Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bariadi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninaanza kwanza kwa kuunga mkono hoja Wizara na bajeti hii. Hongera sana kwa Waheshimiwa Wabunge kwa kuliheshimisha Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, michango yao mizuri ya kusisimua na inayojenga na hakika dhana ya kuishauri na kuisimamia Serikali wameionyesha kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru sana na kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kwa mara ya pili kuwa Naibu Waziri wa Maji. Hii ni heshima kubwa kwangu binafsi kwa familia na wananchi wa Jimbo langu la Bariadi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni dhamana nzito ninayoipokea kwa unyenyekevu na moyo wa kujituma kwa ajili ya Watanzania wote. Imani yake kwangu ni kubwa, nami ninaahidi kuilipa kwa vitendo vinavyoonekana na matokeo yenye tija kwa Taifa letu. Nitafanya kazi kwa bidii kwa uzalendo wa hali ya juu na kwa kuzingatia maadili na uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yangu.
Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe kwa kutusimamia vizuri Bunge lako hili la Kumi na Tatu, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Emmanuel Nchimbi, Makamu wa Rais kwa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa kuteuliwa na kuanza kazi yake kwa kasi kubwa sana nimeshiriki ziara zake nimeona namna ambavyo anawatetea Watanzania. Nimeona namna ambavyo anasimamia haki itendeke, ninaona tumaini kubwa la Watanzania kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo yanatekelezwa na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu Jumaa Hamidu Aweso, huyu ni kiongozi, huyu ni kaka, huyu ni rafiki, huyu ni ndugu ambaye namna ambavyo anaijenga Wizara katika mshikamano na umoja inatufanya kutekeleza majukumu yetu kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, bila kusahau niwashukuru sana sana wananchi wa Jimbo la Bariadi walionipigia kura za kunifanya niwe mwakilishi wao. Ninafahamu kuna Madiwani wako hapa, kuna watendaji wa kata wako hapa, kuna Makatibu wangu wako hapa, lakini pia kuna vijana ambao wanatokana na vijiwe vya kahawa wamekuja kushuhudia mwakilishi wao nikisimama nao kutetea maslahi ya wananchi wa Bariadi na wananchi wa Tanzania nzima.
Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba kazi hii kama ambavyo alisema Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, tunao wasaidizi wetu ambao wanatufanya tutekeleze majukumu yetu, ninatambua kwamba kazi zetu ni nzito. Hata hivyo, kwa upekee kabisa nimshukuru sana mke wangu Grace Kundo kwa kazi nzuri sana ya kunivumilia na kuhakikisha kwamba anaendelea kuwa sehemu ya mafanikio ambayo tunaendelea kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunatambua kazi kubwa ambayo imefanywa na Waheshimiwa Wabunge kwa siku ya leo mambo ya msingi ambayo leo nimeyasikia. Jambo la kwanza, ni kuhusiana na utekelezaji wa miradi viporo ambayo haijakamilika. Tumeyapokea kwa uzito stahiki maelekezo ya Wabunge na sisi tutaenda kuhakikisha kwamba tunasimamia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nimesikia kuhusu upotevu wa maji, hili ni jambo ambalo sisi kama Wizara tumejipanga. Tunayo mikakati, tumebainisha changamoto, tumebainisha vyanzo vya matatizo, lakini tumejipanga kuweka mikakati ya kwenda kupambana na upotevu wa maji.
Mheshimiwa Spika, lengo ni kwamba tusipate changamoto ya maji kupungua kwa wananchi wetu. Tunafahamu kwamba ukidhibiti upotevu wa maji ni njia mojawapo ya kuongeza upatikanaji wa maji. Hilo tunaenda kulisimamia kuhakikisha kwamba linaweza kuleta tija zaidi.
Mheshimiwa Spika, pia, tumesikia suala la vitendea kazi. Waheshimiwa Wabunge tumelipokea tunayo maelekezo, lakini mpaka sasa RUWASA wameshapewa fedha kwa ajili ya kununua...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu muda wako umekwisha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kuunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)