Answers to Primary Questions by Hon. Omari Juma Kipanga (5 total)
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma ya TEHAMA maeneo wanayotumia Wanafunzi kujisomea katika Vyuo Vikuu vya Umma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya maboresho ya Miundombinu ya Internet; Mifumo ya Kujifunzia Kidijitali (LMS); Maktaba za Kidijitali; Elimu kwa Studio za Multimedia; Mifumo ya Kiutawala Kidijiti na kununua Vifaa kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum katika Vyuo Vikuu vya Umma. Lengo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa elimu ya juu wanapata mazingira bora ya kujisomea yanayochochea ujifunzaji wa kisasa, jumuishi, na unaotumia teknolojia kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio ya maboresho haya ni hatua muhimu katika mwelekeo wa kuifanya elimu ya juu nchini kuwa ya kisasa, jumuishi na yenye ushindani wa Kimataifa ili kufikia ajenda ya mageuzi ya elimu ya juu hapa nchini.
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kuongeza fedha za mkopo kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wenye mahitaji maalumu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Daktari, ninaomba nichukue nafasi hii kipekee kabisa kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, na kuwashukuru Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge lako hili Tukufu kwa malezi yenu katika kipindi chote cha miaka mitano. Ushauri wenu kwa Serikali, maoni na miongozo yenu ambayo mara kwa mara mmekuwa mkitupatia sisi kama Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa upande wa Wizara ya Elimu, hili ni swali letu la mwisho kwenye Bunge hili, na niwaombee heri Wabunge wote tuje kuonana tena hapa mwezi wa Kumi na Moja tukiwa na afya njema, Mwenyezi Mungu akatuvushe huko tunakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, sasa ninaomba kujibu swali la Dkt. Nahato, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza fedha za mikopo ya elimu ya juu mwaka hadi mwaka ili kuwawezesha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalumu ambao ni wahitaji na wanaotoka kwenye familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi ili kuwawezesha kumudu gharama za masomo ya Elimu ya Juu na kufikia ndoto zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za mikopo zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 464 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 787 mwaka 2024/2025 na idadi ya wanufaika imeongezeka pia kutoka wanafunzi 145,000 mwaka 2020/2021 hadi 235,799 mwaka 2024/2025 wakiwemo wenye mahitaji maalumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, utoaji mikopo unawapa ahueni wanafunzi wenye mahitaji maalumu au wenye wazazi wenye ulemavu kwa kuwapatia kipaumbele katika upangaji wa mikopo ili kuwawezesha kumudu mazingira ya chuo katika kipindi cha masomo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya wanafunzi 2,398 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2024/2025 kupitia kigezo cha mahitaji maalumu. Serikali inaendelea kupokea ushauri na maoni ya wadau kwa ajili ya kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau ili kubainisha aina ya uhitaji unaostahili kupewa kipaumbele bila kuathiri dhana ya uhitaji inayotamkwa na sheria. Ninakushukuru sana.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi na stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuniteua na kuniamini katika nafasi hii ya kumsaidia Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Suleiman Mohamed Rashid, Mbunge wa Mwera. Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita ni mitihani muhimu ambayo usahihishaji wake hufanyika kwa baadhi ya walimu kukusanywa katika vituo maalum kwa ajili ya jukumu hilo unaozingatia muda maalum, usalama, usiri, mazingira wezeshi na ubora wa kazi.
Mheshimiwa Spika, stahiki za Walimu wanaosahihisha Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne na Sita hulipwa kwa kuzingatia miongozo ya usahihishaji wa Mitihani kwa kipindi husika. Ili kuleta ufanisi wa kazi hiyo, miongozo hiyo imeendelea kuboreshwa mara kwa mara. Serikali itaendelea kuboresha maslahi na stahiki za walimu katika usahihishaji wa mitihani ya Taifa ili kuimarisha na kuongeza ufanisi wa kazi hiyo.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA Tarafa za Nyabiyonza na Nyakakika kwani kuna umbali mrefu toka Chuo cha VETA Kayanga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Wilaya ya Karagwe, Serikali imejenga Chuo cha VETA cha Wilaya kilichopo Kayanga ambacho kina mabweni na kinaendelea kutoa mafunzo. Kwa sasa wanachi wa Tarafa za Nyabiyonza na Nyakakika wanaweza kuendelea kutumia chuo hicho kwa kuwa kinatoa huduma ya malazi katika mabweni yaliyojengwa kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka umbali mrefu.
MHE. THOMAS K. MAGANGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Halmashauri ya Wilaya ya Mlele – Katavi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Thomas Kampala Maganga, Mbunge wa Katavi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mlele ambacho kinatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026. Hadi sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Bilioni 1.032 kati ya Shilingi Bilioni 1.6 zilizotengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa awamu ya kwanza. Mpaka sasa, ujenzi huo umefikia 73%.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga na kupokea fedha ili kuwezesha ujenzi wa chuo hiki kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa mafunzo kama ilivyopangwa.