Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haran Nyakisa Sanga (3 total)

MHE. HARAN N. SANGA aliuliza: -

Je, lini wafanyakazi wa Tanzania watapunguziwa riba ya mikopo na kufikia asilimia saba au nane?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge wa Kigamboni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na sera za uchumi wa nchi yetu, riba za mikopo zinazotolewa na taasisi za fedha nchini kwa wateja mbalimbali, ikiwemo wafanyakazi huamuliwa na soko (market determined). Hivyo, Serikali inaona kuwa kuelekeza taasisi za fedha kuweka viwango vya riba vya asilimia saba au kiwango chochote mahususi au maalumu kwa ajili ya wafanyakazi itakuwa inakinzana na maelekezo ya sera za soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatambua kuwa swali hili lina msingi wa kwamba taasisi za fedha, maeneo pekee ambayo yanapata faida kwa kukopesha ni kwa watumishi ambao mishahara yao kukatwa ni rahisi. Hata hivyo, taasisi ya fedha inaweza kuweka kiwango cha riba kwenye mikopo ya wafanyakazi au mkopaji yeyote kufikia asilimia saba au pungufu ya hapo, kama itaona inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, wafanyakazi au mkopaji yeyote anaweza kukubaliana na taasisi ya fedha na kupata kiwango cha riba cha asilimia saba au pungufu kwa kadri itakavyowezekana. Vilevile, wafanyakazi kupitia waajiri wao wanayo fursa ya kuwasiliana na benki husika na kukubaliana riba wanayoweza kutoza wafanyakazi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. HARAN N. SANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakuja na mpango wa pamoja ili kutoa suluhu ya mageuzi ya sekta binafsi katika kukuza uchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge kutoka Jimbo la Kigamboni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imekamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia takribani 70% ya ukuaji wa uchumi. Ili kufanikisha azma hiyo, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inaendelea kukamilisha Mpango wa Pili wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II). Pia, inaandaa sera mpya ya uwekezaji na mkakati wake wa utekelezaji, kwa lengo la kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki zaidi kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2026/2027 imepanga kuandaa sera, sheria na mkakati wa kukuza sekta binafsi, pamoja na kuandaa mwongozo wa kupima utendaji wa sekta binafsi, mwongozo wa upimaji wa mchango wa sekta binafsi kwenye 70% ya uchumi na mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa takwimu za biashara na uwekezaji. Ofisi pia itaendelea kuimarisha majukwaa ya sekta binafsi kupitia Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Vitengo vya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ngazi za mikoa na Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali inapanga kufungua One Stop Facilitation Centres katika kila Mkoa na Wilaya ili kurahisisha mazingira ya biashara na uwekezaji ngazi ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla, Serikali inaichukulia sekta binafsi kama mshirika mkuu wa maendeleo ya Taifa na itaendelea kuweka mazingira rafiki, thabiti na yenye kutabirika ili sekta hiyo ikue, izalishe zaidi, iongeze ajira, ipanue wigo wa kodi na hatimaye kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. HARAN N. SANGA aliuliza:-

Je, kuna tofauti gani kati ya Daraja la Tanzanite na Daraja la Mwalimu Nyerere Kigamboni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge wa Kigamboni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitaalam Daraja la Kigamboni ni Cable Stayed Bridge lenye urefu wa meta 680 ambalo lilijengwa kwa makubaliano maalum kati ya Serikali na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Katika makubaliano hayo, Serikali ilichangia 40% ya gharama za ujenzi na NSSF ilichangia 60%. Aidha, ilikubalika kuwa daraja hilo litakuwa la kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Tanzanite kitaalam ni Extradosed Bridge lenye urefu wa kilometa 1.03 ambalo lilijengwa na Serikali kwa utaratibu wa kawaida na kwa sasa siyo la kulipia. Ahsante.