Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SAIDI SALIM HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru nami kwa kunipatia nafasi hii. Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi. Pia ninaishukuru Kamati za Siasa kwa ngazi zote zilizonipitisha kuanzia mkoa na wilaya. Kipekee kabisa ninawashukuru wananchi wa Jimbo la Ole, hususan Wajumbe, wamekuwa wema kwangu, ni watu wazuri. Wajumbe hawa watakapokufa wote wataingia Peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa Wizara hii ya Vijana, ninatanguliza pongezi. Pongezi hizi ninazielekeza moja kwa moja kwa Wizara inayoongozwa na kaka yangu, Mheshimiwa Nanauka. Tarehe 4 Aprili, 2026 nilisimama ndani ya Bunge hili Tukufu kuchangia, nikauliza, kwa nini tusianzishe Benki ya Maendeleo ya Vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hilo leo katika wasilisho la Wizara hii, Mheshimiwa Waziri amesema sasa ni muda sahihi wa Serikali, kupitia Wizara ya Vijana, kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Vijana ili Vijana wa Kitanzania waende wakafungue akaunti zao, na wakafanye cash deposit hapo. Wakiwa wanahitaji kukopa, waende wakakope katika Benki yao ya Maendeleo ya Vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipa pongezi Serikali kupitia Wizara hiyo. Nasi mnatupa imani ya kutafuta fikra mbalimbali kuja kuishauri Wizara, kwani tumeona mawazo ambayo tunayaleta, yanachukuliwa, yanachakatwa na wakiona yanafaa, basi wanakuja nayo kwenye mikakati yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuipongeza Wizara ninaomba nichangie, kwa ruhusa yako, kuhusu fursa za vijana ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezitengeneza kupitia Wizara mbalimbali. Tunajua tuna Wizara ya Vijana ambayo ni mpya, lakini kuna fursa za vijana za kiuchumi na za kiajira kupitia Wizara mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, Wizara ya Uchukuzi kwenye Taasisi yetu ya DMI pale, Wizara hii imefanya taasisi zake ziwe za kushikana na kusaidiana. DMI imewezeshwa na TPA chini ya mwekezaji wetu DP World kununua simulator ya kisasa, ambayo inaitwa Full Mission Desk and Engine Simulator. Unaposoma DMI sasa hivi, ndani ya miaka hii miwili iliyopita, unasoma kupitia simulator hii na unapotoka pale unakuwa umebobea. Mtambo huu ambao uko pale ni nchi siyo zaidi ya tatu Afrika nzima ambazo tunaumiliki, tukiwemo na sisi Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, thamani ya mtambo huu ambao umenunuliwa chini ya Profesa Tumaini pale, una thamani ya Dola za Kimarekani 2.8 million. Huu umesababisha vijana wetu wa Kitanzania kwenda DMI, wanapata fursa za kielimu za kisasa na wanapotoka pale wanapata fursa za kiajira, dunia nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Taasisi ile ya DMI tulipokwenda kutembelea, Kamati ya Miundombinu, tumepata fursa za vijana zilizotengenezwa kupitia mtambo huu. Kuna meli za Kimataifa zimejikita sasa hivi kutaka kufunga mkataba na DMI kwamba, cabin crew yote na mabaharia wote wa meli hizo wawe ni vijana wa Kitanzania ambao wametoka pale DMI kupitia mtambo ule. Kwa hiyo, haya mambo hayatokei tu by nature, ni jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan chini ya Serikali yake, ambayo imewezesha kupata fursa kama hizi za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna fursa za vijana zilizoko katika Wizara ya Mawasiliano chini ya mama yetu Mheshimiwa Kairuki. Kuna huu Mfuko wa UCSAF, ambao unajenga minara, kama alivyozindua juzi pale Mheshimiwa Mama Samia. Mpaka sasa tumejenga takribani minara 2,151. Sisi tumebahatika kutembelea mnara mmoja tu, Kigamboni. Mnara huo umetengeneza fursa za vijana za ajira na kiuchumi, kama