Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Faraji Buriani Nandala (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niwe miongoni mwa vijana watakaoweza kuchangia kwenye hotuba hii ya Mapato na Makadirio ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni kijana, na ninafurahi sana leo hii kupata nafasi niweze kuchangia hotuba hii, kwa sababu kama nisingechangia ningeona kabisa sijitendei haki mimi mwenyewe, na pia siwatendei haki vijana wengi wa Kitanzania waliojenga imani kwa Wabunge vijana tuliomo humu Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na mapenzi yake ya dhati kabisa ya kutaka kuona vijana wa Kitanzania wanapata maendeleo, na kwa kuanzisha Wizara hii inayohusiana na maendeleo ya vijana na kumteua kaka yangu Mheshimiwa Joel Arthur Nanauka awe Waziri kwenye hii Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi wangu huo, ninaomba nichangie hoja. Moja ya ajenda ambayo sisi Wabunge hasa wa Chama cha Mapinduzi ilikuwa inatupatia mileage kubwa kwa kundi kubwa la vijana ni kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, tulipokuwa kwenye kampeni zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi walikuwa na matumaini makubwa sana kuhusiana na ahadi hii ya Mheshimiwa Rais ya kutoa fedha shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kwenda kusaidia shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Imani hiyo ambayo vijana hawa walikuwa nayo walikuwa wanategemea kabisa kwamba hii Wizara sasa inakwenda kutatua changamoto zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kutoa zile fedha shilingi bilioni 200, tunamshukuru sana kwa kutimiza ahadi yake na tunajua huyu Mheshimiwa Rais ni mtu wa kutimiza ahadi, akiahidi anatekeleza. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na vijana wengi tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hizi fedha kutolewa na kukabidhiwa kwenye hii Wizara husika, bado malalamiko yamezidi kuwa mengi sana kwa vijana wengi. Lazima tuwe wakweli na tuelezane ukweli. Moja ya changamoto ambayo vijana wanalalamika ni urasimu, lakini kitendo cha hizi fedha kugawiwa kwenye Wizara nyingine za kisekta, kumeendelea kurudisha urasimu ambao vijana wengi wamekuwa wakilalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi vijana tulitegemea kwamba fedha hizi zitabaki kwenye Wizara ya Vijana na Waziri wa Vijana ndiye atakuwa na dhamana ya ku-coordinate na kusimamia fedha hizi ili kesho na keshokutwa tuweze kumwajibisha, tumwulize fedha hizi zimekwenda wapi, na zimetumikaje? Kwa hiyo, kitendo cha kuzitawanya ama kuzitapanya kwenda kwenye Wizara nyingine, kumeendelea kurudisha urasimu ambao vijana wengi wamekuwa wakipinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko haya hasa vijana wa vijijini, kwa mfano mimi ninatoka Jimbo la Ndanda. Vijana wa Msikisi, Mnawatutwe, na Chiwale wanalalamika kuhusiana na hizi fedha za shilingi bilioni 200 kwamba, kwanza hawana taarifa, lakini pia hawajui mchakato mzima wa hizi fedha wanazipataje? Hii inapelekea hali ya idadi ya vijana walioomba hii mikopo kuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa takwimu, idadi ya vijana walioomba fedha hizi za shilingi bilioni 200 ni vijana 30,384. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi vijana ambao walilengwa kwenye hii mikopo wa kuanzia umri wa miaka 15 hadi miaka 35 wanakadiriwa kuwa milioni 21 mpaka milioni 20. Sasa, hii idadi ya vijana 30,384 ni sawa na 0.12%, yaani hatujafikia hata asilimia moja ya vijana ambao walilengwa kwenda kupata hii mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa hapa tumefeli, na lazima tukubali kwamba tumefeli, kwa sababu, lengo lilikuwa ni kuwafikia vijana wengi, lakini vijana walioomba ni wachache. Ile nguvu tuliyoitumia katika kuitangaza hii mikopo kwenye majimbo yetu hatujaitumia hii nguvu kuwafikia na kuwapa taarifa vijana wengi hasa wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali, kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kutaka kuwasaidia vijana wa Kitanzania kwenye hizi fedha za shilingi bilioni 200, kwanza, Wizara ya Vijana kupitia kaka yangu Joel Arthur