapige kazi walete maendeleo kwa wananchi. (Makofi)