Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu 2026/2027–2050/2051, Mapendekezo ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027–2030/2031 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2026/2027; na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati ya 2026/2027 hadi 2028/2029.
MHE. HAIDERALI H. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipatia nafasi hiyo ili niwe miongoni mwa wachangiaji. Nianze kabisa kwa kuwapongeza Wana-CCM wote kwa maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa, tuna kila sababu ya kuwapongeza. Pia ninapongeza Wizara zote za Mipango na Uwekezaji pamoja na Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambayo wamefanya kutuletea ripoti hii, hakika endapo Watanzania tutaifanyia kazi vizuri hiyo, taswira ya Tanzania huko ifikapo itabadilika kabisa Barani Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza kupongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan. Sekta ya Nishati, nina kila sababu ya kumpongeza Waziri husika kwa sababu sasa anaenda kusaini mkataba ambao unatuletea umeme katika vitongoji. Tanzania ya leo kwa uongozi shupavu wa Mama Samia tayari vijiji vyote tumeshawasha umeme. Sasa, taarifa rasmi kama Mbunge wa Ilongero, ninaomba kuwajulisha wananchi wangu kwamba nyumba 11,654 sasa katika vitongoji wanaenda kupata umeme kwa shilingi 27,000. Nina kila sababu ya kujivunia kwamba mimi ni Mwana-CCM na Rais wetu ni Mwana-CCM na anachapa kazi kwa vitendo tumeona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kwetu watu wengi wanahusika na kilimo na ufugaji, kwa hiyo ninazungumzia Sekta ya Kilimo. Sekta ya Kilimo kwetu tuna bwawa ambalo Serikali inatujengea mpakani mwa jimboni kwetu na Manyara ambako ni kwako pia. Wananchi watanufaika na umwagiliaji wa bwawa hili kwa sababu yenye thamani ya shilingi bilioni 17 imetuletea Serikali ya Awamu ya Sita, nina kila sababu ya kuwashukuru kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida tayari tuna neema, tunalo bwawa ambalo hakuna haja ya kujenga, tumepewa ruzuku na Mwenyezi Mungu, tumeshushiwa kutoka mbinguni, yako zaidi ya nane. Serikali haiwezi kuingia gharama ya mabilioni ya fedha endapo yatatumika mabwawa hayo yaliyojaa na maji na samaki pia kama walinzi watalinda. Kuunganisha tu umwagiliaji ili wananchi wakulima na wafugaji waweze kunufaika na hilo, hilo kwa kweli katika mpango kazi liangaliwe vizuri litatusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo katika Sekta ya Kilimo, tuliahidiwa na Serikali kwamba tutakuja kupata soko la vitunguu ambalo ipo nafasi imetengwa nafasi katika Kata ya Merya, fedha shilingi bilioni 2.9 ilitengwa na ilipitishwa, tuko mbioni kukamilisha na Wizara tumeshawasilisha mikataba ambayo walitushauri wao, kilichobakia wao wakamilishe na waweze kutufikishia ili kazi ianze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza sana na tumesikia kilio cha wananchi, kilio cha wananchi ni soko la dengu. Soko la dengu asilimia kubwa soko la hilo zao inasafirishwa kwenda India, lakini wakulima wanalia, Wabunge wanalia wanasema kwamba soko hili linakuwaje. Hivi kweli tunaweza tukaamini kwamba nchini India Wahindi wameacha kula dengu? Ni vitu ambavyo haviingii akilini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba urasimu uliopo wa kodi ndiyo kinachotuumiza. Tukiondoa urasimu huo, hizo dengu, changamoto hizo zipo na Jimboni kwako nisemee wananchi wako pia, tunamaliza mara moja. Hilo ni zao, hiyo siyo almasi, hilo ni zao, hiyo siyo dhahabu, zao linaoza almasi haiozi, ikinyeshewa mvua inaharibika. Hivi sasa wakulima wetu hawalimi tena, wanalipia maghala wamehifadhi. Kwa hiyo, Wizara iweze kuangalia upya utaratibu huo wa hizo tozo ili wananchi wetu waweze kunufaika na waweze kuuza mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia upande wa mifugo, Wizara ina aina mbili ya ufugaji, kuna wale ambao ni wafugaji na kuna wale ambao ni wachungaji. Kuna wale ambao wanafuga mifugo na kuna wale ambao wanachunga mifugo. Sasa hawa wanaochunga mifugo ndiyo unaona kwamba matatizo yanatokea kati ya hawa wafugaji ambao ni wachungaji na wakulima, kwa sababu mifugo hiyo wachungaji wanaiswaga, inatembea kilometres, inaenda mbali, ikirudi inakuwa imeshaharibu mashamba ya wakulima na hapo ndipo tatizo linapoanzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ifike mahali ambapo kwa makusudi kabisa Wizara husika iweze kubadilisha hawa sasa wachungaji waingie katika ufugaji wa kwelikweli. Ufugaji ni pale ambapo unafuga hiyo, unaenda shambani kwako, unaweka malisho yao unawaletea pale walipo ili wanenepe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia upande wa private sector. Private sector imekidhi wafanyabiashara, nikizungumzia wafanyabiashara, ninaomba sana wahusika waangalie kwa jicho la huruma. Kuna wafanyabiashara ambao wajasiriamali, kuna wafanyabiashara ambao ni wadogodogo sana, ambao labda wanauza matunda, wanauza mboga aina mbalimbali, wanauza mihogo, hizo zinawafanya wapate kipato chao na maisha yao yaweze kuendelea. Sasa ifike mahali Serikali kwa makusudi iweze kutangaza kwamba atakayemnyanyasa au atakayempakia katika gari yoyote huyo anayeuza bidhaa zake ili aweze kujipatia kipato chake, iwe criminal offence, ninadhani hata Waziri Mkuu katika ziara yake alishawahi kukemea sehemu nyingi sana hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika private sector, sasa hivi mfanyabiashara akitaka kutoka nje, akitaka kwenda popote pale, anaambiwa kwamba anaruhusiwa kusafiri na dola 10,000 tu, lakini sheria inawabana hata wale wanaokuja kutoka nchi za nje, unawaambia kwamba sasa hauruhusiwi kuja na zaidi ya dola 10,000. Hii sheria ibadilike, wahusika hii sheria ibadilike. Mtu anakuletea fedha, anakuletea neema, anakuja kununua bidhaa zake hapa Tanzania, unamwekea kikomo kwamba asije na zaidi ya dola 10,000! Yaani wewe mwenyewe ndiyo unakuwa chanzo cha kuondoa na kuweka tuta katika ukusanyaji wa mapato yako. Hivyo ni vitu ambavyo haviingii akilini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dola ni kitu gani? Dola siyo dawa za kulevya, ifike mahali ambapo wafanyabiashara waliopo mipakani, waruhusiwe kupokea dola na kupeleka benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Dubai leo, kwa miaka yote hiyo thamani ya dola utakuta 3.55, 3.66 haizidi hapa.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante. Malizia Mheshimiwa muda wako umekwisha.
MHE. HAIDERALI H. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam?
MWENYEKITI: Malizia muda wako umekwisha.
MHE. HAIDERALI H. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na ninakushukuru sana. (Makofi)