Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

Hon. Masanja Kungu Kadogosa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027

MHE. MASANJA K. KADOGOSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuweka sauti yangu kwenye Wizara hii muhimu sana katika Taifa letu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu amekuwa champion mkubwa sana tangu akiwa Mheshimiwa Makamu na sasa hivi Mheshimiwa Rais wa nchi yetu kwa suala la kutua ndoo mama zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimpongeze sana mdogo wangu Mheshimiwa Injinia Aweso anafanya kazi nzuri sana katika Taifa hili na Mwenyezi Mungu amembariki kwamba Wizara hii amekuwa nayo kwa muda mrefu kidogo sasa hivi, lakini ame-grow nayo na ninaamini kwamba Watanzania tunayoyaona humu na wao wanayaona hayo kwamba, kuna kuna maendeleo makubwa sana. Niungane kukubaliana na Waziri kwamba evolution kubwa ya kuleta RUWASA imeleta mabadiliko makubwa sana. (Makofi)

Hapa Spika (Mhe. Mussa A. Zungu) Alikalia Kiti

MHE. MASANJA K. KADOGOSA: Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze ndugu yangu mdogo wangu Mheshimiwa Injinia Kundo kwa kazi kubwa sana anayoifanya ni jirani yangu huyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, nimpongeze Engineer DG wetu, Bwana Wolta Kirita, anafanya kazi nzuri sana katika RUWASA, lakini Injinia Mwajuma ambayo ni PS wetu amekuwa ni mama kinara sana na tunampongeza kwa kupata hiyo zawadi. Pia kuna Injinia Mwampungo, kwa maana ya Wilayani Bariadi na Injinia wa RUWASA wa Mkoa wetu, Ndugu Esatula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeanza kwa kupongeza za kwa sababu wananchi wa Bariadi Vijijini wangenishangaa nisingezungumza haya. Sisi Bariadi Vijijini mpaka wakati tunafanya kampeni tulikuwa na upatikanaji wa maji ilikuwa kama 79.8% lakini kwa sasa hivi baada ya visima kadhaa kufunguliwa upatikanaji wa maji kwenye 84%, kwa hiyo, tuko above kidogo ya average ya 83%. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunashukuru sana katika hili. Kwanza Waziri kwa maana ya Wizara kwa kazi kubwa wanayotufanyia. Pamoja na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote, ni kweli ni lazima niseme kwamba kuna miradi ambayo wanaifanya katika Jimbo la Bariadi Vijijini, kuna miradi kama saba hivi na bahati nzuri dada yangu ameitaja. Mojawapo ni Husi kuna Nkindwabie, Mwauchumu, Sapiwi, Ikunguliyambeshi kwa maana ya Kilalo ninajua miradi hii ina thamani ya bilioni 4.7 na pesa ambazo zimeshatolewa mpaka sasa hivi ni bilioni 1.6. Ninajua katika bajeti hii wametenga kama bilioni 1.1, lakini tunahitaji ili tuweze kumaliza hii miradi bilioni 3.03.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa namna yoyote ndugu yangu ningependa kwamba nishike shilingi, lakini sasa ukaka mzito sitaweza kushika shilingi. Kwa hiyo, haya tutayazungumza kinyumbani kwani tunapenda sana hizi fedha zije ili tuweze kumalizia miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mradi mkubwa sana wenzangu, nisingetaka kurudia unaotokea Ziwa Victoria ambao ninajua itakuwa ndiyo tiba kubwa sana. Bahati nzuri ametupendelea sana kuwa na component mbalimbali mle ndani ikiwepo kwa maana ya ujenzi wa mabwawa ambayo yatatusaidia sana kwenye umwagiliaji, lakini kwenye mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ningetaka nizungumzie la mwisho kwa sababu ni dakika tano tu la Kitaifa. Duniani imefunikwa na maji kwa 71%, lakini katika 71%, 97.5% ni maji ya chumvi na ni 2.5% ndiyo maji ya kunywa au ambayo yanaweza kutumika katika majumba eco system, lakini vile kwa ajili ya agriculture. Sasa hiyo ina maana gani, maana yake ni kwamba kuna kuna scarcity, uhaba wa maji upo.

Mheshimiwa Spika, hiyo inasababisha kusema ni lazima tuwekeze kwenye maji, kama uwekezaji mwingine. Wamezungumzia mambo ya SGR ni lazima tuwekeze kama tutekeza kwenye Bwawa la Nyerere na bila uwekezaji kwa kweli hatuwezi kufika huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwenzangu hapa amezungumzia kuhusu hali ya maji sasa hivi kwenye miji yetu mikubwa. Ukiangalia uchakavu wa miundombinu au na mambo mengine ambayo yanasababisha uhaba wa maji haya ni mambo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna jambo moja ambalo ninapenda kukumbusha na alizungumza yeye mwenyewe; ushirikishaji wa sekta binafsi ni muhimu sana. Sasa hivi DAWASA wanahitaji kama bilioni 200 na ngapi, bilioni 250 kwa ajili ya kumaliza uchakavu tutapata wapi hizo pesa?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ili tutoe yale maji kutoka Rufiji tunahitaji zaidi ya trilioni moja tutapata wapi hizo pesa. Kwa hiyo, uwekezaji kwa maana ya kuvutia sekta binafsi kama Mheshimiwa Waziri alivyozungumza wakati fulani nilikuwa namfuatilia ni muhimu sana ili tuweze kufikia malengo ya kuwa na maji ya kujitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza, ninaomba niishie hapo na ninaomba kuunga mkono wa hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)