Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haran Nyakisa Sanga (4 total)

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze tu majibu ya Serikali, lakini nataka kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, benki zetu zinazoitwa commercial banks zinategemea vitu viwili katika kufanya biashara, kwa kutumia consumers’ loan na Government Bond, kwa sababu hivi vitu vyote vina security kwao. Kwa Serikali kuacha watumishi ambao wamekuwa wakitumikia miaka yao 55, 60 mpaka 65, amekuwa akifanya kazi za Serikali, kwa sababu tunaamini kabisa watumishi wa Serikali siyo wafanyabiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mshahara wake ndicho kitu pekee ambacho anakitegemea ili aweze kupata mkopo aweze kujenga nyumba, apate mkopo aweze kutengeneza maisha yake ya kujikimu kwa ajili ya kustaafu. Je, Serikali ina kauli gani ambayo itawasaidia watumishi hawa kuanza kuwa-motivate katika kufanya kazi, na pia kuwasaidia kwamba watapokuwa wanastaafu, wawe na maisha bora ya kujikimu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Sanga, anauliza maswali haya bila shaka ni kutokana na kwamba wafanyakazi hawa ni dada zetu, ni kaka zetu na wengine ni wanetu. Kwa hiyo, maisha yao na matumaini yao ya kuishi kwa kufanya kazi, mwisho wa siku yawe na faida kwao. Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi ya kifedha kwa watumishi kama ambavyo imekuwa ikifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliunda mfuko maalum wa Advances Fund kupitia Tangazo la Serikali Na. 709 lililotoka mwaka 2018 likisomeka kama “Advances Fund Establishment Order.” Lengo kuu la kuanzishwa mfuko huu ilikuwa ni kuwezesha utoaji wa mikopo kwa watumishi wa umma kwa masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Advances Fund huwa inatozwa kwa gharama ya jumla ya asilimia nne, ambayo kimsingi huwa ni kwa ajili ya services charges na bima tu ya huo mfuko. Mpango huu unawahusisha wafanyakazi au tuseme watumishi wa umma, kwa maana ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na utekelezaji wa utaratibu huu, Serikali ilielekeza taasisi nyingine za umma kuanzisha mifuko yao ya ndani ya utoaji mikopo kwa watumishi wao kwa lengo la kuhakikisha wanapata mikopo yenye masharti nafuu na hivyo kuwezesha kuimarisha ustawi wa uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2021 hadi Januari, 2026 watumishi hao wamekopeshwa zaidi ya shilingi bilioni 497, lakini kwa kipindi cha mwaka 2025/2026 pekee watumishi wamekopeshwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 74.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, watumishi hao wataendelea kuishi kwa matumaini na watastaafu wakiwa wanawezeshwa na Serikali, na bila shaka mpango huu utaendelea kufanyika na jitihada nyingine za kuwezesha wafanyakazi waweze kuwa na maisha mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa mtandao wa barabara kilometa kama 45, lakini naomba niulize swali tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata wakandarasi sita ambao wanatekeleza utengenezaji wa zile barabara za DMDP, lakini toka nimefanya ziara ni miezi minne sasa hivi wameingia site, wengine wameweka vifaa, lakini hawapo site hadi sasa hivi tunavyoongea hapa na kila ukiwauliza wanazungumza wanasema labda fedha hazijatoka.

