Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Faraji Buriani Nandala (4 total)

MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya eananchi wa Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya mwaka 2025/2026 ndiyo hii ambayo tunaitekeleza na tunaelekea kuikamilisha hivi karibuni. Hizi fedha shilingi bilioni tano zilishatengwa, ina maana zipo. Kwa hiyo, nataka majibu ya Serikali, ni lini hasa watawalipa hawa wananchi wakati tuko kwenye process za kupitisha bajeti mpya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ninataka kufapata ushauri wa Serikali, je, wale wananchi waendelee kuandaa mashamba yao au wasiendelee, kwa sababu hii gridi ya Taifa inapita kwenye mashamba ya wananchi? Kama wasiandae yale mashamba, je, Serikali itakuwa tayari kulipa penati itayotokana na kuchelewesha kulipwa kwa hii fidia yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninampongeza sana kaka yangu Mheshimiwa Faraji kwa kufuatilia maslahi ya wananchi wake wa Ndanda, amekuwa anatufuatilia mara kwa mara na kuja ofisini kwa ajili ya kujua hatima ya line hii ambayo itaingiza mikoa ya Lindi na Mtwara katika gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa, sisi Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Fedha, tunajitahidi sana kuhakikisha kwamba fidia italipwa kwa wakati ili wananchi hawa wasiingie kwenye mgogoro mwingine kati yao na Serikali. Kwa hiyo, hilo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunajitahidi kutafuta fedha, na bado muda tunao, na hilo litatendeka ndani ya mwaka huu wa fedha, Mwenyezi Mungu akitujalia.
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.

Swali langu, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ndanda, nataka kufahamu ni lini Serikali itaona ipo haja ya kupunguza siku za maombi ya mikopo hii kutoka siku 90 zilizopo sasa hivi mpaka siku saba au 14, ili tuweze kuwafikia Watanzania wengi kwa muda mfupi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyoliuliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi siku 90 zipo kwa utaratibu, kwa maana ya kwamba wapewe elimu ambayo Mheshimiwa Mbunge ametoka kuuliza ni kipindi cha kupewa elimu, lakini kufanya ufuatiliaji wa kuona kwamba vikundi ambavyo vimeomba ni kweli vina haki ya kupewa mikopo ile na vina uwezo wa kurejesha. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tunauchukua ushauri wake na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Hali ya barabara kwenye Jimbo la Ndanda ni changamoto kubwa sana, hasa Barabara kutoka Kata ya Mlingula, Kata ya Namajani, Kata ya Namatutwe kuelekea Kata ya Msikisi. Ni lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko barabara ambazo zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha changarawe, kiwango cha udongo na kiwango cha Barabara na Serikali hii imeweka mpango wa kuhakikisha tunahama kwenye ujenzi wa barabara za udongo kwenda zaidi kwenye changarawe, lakini pale panapowezekana kujenga barabara za lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati wa utekelezaji wa mipango yetu ya ujenzi wa barabara tutaifanyia tathmini barabara hiyo na kuona uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya kuanza kujenga kwa awamu. Kwa changarawe ama kwa lami kwa kadri ambavyo fedha zitakuwa zimepatikana.
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kundi la vijana ndio kundi lengwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 na Serikali imekuwa ikilielekeza kundi hili kwenda kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo pamoja na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, kundi hili limekuwa likikabiliwa sana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikiathiri shughuli hizi za kiuchumi na kurudisha jitihada za vijana hawa.

Mheshimiwa Spika, swali langu, ni upi mpango wa Serikali kupanga bajeti maalum kwa ajili ya kundi la vijana ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo na uvuvi ambao wanapata changamoto sana za mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge; kwanza nimpongeze sana kwa namna anavyoendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo lake. Ni ukweli kwamba Serikali kwanza imeendelea kuwawezesha vijana kupitia mifuko mingi ya vijana ikiwemo hata juzi mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwenda kwenye Wizara ya Vijana. Hii yote ni kujali kwamba vijana wanafanya kazi na wanapata mitaji ya kuendesha biashara zao.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tuseme tumejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba kundi hili la vijana tunaliwezesha kwa kiasi kikubwa ili lisitetereke kwa namna yoyote, waweze kujiinua kiuchumi kupitia shughuli zao wanazozifanya za kila siku.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.