Nanauka mfanye upya review ya ushiriki wa hizi Wizara ambazo fedha zimepelekwa. Je, walishiriki ipasavyo katika kufikisha taarifa kwa vijana? Kama taarifa ikionekana kwamba hizi Wizara hazikushiriki vizuri, basi fedha hizi zirudishwe kwenye Wizara ya Vijana, zitafutiwe namna nyingine ya kuweza kugawanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, muda uliotumika kutangaza hii mikopo ni siku chache sana. Tangazo limetoka tarehe 21 na tarehe 3 Aprili, 2026 ilikuwa ndiyo deadline ya hii mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wengi biashara zao siyo rasmi, hazijarasimishwa, hawana leseni, hawana TIN Number lakini muda huu mchache kijana huyu anawezaje kupata muda wa kuandaa biashara yake, atafute TIN Number, atafute leseni, aombe mkopo kisha apate? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tulikuwa tuna dhamira ya kuwasaidia vijana, tungeangalia changamoto za vijana katika muda ambao wangeweza kuandaa biashara na kuomba huo mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masharti yanayotumika katika huo mkopo, kwanza uwe na TIN Number, uwe na leseni. Vijana wengi wa kijijini kwangu kule Mpanyani, na Chiwale biashara zao siyo rasmi, wanafanya biashara ndogo ndogo, hawana TIN Number, hawana leseni. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali kupitia Wizara ya Vijana, wafanye review upya ya hii mikopo ya shilingi bilioni 200 ili tuweze kuwafikia vijana wengi wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itapendeza, kwa nini hii mikopo isigawanywe kwa mtindo wa majimbo? Kwa sababu Tanzania hapa tuna majimbo 272, kama hizi shilingi bilioni 200 zingegawanywa kwa majimbo 272, inamaanisha kila jimbo lilikuwa lina uwezo wa kupata fedha shilingi 735,294,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ningepata hizi fedha shilingi 735,294,000 ningezigawanya kwenye kata zangu 16, na kila kata ingepata shilingi 45,955,000. Kama ningegawanya kwenye vijiji 70 vilivyopo kwenye Jimbo langu la Ndanda, inamaanisha kila Kijiji kilikuwa kinaweza kupata shilingi 10,500,000. Inamaanisha kila Kijiji kilikuwa kina uwezo wa kutoa vijana watano ambao wangeweza kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kuwa Tanzania tuna vijiji visivyopungua 12,318, tungezidisha mara 350, maana yake vijana 4,311,000 wangenufaika kupitia mikopo, kuliko huko hizo fedha zilikopelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kumsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuje na huu mfumo kugawa hizi fedha kupitia majimbo badala ya kuzitawanya kwenda kwenye Wizara na kurudisha urasimu ambao vijana wengi hawahitaji fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niwe miongoni mwa wachangiaji kwenye Hotuba hii ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa na Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Aweso na Naibu wake Mheshimiwa Kundo Mathew.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, nichukue nafasi hii kuanza kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa dhati na wa upendo wa kuona namna gani anataka kumtua mama ndoo kichwani. Dhamira yake hii imeonekana mapema kabisa wakati anaingia madarakani mwaka 2021 wakati bajeti yake ya kwanza kabisa aliyoanzisha ya shilingi bilioni 756 na leo hii tunazungumzia zaidi ya shilingi trilioni 1.12 zaidi ya ongezeko la 68%. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia kwa dhamira yako hii ya dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, nitakwenda mbio mbio ili nijaribu kuwasilisha yale ambayo wananchi wa Ndanda wameniagiza. Kwanza kabisa nilete shukrani zangu kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi wa chujio ambapo kesho kutwa siku ya tarehe tisa tunakwenda kuzindua na Mwenge wa Uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumpongeza pia Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutafutia alternative ya fedha zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa chujio kwenye chanzo cha maji cha Mbwinji ambapo chanzo hiki ni kikubwa na tegemezi sana kwa zaidi ya majimbo manne yaliyopo kwenye Jimbo la Ndanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ndanda