Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza ninaomba kutumia nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, lakini pia kumshukuru Naibu Spika, pamoja na Wenyeviti wote watatu wa Bunge letu na ni imani yangu kwamba wote leo wamo humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakushukuru wewe binafsi kwa kutupa heshima kama Wizara yetu ya Ulinzi na kuja kuongoza sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kuishukuru Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Wamekuwa ni watu wanaojua nini maana ya ulinzi na usalama ndani ya nchi yetu, lakini pia nitumie nafasi hii pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, lakini na wale ambao hawajachangia. Kwa wale waliochangia wapo Waheshimiwa Wabunge saba, michango yao yote tumeichukua, lakini tumeichukua kwa ukamilifu na tutaifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijikite katika yale mambo ambayo yamejirudia ili niweze kutoa ufafanuzi; cha kwanza, nimshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Ado, na nimekushukuru kwamba pamoja na ulivyozungumza kulingana na unapotoka, lakini umeamini kwamba tahadhari juu ya ulinzi ni nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ndio nchi ambayo tunapenda tuijenge, nchi ambayo tuna dini tofauti, nchi ambayo tuna vyama tofauti, lakini inapofika suala la ulinzi na usalama tunakuwa kitu kimoja. Kwa hiyo, ninakushukuru ndugu yangu Mheshimiwa Ado. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nijielekeze kutoa ufafanuzi juu ya maveterani wale wazee wetu waliopigana, wengine wamelala mauti, lakini wengine wapo hai wa vita ya Kagera. Cha kwanza, ni vyema Bunge lako Tukufu lijue kwamba Amiri Jeshi Mkuu kwa maana ya Mheshimiwa Rais, amewapa hawa maveterani wa Kagera heshima kubwa kwa sababu tangu walipomaliza vita ile, vita ya Kagera ilikuwa ina makundi matatu; kundi la kwanza lilikuwa ni wanajeshi waliokuwa jeshini, lakini kundi la pili ni watu kwa maana ya wenzetu ambao walijitoa wakasema kwa sababu tumevamiwa sasa tujitoe, wakaji-mobilize wenyewe hawana mafunzo ili waende kwa ajili ya kuikomboa nchi na kupambana na Nduli Idi Amin.
Mheshimiwa Spika, lakini kundi la tatu lilikuwa ni Jeshi la Akiba. Sasa katika hili baada ya vita ya Kagera, wale wazee wetu walivyorudi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama vilitoa nafasi kwa watu kwenda kuajiriwa kwenye vile vyombo vingine tofauti na jeshi kwa sababu wapo walioenda kwa ajili ya lile zoezi tu la vita. Sasa wapo waliokosa sifa za kuajiriwa na vyombo vingine tofauti na jeshi kwa sababu wapo walioenda kwa ajili ya lile zoezi tu. Sasa wapo waliokosa sifa za kuajiriwa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa wakati ule kwa sababu walikuwa wamepata majeraha hawana sifa. Hawa ndio ambao sasa tunawazungumzia.
Mheshimiwa Spika, kwa huruma ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, pamoja na kwamba wakati ule walilipwa kifutajasho shilingi 5,000 kwa wakati ule iliyokuwa inaitwa Ahsante Nyerere. Baada ya kulipwa, pamoja na mambo yote yaliyopita, Mheshimiwa Rais mwaka jana akatoa maelekezo kwetu sisi Wizara ya Ulinzi kwamba wale wazee wetu ambao waliipambania nchi sasa ni vizuri Wizara ikaangalia namna ili waingizwe kwenye daftari la pensheni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa mwezi Juni kuna taratibu kidogo zinatokea kwamba hili ilikuwa ni mwezi Juni, kwa hiyo lazima zile taratibu za kiserikali kutangaza liwe gazetted ili sisi kwenye Wizara ya Ulinzi tuweze kukaa kwenye halmashauri ya majeshi, tubadilishe baadhi ya vipengele ambavyo vitaruhusu sasa wale wazee wetu waweze kuingizwa kwenye daftari la kulipwa pensheni, kazi hiyo mpaka sasa ninavyozungumza tumeshaifanya na imeshakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi ya pili ilikuwa sasa ni namna ya kuwatambua wako wapi hawa. Kazi hii naomba Waheshimiwa Wabunge watatusaidia ili kwa namna moja au nyingine waweze kufikiwa kila mmoja. Tukawasiliana kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa sababu kila wilaya sisi tuna Mshauri wa Jeshi la Akiba au Mshauri wa Mgambo. Kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya tumeshabatambua zaidi ya wazee wetu 7,800 tayari ambao sasa katika hawa tayari tumeshafanya ile quantification kwamba wanapaswa kulipwa ni hawa na tumeshapeleka majina haya Hazina, Wizara ya Fedha, ili na wenyewe wafanye uhakiki na hawa wazee tayari waanze kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, rai yangu mimi kwa Waheshimiwa Wabunge akiwemo na ndugu yangu Mheshimiwa Ado mtusaidie kutoka kwenye majimbo yenu. Sisi tutatoa maelekezo na ushauri kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, watusaidie sasa kutoa tangazo kwa wale ambao hawana taarifa rasmi...
