Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Steven Lemomo Kiruswa (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hii iliyopo mezani ya bajeti yetu ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuwa hapa leo kwa mara nyingine katika bajeti hii ya kwanza tangu tuingie katika Awamu hii ya Muhula wa Pili wa Serikali ya Mama Samia, Serikali ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru yeye mwenyewe kwa kuendelea kuniamini kuwa Naibu Waziri wa Madini nikimsaidia Waziri mahiri, kijana mwenye hekima na busara na mwenye kipaji cha uongozi, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde ambaye chini ya uongozi wake tumeona matokeo kama yalivyowasilishwa kwenye hotuba yake leo asubuhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya uongozi wake na timu kubwa tunayofanya nayo kazi inayoongozwa na Katibu Mkuu Mheshimiwa Samamba pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Kamishna wa Madini, Viongozi na Wakurugenzi wa Taasisi mbalimbali na Bodi zinazosimamia hizo Taasisi za Wizara kazi mnayoiona ni matokeo ya kazi ya timu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya ufinyu wa muda nijikite kujibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Kamati yetu, lakini pia nimwachie Waziri nafasi aweze kujibu hoja za wajumbe walioongea hapa ambao ni Wabunge. Hata hivyo, nisianze kabla sijaishukuru Kamati tuliyonayo. Kamati hii ya Wizara ya Madini ni Kamati mahiri, yenye wataalam wa madini, ni Kamati yenye watu wenye maono na ambao wamejitoa kwa hali na mali katika kusaidia uendeshaji wa Wizara hii kwa ushauri na maoni mbalimbali ambayo sisi tumeyapokea na kila wakati tumekuwa tukiyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa yao ya leo kuna baadhi ya hoja ambazo wamezileta. Kwa mfano wamesema wanaishauri Serikali iendelee kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa migodi nchini. Sisi katika kuliitikia hili ambalo tumepokea huu ushauri tumetenga shilingi 4,750,000,000 kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya TEHAMA ambayo itakwenda kutusaidia kurahisisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa shughuli za uchimbaji madini nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia imeishauri Serikali iendelee kuimarisha ushirikiano wa Serikali katika Wizara yetu na Serikali za Mitaa, watu binafsi, sekta binafsi na taasisi za utafiti. Katika hili ninapenda kuijulisha Kamati yangu Tukufu kwamba, Serikali imeendelea kushirikiana kwa karibu sana na hizi taasisi. Kwa mfano, kuna ushirikiano wa karibu sana katika suala la ufungaji migodi, suala la ukaguzi wa migodi, suala la ukaguzi wa madini yanavyochimbwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kuna wataalam kutoka TAKUKURU, kuna watu kutoka Ofisi ya DC, kuna wataalam mbalimbali ambao hushiriki shughuli hizo na hata katika shughuli za CSR ambazo Wabunge wameliongelea sana hilo suala hapa na ninajua Waziri atalitolea ufafanuzi, kwamba kwenye CSR siku zote ni Kamati inayoundwa yenye mwekezaji na wajumbe kutoka halmashauri, ndiyo wanaofanya hizi kazi, kwa hiyo ushirikiano huo utaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Kamati iliishauri Serikali kupitia Wizara ya Madini kwamba waongeze usimamizi wa kina kwa taasisi zake. Tuwaongezee uwezo taasisi zetu, tuwape vitendea kazi, tuwape magari, tuwape vifaa, tuwaongezee mafunzo na ofisi na haya yote tumeendelea kutekeleza, kila mwaka wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utendaji kazi kwenye taasisi zetu zote tano zinazosimamiwa na Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuliongelea Shirika letu maarufu la STAMICO (Shirika la Taifa la Madini). Kamati imependekeza kwamba baada ya kuona kile kiwanda cha Tabora ambacho Mheshimiwa Mbunge wa Sikonge ameliongelea sana hapa kwamba huo mtambo haujaanza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kusema kwamba tulipokwenda kutembelea kwenye commission tuliwapa siku 30 waanze kufanya kazi. Tunafuatilia kwanza tujue kama kweli bado haujaanza kazi, lakini Rafiki Briquettes ambayo ni nishati safi inayotokana na makaa ya mawe licha ya kwamba imewekezwa hapo Tabora, Kamati iliomba tutafute maeneo mengine ya kuongeza kwa sababu ya wakulima wa tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu hii kwa maelekezo yao imetupatia kazi ya kuendelea kufanya tathmini tuone ni wapi tunaweza kuongeza mitambo ya Rafiki Briquettes ili kuondoa changamoto ya watu wanaotumia kuni katika kuchoma tumbaku. Tumewekeza hii mitambo Kiwira, tumewekeza Pwani, tuna mitambo inakuja Dodoma, kuna mengine itaenda Geita na STAMICO wataendelea kupanua wigo wa kutekeleza azma ya kusambaza nishati safi mbadala inayotokana na makaa ya mawe ambayo tunayo kwa wingi katika nchi yetu katika kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia imeendelea kuishauri kupitia Wizara yetu kwamba STAMICO ishiriki kikamilifu katika uwekezaji wa uchimbaji wa migodi mikubwa. Pia ninapenda kuwaambia Wajumbe wa Kamati na Bunge lako Tukufu kwamba tumewatengea STAMICO shilingi 4,100,000,000 katika bajeti ya mwaka huu ili wazidishe utafiti katika kugundua maeneo yenye uchimbaji mkubwa ambao unaweza ukawa na tija na wao wafanane na Barrick, GGML na Ashanti Gold Mine. Huo ndiyo mwelekeo na siri ya mafanikio kwenye uchimbaji, ni utafiti na ndiyo maana Wizara inaendelea