Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, asiyeshukuru watu hata Mungu hawezi kumshukuru. Kwa dhati ya moyo nikushukuru wewe binafsi hasa kwa uendeshaji wako wa Bunge na mageuzi makubwa ambayo umefanya katika Bunge letu, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika Wizara yetu hii ya Maji. Ninataka nimhakikishie mimi Jumaa Aweso ambaye nimepewa dhamana katika Wizara hii ya Maji sitokuwa kikwazo kwa Watanzania na kwa Waheshimiwa Wabunge kupata maji safi salama na yenye kutosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Makamu wa Rais, lakini kwa dhati ya moyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu tangu ameaminiwa kwa muda mfupi amefanya ziara katika maeneo mbalimbali katika sekta yetu ya maji, lakini amekutana na watendaji wote wa Wizara yetu ya Maji. Nini maana yake? Mheshimiwa Rais ameelekeza kwamba anapoondoka aache tabasamu. Mtendaji Mkuu anasimamia kuhakikisha tabasamu inapatikana kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kwa dhati kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Wametoa maoni, ushauri na mchango, sitaki nisimame hapa kujitetea. Maoni na ushauri ambao wameutoa sisi tunaupokea kwa ajili ya kwenda kuufanyia kazi na kwenda kuimarika zaidi katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuaminiwa kwa mara nyingine kuwa Waziri wa Maji, jambo la kwanza ambalo tumelifanya sisi kama Wizara ya Maji tumesema kwanza tufanye tathmini. Tumejitathmini kama Wizara, lakini tumefanya tathmini hasa juu ya watendaji wetu hasa katika taasisi zetu. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa juu ya suala la ukamilishaji wa miradi.
Mheshimiwa Spika, ukisoma katika hotuba yangu ya bajeti moja ya vipaumbele vyetu saba tulivyoviweka katika Wizara yetu ya Maji ni ukamilishaji wa miradi ambayo tumeianza. Ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tuna miradi 992 vijijini, tuna miradi 196 mijini, tuna miradi ya maji 26 ya maji taka mijini. Ninataka nikuhakikishie hii ndiyo vita tunayokwenda kupigana kuhakikisha miradi hii ambayo tulioianza tunakwenda kuikamilisha ili Watanzania wao mijini na vijini waweze kupata huduma maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, uongozi ni kuacha alama. Waheshimiwa Wabunge wamezungumza miaka yote kuhusu suala la maji. Ninataka niwaambie huwezi kujua unapokwenda kama hujui ulipotoka, tumetoka mbali. Nchi yetu ya Tanzania ina vijiji 12,333 mpaka 2006 tulikuwa kwenye vijiji 3,000. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliapa na akaja na kauli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani na alihutubia katika Bunge hili, akasema mimi ni mama na asilimia kubwa wanaoteseka juu ya adha ya maji ni akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, akaenda mbali kunielekeza mimi Waziri wa Maji nikimzingua atanizingua. Ninataka niseme tumeanzisha Wakala wa Maji Vijijini, leo tumefika vijiji 10,758, mama apewe maua yake.
Mheshimiwa Spika, ninataka niseme vijiji vilivyobakia katika nchi yetu ya Tanzania ni vijiji 1,575. Waheshimiwa Wabunge lazima tuingie katika historia. Moja ya kazi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuisimamia Serikali. Ninaomba watusimamie sisi Wizara ya Maji katika kipindi hiki cha miaka mitano nikiwa kama Waziri wa Maji, ninaona nchi yote ya Tanzania na vijiji vyote vinakwenda kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Maji tumeweka mikakati. Mkakati wa kwanza; ili tuhakikishe vijiji vyote vinafikiwa na huduma ya maji safi na salama tumesema tuwekeze kwa watendaji kwa maana ya rasilimali watu. Tunataka Mtendaji wa Wizara ya Maji aseme inawezekana. Tunataka mtendaji wa Wizara ya Maji awe ni mtu ambaye analeta matokeo. Hatutaki Mkurugenzi suti. Hatutaki mtendaji anayojua AC imeisha. Hatutaki mtendaji anayesema Wi-Fi imekwisha. Tunataka Mtendaji wa Wizara ya Maji asizoee shida za wananchi katika kuhakikisha watu wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo tulokubaliana kama watendaji wa Wizara ya Maji, alternative financing. Tunajua kabisa Wizara ya Maji, Mheshimiwa Rais anatupatia fedha, lakini lazima tujiongeze kwamba tuwe na alternative financing.
Mheshimiwa Spika, tumekwishaanza Tanga. Tuli-aim tupate shilingi 53,000,000,000, tumepata shilingi bilioni 54. Hayo ni mafanikio makubwa. Tunazielekeza mamlaka zingine ziige. Hili tumeanza na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hivi karibuni tutaanzisha water infrastructure bond ambayo itakwenda kutatua matatizo ya maji na kujenga miradi ya kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine tumeona fursa ya Mheshimiwa Rais ya mahusiano ambayo ameyafanya kwa muda mfupi katika Wizara yetu na katika Taifa letu. Amenipa kibali nimekwenda Ufaransa. Nimekwenda Ufaransa, nimerudi tumepata shilingi 220,000,000,000, tumesaini Morogoro. Morogoro wanakwenda kupata huduma ya maji safi na salama. Tumekwenda Korea kwa muda mfupi kwa kibali cha Mheshimiwa Rais. Tumekwenda tumerudi na fedha kwa ajili ya majitaka katikaJjiji la Dar es Salaam, kwa ajili ya majitaka kwa ajili ya Jiji la Dodoma, kwa ajili ya majitaka kwa Jiji la Iringa, kwa Mji wa Iringa. Hayo ndiyo mapinduzi ambayo anayafanya Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tumelifanya tumeweka timu katika Wizara yetu, Wataalamu, kazi yao asubuhi… (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa tusubiri. Mic yako haifanyi kazi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, katika jambo lingine ambalo tumeliona ni kwamba tutumie private sector kwa maana involvement ya private sector. Lazima tukubali involvement ya private sector siyo mpaka tajiri awe mzungu. Leo tunashuhudia kama mtu anaweza kununua coaster vijijini, anaweza kununua basi vijijini, anaweza kujenga mradi wa shilingi milioni 30 na watu wakapata huduma ya maji safi na salama. Sisi Wizara ya Maji jukumu letu ni kusimamia gharama na ubora.
