MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga mnara wa mawasiliano katika Vijiji vya Kazamoyo, Imani na Kilimani katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Fadhili Sandali Chilombe, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka minne jumla ya minara 1,041 imejengwa na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi. Kati ya minara hiyo, minara 758 imejengwa kupitia Mradi wa Tanzania Kidigitali ambao ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais, tarehe 13 Mei, 2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) inaendelea na jitihada za kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyosalia ambapo tarehe 5 Desemba, 2025 mikataba ya kufikisha huduma za mawasiliano katika Kata 201 ilisainiwa na utekelezaji wake unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2027.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, Serikali kupitia UCSAF imepanga kufikisha huduma hizo katika maeneo mengine 280, yakiwemo maeneo ya kimkakati kama vile reli ya kisasa, hifadhi za Taifa, barabara kuu na maeneo ya mipakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na taasisi zake na makampuni ya simu, inaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Miaka Mitano (2025 – 2030) wa ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu wenye lengo la kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Lukumbule ina minara minne ya mawasiliano iliyojengwa na Makampuni ya Simu ya VIETTEL (mnara mmoja) na TTCL (minara miwili) pamoja na mnara wa Helios Towers Tanzania ambao Vodacom, Airtel na Honora wanautumia kwa pamoja kwa kuweka vifaa vyao vya mawasiliano. Aidha, kutokana na changamoto ya mawasiliano katika Kata hiyo, Vijiji vya Kazamoyo na Imani vimejumuishwa katika mradi wa mawasiliano vijijini, awamu ya tisa unaotekelezwa na Wizara. Usanifu wa minara katika vijiji hivyo umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza mapema Februari, 2026 na kukamilika mwishoni mwa Mei, 2026, ambapo wananchi wataanza kunufaika na huduma za mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kilimani kitapata mawasiliano kupitia mnara wa Kazamoyo mara utakapokamilika. (Makofi)