Sasa tunaomba kauli ya Serikali, ili wananchi wale waweze kupunguziwa adha ya zile barabara walizokuwa wamezitindua maana zinakwamisha upitaji. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Sanga, Mbunge wa Kigamboni na bahati nzuri alipata ziara ya Waziri wetu, alifika kule na akajionea barabara hizi. Pia namhakikishia Mheshimiwa Sanga, mimi na yeye baada ya hapa tuwasiliane ili tuone fedha hizi ambazo Serikali imeshazielekeza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizi kilometa 45. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali, lakini ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa, uchumi jumuishi ni mfumo wa uchumi unaohakikisha kila mtu ananufaika na maendeleo ya kiuchumi. Je, wananchi wa Kigamboni wananufaika vipi na uchumi jumuishi kama Serikali haijaweka kwenye mpango ujenzi wa Barabara ya BRT kutoka Kongowe - Mji Mwema - Feri na barabara ya lami kutoka Feri kwenda Pemba Mnazi ili vijana wa bodaboda, vijana wa mamalishe, machinga wa Kivukoni pamoja na Pemba Mnazi, Wavuvi wa Gezaulole, Wakulima wa Mbogamboga Mtaa wa Sala na Kibada waweze kunufaika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninataka kujua ni lini Serikali itaanza kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira bora ya biashara MKUMBI II kwa maana ya kutoa utitiri wa leseni za biashara kwa wafanyabiashara hususani wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Haran Nyakisa Sanga, Mbunge kutoka Jimbo la Kigamboni kwa maswali yake mazuri mawili, pia Mheshimiwa Haran ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na amekuwa akichangia sana suala la uwekezaji hususani Kigamboni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo ninaomba nijibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, ni kweli Dira yetu ya 2050 na mpango wetu wa miaka mitano wa 2026 - 2030 umezingatia kwamba tunahitaji kuja na uchumi jumuishi. Katika hili ninatambua kwamba Kigamboni ni eneo ambalo ni very potential kwa uwekezaji na tuna wawekezaji wengi sana wameweka viwanda Kigamboni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia hili sisi kama Serikali na ndiyo maana kwenye mpango wa miaka mitano tumwekea kipaumbele kuboresha mazingira rafiki hususani miundombinu ya barabara, vilevile BRT kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapovutia wawekezaji katika maeneo yale, wawe tayari kwenda kwa ajili ya kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mbunge tumepokea hoja yake na sisi kama Serikali tutaiingiza kwenye mpango yetu tuhakikishe kwamba wale wawekezaji ambao wanataka kwenda kule waweze kwenda na tuweze kupata manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni kuhusu MKUMBI II ni kweli kama Serikali tayari tupo mbioni kukamilisha utengenezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na tayari huu mpango ulishapitia katika uhakiki Mheshimiwa Rais kutoka Zanzibar alikuja kwa ajili ya mapitio na tunategemea mwezi ujao tutazindua huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwa kupitia huu mpango tunaenda kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hususani kupunguza utitiri wa kodi, tozo, lakini urasimu ambao unaendelea katika kukuza sekta binafsi. Ninaomba kuwasilisha. (Makofi)

MHE. HARAN N. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niseme sijaridhika na majibu ya Mheshimiwa Waziri, kwa sababu haioneshi utofauti wa Daraja la Kigamboni na Daraja la Tanzanite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoelewa mimi, haya madaraja yote yamejengwa kwa fedha za mkopo, lakini pia Serikali inahusika katika kulipa ile mikopo ambayo imetumika katika kujenga haya madaraja. Ukianza kuangalia Serikali hapa imechangia 40% na NSSF imechangia 60%. Wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakilia sana kulingana na tozo zinazotolewa pale darajani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri; je, Serikali iko tayari kutoa 40% kama sehemu ya huduma, ikabaki 60% ili kushusha tozo inayotolewa pale Kigamboni? (Makofi)

Swali la pili, wananchi wa Kigamboni wamechangia sana tozo pale darajani. Nini kauli ya Serikali kufuta tozo kabisa ili waendelee kupita kama wanavyopita watu wa Tanzanite? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza si vyema kulirudia swali kama lilivyoulizwa. Swali liliulizwa nini tofauti kati ya Daraja la Tanzanite na Daraja la Kigamboni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa tofauti hiyo, kwanza kitaalamu kwa maana swali liko hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, kuna tofauti gani kati ya Daraja la Tanzanite na Daraja la Mwalimu Nyerere Kigamboni. Tumetoa tofauti kitaalam kwa maana ya ujenzi ilivyojengwa, lakini pia operations zake zinafanyikaje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niliweke wazi hivyo, ili sijui, lakini ndiyo swali lilivyoulizwa.

Sasa naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na maelezo yako, ndiyo maana wakati mwingine tunaruhusu maswali ya nyongeza ambayo yako chini ya Wizara yako, ambayo unaweza kuyajibu. Yale ambayo unaweza kuyajibu, unayajibu hapo, yale ambayo huna majibu basi utayeta majibu baadaye. Kwa hiyo, naomba ujibu maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi mwelekeo wa Serikali na hata mwelekeo wa Dira ya 2050 ni 70% private sector na 30% Serikali na huko ndiyo maana hata leo, tunafikiria kujenga barabara ya kutoka Kibaha kuja Chalinze, kuja Morogoro ikiwezekana mpaka Dodoma kwa Mpango wa PPP ambazo hizo barabara zitakuwa ni za kulipia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa NSSF sisi tunasema tuna kivuko ambacho tunasema ni daraja linalotembea na hili daraja lingine la Kigamboni Serikali iliingia ubia na wenzetu wa NSSF na ndiyo maana likawa la kulipia tangu mwanzo. Hili Daraja la Kigamboni ambalo lililinganishwa tumesema ni kama madaraja mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge maoni hayo tumeyapokea na tutakwenda kuyafanyia kazi, lakini niwajulishe tu Waheshimiwa Wabunge tunakoelekea sasa hivi hata kwenye barabara na nchi zingine sasa hivi ni PPP na ndiyo utaratibu ambao hata Mheshimiwa Rais ametuelekeza tuanze kufanya kazi na wenzetu wa private sector, ahsante.