zifuatazo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnara ule wa pale Kigamboni ambao tumeenda kuutembelea umewezesha kuajiri au kujiajiri vijana 157 kama mawakala. Wamepata job opportunity kupitia mnara ule ambao umejengwa. Vilevile kuna vijana wa Bolt na Uber walikuwa pale hakuna network. Kwa hiyo, wanasema mtandao kulikuwa hakuna, walikuwa hawawezi kwenda kutoa service katika maeneo yale. Baada ya kujengwa mnara huu, vijana wetu wa Uber na Bolt wamejikuta wanaenda pale kupata riziki zao za kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukakutana na vijana ambao wamejiajiri kupitia online shopping pamoja na delivery services za online pia, nao wamejiajiri baada ya mnara ule kufika pale. Vilevile, tukakutana na wanafunzi ambao wanasoma chuo kikuu. Vijana wetu hawa ambao ni wasomi walikuwa wanapata shida ya mawasiliano wakiwa wako pale Kigamboni, walikuwa hawana network, wakati wa usiku wanasumbuka. Baada ya Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, kupeleka mnara huu, vijana hawa wamepata ajira, mawakala 157, Bolt wanaenda pale kujiajiri, online shopping wanafanya kazi zao na vijana wetu ambao wanasoma, wamejipatia fursa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kutembelea TCAA, kuna fursa iko pale Chuo chetu cha Mamlaka ya Anga Tanzania, fursa ya kipekee kabisa. Kuna kozi inatolewa pale inaitwa ni Aircraft Controller. Hii Aircraft Controller ambayo inatolewa pale, vijana wanatoka Somalia, tumekuta zaidi ya wanafunzi 70 na wengine 34 kutoka Uganda wanasoma kozi ile kwa thamani ya shilingi milioni 70. Ni kozi ya wiki saba, lakini Mheshimiwa Mama Samia katoa maelekezo kwa Mheshimiwa Prof. Mbarawa, Kijana wa Kitanzania anayekwenda kusoma Aircraft Controller ndani ya chuo hiki alipie shilingi milioni 10 tu. Hizi ni fursa ambazo ziko katika Wizara nyingine, lakini zinatufaa sisi vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaendelea kuchangia mchango wangu. Sisi vijana tulikuwa tunasikitika hapo zamani, zikitokea nafasi za jeshi tunatafutwa vijana; zikitokea nafasi za Polisi tunatafutwa vijana; zikitokea kazi ngumu za zege, tunawekwa vijana; lakini kazi za uongozi hatushirikishwi vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Bunge hili ambalo tupo, tuna Wabunge wa Vijana ambao ni Viti Maalumu na tuna Wabunge wa Majimbo ambao ni vijana. Leo ndani ya Bunge hili tuna Mawaziri ambao ni vijana. Leo ndani ya Bunge hili kuna Makatibu Wakuu, kuna Maafisa Mezani pale wote ni vijana. Haya ni maono ya Mheshimiwa Mama Samia kupitia kuwajali vijana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichangie kwa kusoma maneno matukufu kutoka katika Biblia. Methali 3:5-6 kuna maneno ya kumtia moyo Mheshimiwa Mama Samia, yanasema, “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atanyoosha mapito yako.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika Kitabu Kitukufu cha Quran kuna aya inayosema, “Isubiru wa Swabiur”. Ee Mama Samia Quran inakwambia; subiria na uvute kwenye subira. Pia kuna aya inasema, “Wa Bashir As-Sabireen.” Nimpe ishara njema Mheshimiwa Mama Samia, kwa anayoyasubiria ndani ya nchi hii. Mama fanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. SAIDI SALIM HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kuwa kunijaalia miongoni mwa watu ambao wako katika nyumba hii takatifu. Aidha, kwa vile ni mara yangu ya kwanza ninapenda kuchukua nafasi hii kukishukuru kwa dhati ya moyo wangu Chama changu Cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya Jimbo, Wilaya, Mkoa; ngazi ya Ofisi Kuu Kisiwandui, pamoja na Kamati Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wake mahiri, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ninachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Dkt. Samia