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, ni Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, samahani, ni Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, watusaidie sasa kutoa tangazo kwa wale ambao hawajafikiwa ili waweze kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, naomba sasa nitoe pia ufafanuzi kwenye hoja ya pili ambayo imejirudia.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni namna ya vijana wetu wa kidato cha sita waweze kujiunga kwenye Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza ni nia ya dhati ya Serikali kwamba baada ya kufanya tafiti za kina, tukagundua kama nchi kwamba lipo jambo ambalo tunapaswa kulifanya ili kuhakikisha kwamba tunaongeza ukakamavu, uzalendo, lakini pia na uzalishaji mali kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Spika, hapo nyuma kidogo kulikuwa kunakuwa na baadhi ya hata migomo kwenye vyuo vyetu. Sasa tukafanya utafiti na kugundua kwamba ipo haja ya kuwafunza hawa vijana wenzetu uzalendo na nini maana ya kulinda nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tangu Jeshi la Kujenga Taifa lilipoanza, takwimu zinaonyesha kwamba hata ndani ya vyuo vyetu vikuu ambavyo vina watu wa dini tofauti, vyama tofauti, hakuna migomo. Hili ni zao la mafunzo ambayo yanafanyika. (Makofi)
Kwa hiyo, baada ya hiyo Mheshimiwa Rais ameshatuelekeza kwamba nia yake ya dhati ni kuhakikisha kwamba vijana wote wanaomaliza kidato cha sita waweze kujiunga. Ile bajeti yetu ambayo sasa tunaendelea kuifanyia kazi mpaka sasa tuna uwezo wa kuchukua vijana 60,000 lakini tumeweka malengo yetu kama wizara kupitia JKT kwamba tuweze kuchukua vijana 140,000. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa katika malengo yale tumeweka yale ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. Malengo yetu yamewekwa kwamba kufikia mwaka 2031 tuwe tayari tuna uwezo wa kuchukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita, hilo ni lengo la kwanza na lengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo la pili ambalo pia ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni kwamba yale mafunzo ya miezi mitatu, bajeti ya Serikali ikiruhusu tutayaboresha siku za usoni ili yaweze kwenda zaidi ya miezi mitatu kama ilivyokuwa zamani. Hii inamaanisha nini, hii inamaanisha kwamba si kila kijana anayeenda kwenye Jeshi la Kujenga Taifa anaenda ili aajiriwe kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, hapana.
Mheshimiwa Spika, tunawapeleka pale ili wakajifunze wengine namna ya kujitegemea na kutengeneza maisha yao kupitia uzalishaji mali. Kwa hiyo, tunaingiza mfumo ambao tutakuwa pia na sisi tunafanya vocational training. Hiyo itatusaidia na itasaidia hata Wizara yetu ya Vijana kupitia Ofisi ya Rais ili iweze kupitia Wizara yetu ya Ulinzi na sisi tuwe chanzo cha kufunda wale vijana na kuweza kupanua wigo wa ajira za kujitegemea.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili, hayo ndiyo maelezo ambayo tuna uhakika kwamba utekelezaji unaendelea na mpaka sasa hata bajeti ya mwaka huu imeongezewa kwa ajili ya kuweza kutengeneza miundombinu wezeshi ya kuweza kuongeza vijana kwa mwaka ujao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatu ambalo nilipenda pia nitolee ufafanuzi kidogo ni fidia. Ni kweli kwamba lazima nikiri michango ya Waheshimiwa Wabunge na wale wenzetu wachangiaji wote. Sisi kama jeshi ni kweli kwamba tuna uhitaji wa baadhi ya maeneo ambayo yapo kimkakati. Yapo kimkakati ili kuweza kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu. Uzuri uliopo ni kwamba wananchi wetu ni waelewa sana. Jeshi linapoonesha nia ya kutaka eneo, wanakuwa wepesi sana wa kuweza kukubali kwamba sisi tunaweza tukapisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye yale maeneo yote ambayo tumeyafanyia uthamini, mpaka sasa tumeshazungumza na wenzetu wa Wizara ya Fedha na tumeshalipa zaidi ya shilingi bilioni 12 kwenye huu mwaka unaoishia wa 2025/2026. Lakini kwenye bajeti hii ya sasa tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 30 ili tuweze kulipa zile fidia za haya maeneo yote ambayo tayari uthamini umeshakufanyika.
Mheshimiwa Spika, tuna imani kwamba maeneo yote ambayo yamefanyiwa uthamini, Serikali yetu kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha italipa zile fedha baada ya kuwa bajeti mpya imeanza kutekelezwa. Hivyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge muelewe kwamba ukweli ni kwamba sisi ndio tunaopaswa kuzuia migogoro na wananchi waweze kuliheshimu jeshi, lakini pia waweze kuiheshimu Serikali yetu na kuhakikisha kwamba wanakuwa wao ndio walinzi namba moja wa kutoa taarifa za kiusalama na kuwa na mapenzi na nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba niwashukuru sana ndugu zangu wa Wizara ya Ulinzi, nikianza na Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe; pia Mkuu wetu wa Majeshi na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi letu la JWTZ. Namshukuru pia ndugu yetu Mkuu wa JKT na Wakuu wa Kamandi wote ambao mmefika hapa, Wakuu wa Idara, Wakuu wa Mashirika yetu ya SUMA-JKT, Mzinga pamoja na Nyumbu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa niwashukuru ninyi Waheshimiwa Wabunge kwanza kwa imani kubwa ambayo mmeipa nchi yetu na mmempa Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba Wizara yetu ya ulinzi inakuwa ni Wizara nyeti na hii inamaanisha kwamba wote tunaelewa nini maana ya amani hata tuwe na malengo ya namna gani ya Vision 2050, kama hatuna usalama ndani ya nchi yetu, kama hatuna amani ndani ya nchi yetu, kama hatulindi mipaka yetu sisi wenyewe kwa ku-identify adui, hiyo kazi yote ambayo tunaipanga haitaweza kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, heshima mliyotupa sisi tutailinda na sisi tupo kwa ajili ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, lakini pia na Vision yetu ya 2050 iweze kufikiwa jinsi inavyopaswa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)