Mheshimiwa Spika, tumeona leo Wizara ya Elimu pamoja ni jukumu la Serikali kutoa elimu, zipo shule za private zinatoa elimu. Tunaona kuna Wizara ya Afya jukumu lake ni kutoa afya, lakini vipo vituo vya afya vya private, watu wanapata huduma. Ninataka tuseme na sisi kwa nia moja lazima tulimalize tatizo la maji. Pia, wapo wadau mbalimbali kwa maana ya NGOs pamoja na wadau wengine wa benki, taasisi za dini, leo tunazialika kuhakikisha nguvu zetu tunazielekeza katika vijiji 1,575 ambavyo vimebaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninataka niwatie moyo Waheshimiwa Wabunge tumeweka huu mkakati wa vijiji 1,575 na tumeviwekea kauli. Wizara ya Maji inaitikia, 1,575 tupo site kikazi zaidi. Huo ndiyo uelekeo wa Wizara yetu ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeanza kuwatangazia wenzetu. Tumepata Water for People amekuja kwa muda mfupi ametupa zaidi ya shilingi bilioni 77 ameenda kufanya kazi pale Mpwapwa. Kwa hiyo, huo ndiyo uelekeo wetu wa Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine Wizara ya Maji lazima tukubali kubadilika tutumie teknolojia kwa ajili ya mageuzi ya Wizara yetu ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni zilipendwa leo kusikia mwananchi wa Tanzania anabambikiziwa bili za maji. Ni zilipendwa kusikia kwamba kuna upotevu wa maji. Teknolojia lazima zitumike. Yapo baadhi ya maeneo kisima kinachimbwa, lakini wananchi wanatumia maji chumvi, haiwezekani. Ipo mitambo ambayo tunaweza tukatumia kubadili maji chumvi na kuwa maji baridi ili Watanzania waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Huo ndiyo mwelekeo wa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, Nchi yetu ya Tanzania si maskini wa vyanzo vya maji. Tuna Ziwa Victoria, tuna Ziwa Nyasa, tuna Ziwa Tanganyika, tuna Mto Ruvuma na Mto Pangani, uelekeo wetu tukatumie vyanzo toshelevu katika kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji.
Mheshimiwa Spika, tunajua kabisa tunakwenda katika Dira 2050. Tunapokwenda katika Dira ya 2050 lazima tuwe na maji toshelevu. Tunakwenda kwenye kongani ya viwanda. Kilimo ambacho tunachotaka kulima tusitegemee kudra za Mwenyezi Mungu, tunataka kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, ili tuweze kuwa na kilimo cha umwagiliaji maana yake lazima tuwe na rasilimali toshelevu zitakazoweza kutumika.
Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge jambo lolote kubwa au maono yoyote makubwa unayotaka kuyafanya mara nyingi yanaanza na ‘haiwezekani.’ Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi ambaye mambo yaliyoshindikana leo yanawezekana.
Mheshimiwa Spika, miaka tangu 1954 lilizungumzwa Bwawa la Kidunda leo linatekelezwa. Miaka tangu ya 1973 lilizungumzwa Bwawa la Farkwa tukimaliza Bunge tunaenda kumkabidhi mkandarasi kwa ajili ya kuanza kazi. Tunapozungumza National Grid ya Taifa siyo kama tutaenda kufanya tumeshaanza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nenda zako Kilimanjaro, tuna Mradi wa Same - Mwanga zaidi ya shilingi bilioni 400 umekamilika. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba Mradi wa Same Mwanga ufike Korogwe. Ukifika Korogwe tuna Mradi wa zaidi ya shilingi bilioni 172 wa Miji 28. Uungane na maji ya Mradi wa Same Mwanga yaende Handeni, Korogwe, Muheza, yafike mpaka Chalinze kwa Mheshimiwa Ridhiwani yatakutana na maji ya DAWASA yataungana.
Mheshimiwa Spika, ukienda zako kule Ziwa Victoria maji yamefika Tabora. Malengo ya Mheshimiwa Rais maji yale sasa yafike hapa katika Jiji la Dodoma. ukienda Simiyu tuna mradi wa zaidi ya shilingi 440,000,000,000 tunayatoa maji ya Ziwa Victoria kwa ajili ya kuyaunganisha wilaya zote katika Mkoa wetu wa Simiyu. Huo ndiyo uelekeo wa Wizara yetu ya Maji na huo ndiyo uelekeo wa Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hapatikani kila mahali. Tumempata lazima tumtumie kwa maslahi ya Watanzania na sisi tuweze kukumbukwa katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaomba kutoa hoja. Ahsante sana. (Makofi)