kwa ushindi wa kishindo alioupata tarehe 29 Oktoba, 2025. Baada ya shukrani hiyo, ninaomba nichangie hoja iliyopo Mezani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu nitajikita kwenye mambo makuu mawili. Mambo haya yataelekea kwenye implementation ya bajeti yetu hii ambayo iko mezani kwa Mwaka 2026/2027. Jambo la kwanza, ili tuweze kufanikiwa katika bajeti yetu hii wachangiaji tumechangia tufanye investment kubwa kwenye masuala mazima ya kilimo, biashara na madini. Kwa uono wangu, ninapenda niongeze sehemu nyingine ya investment kubwa ambayo tunapaswa kuwekeza, ni katika vijana wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sensa vijana ni more than 75%, lakini rika la watoto baada ya miaka miwili au mitatu nao wana-turn kutoka kwenye childhood wanakuja katika rika la vijana, so in general vijana wanachukua namba kubwa ya watu katika Taifa hili. Tukiweza kuwekeza katika sekta hizi zinazowahusu vijana tutaweza kuchangia pato la nchi hii na kuchangia katika bajeti yetu hii kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuwekeza kwa vijana kupitia elimu, habari, teknolojia na michezo. Kupitia elimu vijana tunawasomesha masomo ya physics, biology, chemistry, history na masomo mengine mbalimbali, lakini kuna wimbi kubwa la vijana akili zao zimekita sana katika masuala ya michezo. Ninaishauri Serikali tuanze kuwekeza kupitia sports academies. Michezo sasa hivi ni biashara kubwa sana na tayari inachangia mapato makubwa katika mataifa ambayo yameendelea kwa kuajiri wachezaji wa mipira na michezo mbalimbali duniani na kuweza kupata mapato mbalimbali katika Taifa husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, iwapo tutaanzisha hizi sports academies kuanzia ngazi za watoto hadi vijana, vijana wetu wengi wataweza kujiajiri na kuajiriwa kupitia hii sekta ya michezo. Hata hivyo, tunapaswa kuwekeza kuanzia kwenye shina. It means tuajiri walimu professional, kwa ajili ya michezo, ambao wataweza kusomesha watoto kuanzia ngazi za nursery, primary, secondary na hata ngazi za vyuo vikuu kuwe kuna syllabus kabisa ya kusomesha haya masuala ya michezo, ili tupunguze wimbi kubwa la vijana ambao hawana ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo litatuwezesha kupata fedha zaidi katika zoezi letu hili la bajeti ambalo tunakwenda nalo sasa hivi ni kupitia habari. Tumemwona Mheshimiwa Waziri Makonda, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi bilioni mbili kuwawezesha content creators, hii ni ajira kubwa sana kwa vijana. Kama tutaweza kuwa-facilitate vizuri, Mama kaleta hizi shilingi bilioni mbili zikiweza kutumiwa very effectively basi zitakuza kipato cha vijana wetu kutoka hatua moja kwenda nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hili ninashauri kwa vile tuna benki mbalimbali hapa kwenye nchi yetu, tuna benki ya kilimo tumeianzisha. Kwa nini tusianzishe benki ya maendeleo ya vijana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili hizi fedha ambazo zimetengwa, shilingi bilioni mbili, kupitia Wizara ya Habari, first ziwe deposited pale kwenye benki yetu, kwa ajili ya vijana. Tumesikia Mheshimiwa Rais kupitia Waziri wetu wa Vijana ambapo katuwekea Mheshimiwa Nanauka pale, katenga shilingi bilioni 200, kwa ajili ya kuwawezesha vijana. Kwa nini fedha hizi zisiwe first deposited kupitia benki yetu maalum ya vijana, ili vijana waweze kwenda kutumia fedha hizi katika sehemu zao maalum na wakitaka mikopo, wakitaka kuwa-facilitated kwenye mambo yao mbalimbali vijana hawa waweze kwenda kuchukua pale kwenye benki yetu hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kupitia maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili tuweze kukuza uchumi wetu na kuweza kupata fedha ambazo zitasababisha bajeti yetu kukua siku hadi siku na uchumi wetu kupanda, kama ilivyo nchi yetu uchumi wake unakua kwa kasi zaidi na tunawekeza pesa nyingi kupitia sekta ya ujenzi, uchukuzi na miundombinu. Hapa Serikali kwa mwaka tuna-allocate billions of money ambazo zinaenda kujenga miradi mbalimbali katika Taifa letu, lakini katika fedha hizi ambazo zinaenda kuwekwa pale tunaenda kukuza uchumi wetu at the same time tuna-facilitate uchumi wa nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapo-compete kampuni za international na kampuni zetu local tunashindwa kushindana na kampuni zile zinazokuja kutoka nje ya nchi kwa sababu kuu tatu; kampuni zinazokuja kutoka nje ya nchi zinatushinda technical, financial na working experience. Zikija tukikaa nazo mezani, tuki-bid nazo pamoja, hizi kampuni za ujenzi na kujenga miundombinu mbalimbali zinashinda zile tenda. At the same time tunatumia fedha, billions of money ambazo Mheshimiwa Samia ana-allocate kupitia Wizara hizi kujenga miundombinu ya nchi yetu, lakini tunakwenda kuchochea uchumi wa nchi nyingine kwa sababu, zile kampuni zinapopata tenda ndani ya nchi yetu zina-take profit from these tenders and then wanaenda kujenga kwenye mataifa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa ninaishauri Serikali, ili tupate fedha hizi ziweze kukuza uchumi wetu, lakini vilevile iwe ni sababu ya ku-facilitate ukuaji wa maendeleo kwa jamii yetu. Tutengeneze mazingira rafiki kwa kampuni zetu za ndani ziweze ku-compete kuanzia internally mpaka externally. It means hapa, kama Serikali, tutatenga fedha tuzi-fund hizi kampuni. Kama tutakaweka Sheria fulani, let’s say imekuja kampuni kubwa kutoka China, imekuja kujenga flyover hapa, tukaweka Sheria kupitia kampuni hii ambayo imekuja, basi ifanye joint venture na kampuni yetu local.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke Sheria kama hii, kazi total ni shilingi bilioni 200, lakini you must give sub-contract from a local company, ili kupitia sub-contract hii ambayo itapewa hii local company kuna mambo tutaweza kuya-gain. Tutaweza ku-gain experience from international company, lakini ile kampuni yetu ambayo ni local, instead ya kukaa bila kuipata ile kazi kubwa itakuwa nayo imepata kazi; itaweza kuajiri vijana mbalimbali na hawa Gen-Z ambao wako mtaani ambao wanamnyima usingizi Mama Samia, mama anapenda kuwaona vijana wake wamepata ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili apate usingizi mnono basi ni lazima tuwezeshe kampuni zetu za ndani, mama aweze kulala aone vijana wake wote wamepata ajira kupitia kampuni hizi za ujenzi ambazo zinakuja kufanya miradi mbalimbali. Tutapata experience na ile key personnel, wale technical staff ambao tuponao wakishirikiana na technical staff kutoka kampuni kubwa watajenga technics ambazo wanazitumia ku-complete hizo project kubwakubwa na mambo mengine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie kuchangia kwangu katika hoja hii kwa kusema maneno matakatifu kutoka katika Vitabu Vitakatifu. Ninaanza kunukuu kutoka Kitabu Kitakatifu; Ayubu 42:2 anasema; “Ninajua ya kuwa, wewe waweza kufanya mambo yote na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuiliwa.” Kwenye Qurani kuna maandiko yanasema, “Qaddara Allahu wamaa shaa fa’ala.” Vilevile, kuna aya inasema; “Innama amruhu idha araada Shay’an an yaquula lahu kun faya kun.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba Watanzania wamwachie mama afanye kazi. Mama yupo kazini amesimamishwa kwa kadari ya Mwenyezi Mungu na hawezi kutetereka isipokuwa kwa kadari ya Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)