kuwaongezea fedha katika bajeti yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Kamati imeelekeza kwamba kuna vituo vya mfano walivyovitembelea wakashauri tuendelee kuweka vituo vya mfano vya kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo. Walienda cha Katente, Lwamgasa, walitembelea vyote lakini sasa wanataka tuongeze hivyo vituo na sisi kama Wizara tumeitikia wito huo. Tuna vituo vingine viwili vinakwenda kujengwa katika mwaka huu wa fedha katika maeneo ya Buhemba na katika maeneo ya Mwakitolyo katika Mkoa wa Shinyanga, Buhemba ipo katika Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kituo kingine cha umahiri katika Sekta ya Uchakataji Chumvi ambayo imekamilika ipo kule Lindi na inaweza ikaanza kazi wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi miwili au mitatu ijayo. Kwa hiyo, STAMICO itaendelea kupanua wigo katika kuwajengea wachimbaji wadogo uwezo kwa kuweka vituo mahiri vya utoaji mafunzo na uongezaji wa thamani madini yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia iliendelea kuhamasisha katika Sekta ya STAMICO kwamba Serikali ijikite zaidi katika kuongeza hii fani ya ukaguzi. Kwa sababu suala la ukaguzi ni nyeti sana katika masuala ya usalama wa watu migodini, mazingira na kadhalika, lakini sisi kama Wizara tumeendelea kupanua wigo katika ukaguzi. Mwaka huu wa fedha unaoishia tulikagua migodi mikubwa sita, tukakagua ya kati 31 na migodi ya wachimbaji wadogo wadogo 9,621.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Kamati imeendelea kuishauri Serikali kwamba Maafisa wetu wa Ukaguzi wajengewe uwezo. Kila mwaka wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya mafunzo na tunaendana na teknolojia ya kisasa, kila teknolojia mpya inapotoka sisi hatupo nyuma katika kuinunua kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalam wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ilitushauri kwamba tuangalie namna ya ku-deal na suala zima la watu wanashikilia leseni, watu wanahodhi leseni. Suala hili ninajua Waziri atalitolea ufafanuzi kwa kina. Hata hivyo, itoshe kusema kwamba Serikali imepokea huu ushauri na tutaendelea kufuta leseni zinazokuwa hazifanyiwi kazi. Hili ni zoezi endelevu na baada ya kufuta Waziri atazitangaza na wachimbaji wadogo ndiyo watapewa vipaumbele katika leseni zinazokwenda kufutwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yetu pia imeendelea kushauri Wizara kwamba mifumo ya kidijiti iendelee kuimarishwa ili kurahisisha utendaji kazi na ufanisi wa kazi zetu kama Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu katika suala hili, Serikali inalifanyia kazi kwa umakini sana. Sasa hivi tupo katika hatua za kuboresha mfumo tulionao wa utoaji leseni, ufutaji leseni, ulipiwaji leseni. Kwa hiyo, tunategemea siku siyo nyingi zijazo mtu atatumiwa tu ankara yake aweze kulipia leseni yake na ndani ya muda ambao utakuwa umebainishwa na kanuni zitakazorekebishwa, asipofanya hivyo leseni yake inapotea automatically. Kwa hiyo, ninadhani teknolojia inaenda kutupeleka ndani sana katika usimamizi wenye ufanisi katika sekta yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia ilishindilia sana katika kutuhimiza tusimamie suala la tafiti za kina. Katika hili wanaitakia GST iongezewe uwezo wa kufanya utafiti kwa kina zaidi. Katika kipindi hiki tulichoko Serikali kwa kushirikiana na wadau wametenga bilioni 53 kwa ajili ya kusaidia GST waweze kufanya tafiti za ki-geophysical kwa kutumia ndege na fedha hizi zitatusaidia kuongeza hii 16% ambayo imeeongelewa kwa muda mrefu kwa kuongeza 18% nyingine katika eneo ambalo limefanyiwa utafiti wa kina juu ya ardhi ya nchi yetu, hivyo kufikisha 34% ndani ya muda wa kipindi cha mwaka huu wa fedha mpaka mwaka ujao ili tufikapo mwaka 2030 walau ile 50% ya Vision 2030 iwe imefikiwa katika utafiti wa kina wa madini yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii ambayo tunaenda kuwaomba Waheshimiwa watupitishie, GST wametengewa zaidi ya shilingi 92,200,000,000 kwa ajili ya kuongeza tija katika utafiti wao. Tunakwenda kununua ndege, tunakwenda kutumia drone pia tutakuwa na ya kwetu kwa ajili ya utafiti wa kina na kununua vifaa mbalimbali vya kisasa sambamba na kujenga maabara ya kisasa ambayo inaendelea kujengwa hapa Dodoma na zingine za kikanda ambazo zinajengwa katika Mikoa ya Geita na pia katika Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ninasikia kama hiyo ndiyo kengele ya mwisho, itoshe tu kusema kwamba sisi kama Wizara tumepokea maoni ya Kamati yetu, tunayafanyia kazi, tuko tayari pia kuwasilisha kwa maandishi na haya yote ambayo Wabunge zaidi ya 20 waliyochangia leo hapa ndani tumenukuu na tunakwenda kutumia mawazo yao, ushauri wao na maoni kuendelea kuboresha utendaji wa sekta yetu hii ambayo ni tegemeo la uchumi wetu katika kutupatia fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Rais siku ile alipokuwa anazindua hili Bunge, alisema kwamba katika nyakati hizi za kuyumbishwa na yale mambo yaliyotokea Oktoba, sekta ambayo tunaitegemea itaibeba nchi hii ni sekta ya madini. Kweli wameona matokeo yake jinsi mapato yanavyopanda. Tunategemea kwamba tafiti hizi zitapokwenda kufanyika, sekta hii itakuja kuwa kinara katika kulijenga Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru kwa nafasi uliyonipa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)