MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwenye Jimbo la Tunduru Kusini, ninakotokea, kuna barabara kuu mbili ambazo ni muhimu sana kwa uchumi wa eneo lile. Barabara ya kwanza inaanzia Misechela – Namasakata – Tuwemacho mpaka Mjini; na ya pili inaanzia Mtina – Nasya – Tuwemacho mpaka Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara hizi kila moja ina eneo korofi. Kwa mfano, hii inayoanzia Mtina – Nasya kuna eneo linaitwa Lamitado, pana kipande cha kilomita kama moja hivi ambayo mvua ikinyesha korosho hazipiti pale, magari yanalala pale hata siku tatu, siku nne. The same kwa upande wa Namasakata, kwenye Daraja linaloanzia Namasakata kwenda Chemchem, kuna kipande kina changamoto ambapo korosho ndiyo zinatoka nyingi, lakini huwa tunapata tabu kuzipitisha pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kupata Kauli ya Serikali, ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, maeneo yale yanapata suluhisho la kudumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru Kusini, jana wakati anatoa hoja hapa alitoa elimu kubwa sana ya umeme kwa Mheshimiwa Ado Shaibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hizi za Tunduru Kusini, maeneo yote korofi sisi tunayafahamu na tunakwenda kuyafanyia kazi. Tumefanya hivyo kwenye maeneo mengi ya nchi yetu kwa kutumia miradi mbalimbali, ukiwemo Mradi wa Agri Connect, pamoja na Mradi wa Rise. Vivyo hivyo, tutaangaza macho kwa ajili ya wananchi wa Tunduru Kusini. (Makofi)
MHE. ENG. FADHILI S. CHILOMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina swali moja lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni pamekuwa na ongezeko kubwa sana la watumiaji wako wa simu kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Jimbo la Tunduru Kusini, hali hiyo imesababisha baadhi ya minara kuzidiwa na ubora wa mawasiliano kutoka kwenye minara hiyo kupungua.
(a) Je, Serikali haioni haja ya kwenda kufanya review, kwa maana ya mapitio kwenye baadhi ya minara ili kuangalia uwezekano wa ama kuongeza masafa au kujenga minara mingine karibu na maeneo hayo?
(b) Je, kama inakubaliana na mimi, kazi hiyo itaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mhandisi Fadhili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kufanya tathmini upya ni kweli baadhi ya minara kutokana na kuongezeka kwa watumiaji inakuwa inazidiwa. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA kutuma wataalam katika maeneo ya Jimbo la Tunduru Kusini ili wafanye tathmini na kubaini changamoto hiyo haraka iwezekanavyo. (Makofi)