wanashukuru sana kwa hizi fedha ambazo zimetolewa na Serikali. Pia Jimbo la Ndanda ndiyo hub ya maji kwa zaidi ya majimbo manne au matano yaliyopo Mkoa wa Mtwara. Maji mengi yanatokea kwenye Jimbo la Ndanda, na hii inathibitika kupitia mradi wa MANAWASA ambao unazalisha zaidi ya lita za maji 8,100,000; lakini uzalishaji wa maji haya umekuwa hauwanufaishi hasa wananchi wa Jimbo la Ndanda na kuwanufaisha zaidi majimbo mengine kwa mfano Nachingwea, Masasi Mji na Ruangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ndanda ndio walinzi wa mradi huu mkubwa wa MANAWASA kupitia chanzo cha Mbwinji, lakini mpaka leo hii ni kata nne tu ambazo zinanufaika kupitia mradi huu wa MANAWASA. Hivyo, wananchi wa Jimbo la Ndanda wamenituma nije nikuombe na wao wanahitaji wanufaike kupitia mradi huu wa MANAWASA kwa sababu mradi huu wa MANAWASA ndiyo mradi ambao unatoa maji ya baridi, na mazuri ukilinganisha na kata nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwepo huo kuna mambo ambayo wananchi wa Jimbo la Ndanda wanataka kuyoana. Kwanza kabisa uzalishaji kwenye vyanzo vingi vya maji kwenye Jimbo la Ndanda umeendelea kupungua kutokana na shughuli za kibinadamu kuongeza na uchimbaji wa madini na kilimo. Hii husababisha uzalishaji wa maji kwenye Jimbo la Ndanda kupungua na kusababisha mgawanyo mkubwa wa maji kwenye Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, wananchi wa Jimbo la Ndanda wanaomba Serikali ikiwezekana, basi iwekeze fedha kwenye ujenzi wa Bwawa Mkumba Shamba lililoko kwenye Jimbo la Nachingwea, Bwawa lile ambalo lina uwezo wa kuzalisha lita bilioni 24 kwa mwaka na lita milioni 66 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi kuanzishwa kwa mradi huo kutasababisha watu wa Nachingwea waweze kuwa na maji yao pekee badala ya kutegemea maji kutoka kwenye Jimbo la Ndanda, na yale maji ambayo yanatoka kwenye Jimbo la Ndanda yaende kuhudumia wananchi wa Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wananchi wa Jimbo la Ndanda wanaomba kama Serikali itawapendeza wawekeze kwenye mradi wa maji wa Mahiwa Nyangao mradi ambao utakuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni tisa na kutatua changamoto ya maji kabisa kwenye Jimbo la Ndanda na Wilaya ya Masasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Jimbo la Ndanda ndiyo Jimbo ambalo linaongoza kwa uzalishaji wa maji, zipo changamoto. Kwa mfano, leo hii kwenye Jimbo la Ndanda kuna zile DP (Domestic Point) 219 kwa ajili ya uuzaji wa maji, lakini mpaka kufikia jana ni DP 70 tu ndizo ambazo zinafanya kazi wakati DP 219 hazifanyi kazi na kusababisha wananchi wengi wa Jimbo la Ndanda kukosa huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya hizi DP kutokufanya kazi, kwanza kabisa wanalalamika wale watoa huduma kwamba wanabambikiwa fedha za ukusanyaji wa mapato kutokana na hizi DP. Leo hii wanakusanya fedha, wakienda kwenye hizi mamlaka kupeleka zile fedha, wanasema fedha mliyokusanya ni ndogo na bili iliyosoma ni kubwa. Wale watendakazi wanaacha kazi kwa sababu mishahara yao na posho zao zinatumika kwenda kufidia madeni zinazotokana na hizi DP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, kwanza wale watu ni watendakazi, siyo waajiriwa wa moja kwa moja. Ni watu tu ambao wanachukuliwa. Ninaomba mamlaka zitoe ajira kwa wale wafanyakazi, waajiriwe; wapate ajira za kudumu ili mzigo wa hili deni linalotokana na kuongezeka kwa bili usiende kuelemea kwa wale watendakazi, uwe wa mamlaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ushauri wangu mwingine, mamlaka za upimaji (wakala wa upimaji) wawe na utaratibu wa kuzipima hizi mita mara kwa mara kuangalia ufanisi wake na ili kuondoa huu mzigo mkubwa ambao wananchi wanalipa bili ambayo ni tofauti na kile ambacho wametumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri mwingine kwa hizi mamlaka, zichukue hatua ya haraka kabisa katika kutoa ajira ili hizi DP 219 ziweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kutokana na muda haya mambo mengine, nitachangia kwa kutumia njia ya mtandao. Ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)