Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ibrahim Mohamed Shayo (7 total)

MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, Moshi ni Mji ambao ulikuwa na viwanda vingi sana, lakini viwanda vile sasa hivi vimekufa na vimechukuliwa na wawekezaji na wale wawekezaji hawawekezi wamevichukua tu kama magofu. Ni lini Serikali itaweza kuwanyang’anya viwanda vile na kuvifanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilivitoa viwanda hivi kwa wawekezaji kwa nia ya uzalishaji. Mkataba wa makabidhiano wa viwanda hivi kwa hao wawekezaji unawataka wauheshimu kwa maana ya kuendelea na shughuli za uzalishaji. Ndiyo maana kwa Moshi kuna Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools ambacho mimi mwenyewe nilikuwa pale wiki mbili zilizopita kazi za uzalishaji inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maeneo mengine ambayo wawekezaji wamepewa viwanda hivi na havizalishi, rai yetu ni moja tu kuwaambia kwamba, aidha warudi kwenye uzalishaji ama Serikali itachukua hatua ya kuwapatia viwanda hivyo wawekezaji ambao wana nia ya dhati ya kushiriki katika ujenzi wa Dira ya 2050 kwenye Uchumi wa Viwanda na Uzalishaji kwa ajili ya shughuli ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao yetu.
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninaomba niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Barabara ya Maili Sita – Kiboriloni ujenzi wa njia nne utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kuianza hiyo barabara, kwa sababu ni barabara ambayo inaanzia Tengeru inakwenda Kikafu – Maili Moja – Kiboriloni kwa njia nne. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko kwenye hatua za mwisho kabisa ili barabara hiyo ianze kujengwa. (Makofi)
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana, ulipokuja Moshi uliwaahidi wananchi wenzangu wa Moshi kwamba Serikali itakwenda kujenga mortuary ya kisasa. Je, ni lini mortuary ile inakwenda kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ibrahim, Mbunge wa Moshi kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwapigania wananchi wa Moshi. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekwishakupeleka shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mortuary pale Moshi na mkandarasi ameripoti site wiki iliyopita na tumesema kwa kazi nzuri aliyofanya Mheshimiwa Mbunge pindi ujenzi utakapoanza atakwenda yeye mwenyewe kuweka jiwe la msingi katika mortuary ile ya Hospitali ya Mawenzi.
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa kuuliza swali dogo. Mheshimiwa Naibu Waziri, Moshi ulikuwa ni Mji mwenye viwanda vingi sana, lakini kwa sasa viwanda vyetu Moshi vimekufa na vilivyokuwa vimebinafsishwa waliobinafsisha wameingia mitini. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba tunakwenda kuanzisha viwanda vipya na kufufua vile ambavyo vimekufa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mbunge kutoka Moshi Mjini kwa maswali yake mazuri na nilifanya ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Moshi Mjini, mojawapo ya changamoto ambayo alii-raise Mheshimiwa Mbunge ni suala la viwanda ambavyo vilikuwepo kule ambavyo kimsingi havifanyi kazi, lakini vilevile mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunakuja na viwanda vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Moshi ni mojawapo ya maeneo yetu ambayo tumeya-target kwa ajili ya kukuza viwanda hususani kwenye upande wa kilimo, vilevile kwenye viwanda mbalimbali vya manufacturing. Ninaomba nimhakikishie kwamba hoja yake tumeichukua na katika mipango yetu tutaipa kipaumbele. Ninashukuru sana.
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri umekuwa ukiniambia kila siku tarehe 01 Juni, mkandarasi ataingia site kuhusu barabara ya Mailisita kuelekea Kiboroloni ya njia nne. Je, ni lini unawaambia wananchi wa Moshi Mjini mkandarasi ataingia site?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI K.n.y WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Shayo kwa jinsi ambavyo anakumbushia barabara hii. Endelea kuvuta subira Mheshimiwa Shayo, tunakamilisha taratibu za kifedha ndani ya Serikali kama ambavyo Serikali hii imefanya mengi kwenye Jimbo la Moshi na wewe unafahamu kwenye uwanja wa ndege tumepeleka mabilioni pale, nataka nikuhakikishie hata hii vuta subira tutakwenda kufika na wananchi wa Moshi watafurahia.
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Moshi Mjini kuna madaraja mawili; daraja la kwanza lipo Kata ya Ng’ambo na daraja la pili lipo Kata ya Mji Mpya. Madaraja yale kutokana na mvua hizi, ni mabovu sana. Je, ni lini Serikali itakwenda kuyarekebisha madaraja haya ili wananchi wale wawe salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Shayo, Mbunge wa Moshi Mjini kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na madaraja na kuyatengeneza mara kwa mara. Ninafahamu Mheshimiwa Mbunge ana changamoto ya Daraja la Kata ya Ng’ambo ambalo limekatika siku chache zilizopita na kuathiri mawasiliano kutoka kata hiyo kwenda kata za jirani. Ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali hii itafuatilia kuhakikisha kwamba tunafanya matengenezo mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kumwelekeza Meneja wa TARURA, Wilaya ya Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro wafike eneo la site wafanye tathmini mapema iwezekanavyo ili tupate fedha za dharura kwa ajili ya kurekebisha hali hiyo. (Makofi)
MHE. IBRAHIM M. SHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi, kuna Mradi wa TACTIC wenye gharama ya shilingi bilioni 22.9 barabara ya kilometa 13.3 ambao uko Mjini Moshi. Mradi huu mkandarasi anautengeneza kwa kusuasua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kauli Serikali kuhusu mradi huu kuweza kwenda kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA, SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa TACTIC katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa Mheshimiwa Mbunge Ibrahim ni moja ya miradi 45 inayotekelezwa na Serikali, na ni kweli kwamba tumekwishapata mkandarasi lakini utekelezaji au kasi ya utekelezaji wa mradi ule hairidhishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kupitia TARURA tumekwisha mwelekeza; kwanza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, lakini na timu yetu ya wataalam ikae na mkandarasi mapema iwezekanavyo tuweze kuona nini changamoto ya mkandarasi ili tuweze kuchukua hatua ikiwemo na ikiwezekana kuvunja mkataba kwa kadri ya vifungu vya mkataba au kuhakikisha anaanza kufanya matengenezo ya barabara hiyo ili iweze kukamilika kwa mapema iwezekanavyo.