Answers to supplementary Questions by Hon. Omari Juma Kipanga (4 total)
MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika swali langu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa sasa hivi Serikali imeboresha sana TEHAMA katika vyuo vikuu. Je, imejipangaje kuwajumuisha wafanyakazi wa TEHAMA katika vyuo vikuu ambao sio wataaluma kushiriki katika kuboresha TEHAMA katika vyuo vikuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Vyuo vikuu vya umma nchini vinaendesha masomo ya masafa (distance learning) kwa wanafunzi walioko mikoa mbalimbali. Je, Serikali imejipangaje kuwasaidia wanafunzi hawa hasa katika upande wa TEHAMA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba kumpa taarifa Dkt. Nahato kwamba, Serikali tayari imeanza mkakati wa maboresho ya vyuo vikuu vyote nchini, kupitia mradi wetu mkubwa kabisa ujulikanao kama higher education for economic transformation ambao una mawanda karibu sita au maeneo sita ambayo yanafanyiwa kazi. Eneo la kwanza ni ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya campus hizi zilizopo pamoja na campus mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni kusomesha wahadhiri ndani pamoja na nje ya nchi; eneo la tatu, ni kutunga mitaala mipya pamoja na kuboresha ile mitaala iliyopo; eneo la nne, ni ushirikiano baina ya vyuo vyetu vikuu pamoja na viwanda; eneo la tano, ni uwezeshaji wa wenzetu wenye mahitaji maalum; na eneo la sita, ni hili eneo la TEHAMA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika eneo la TEHAMA Serikali imejikita kufanya mambo yafuatayo ili kuboresha mazingira ya TEHAMA katika vyuo vyetu: ambapo eneo la kwanza, tutafanya upanuzi wa miundombinu mbalimbali ya internet kuhakikisha kwamba tunakuwa na smart classes, lakini tunakuwa na smart campus ambazo zitakuwa sasa zinawasiliana siyo tu ndani ya nchi, bali hata kufikia vyuo vingine katika nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni kutengeneza mifumo sasa ya kidijitali ile ya kujifunzia na kusomea. Eneo lingine ni kutengeneza maktaba za kimtandao au maktaba za kidijitali ili kupata ile e-Learning kwa ujumla wake. Eneo la nne ni sasa hiyo elimu iliyozungumzwa kwa njia ya masafa, inazingatiwa kwenye eneo hili, lakini vilevile tunatengeneza sasa studio katika vyuo vyetu vyote vikuu ili kuweza kutengeneza vipindi ambavyo siyo lazima Mwalimu muda wote awepo darasani. Wanafunzi wanaweza ku-access kupitia maktaba zetu, lakini vilevile kuna ununuzi wa vifaa sasa kwa ajili ya kufanya mifumo hii iweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo haya yote yanajumlisha vilevile watumishi wasio wanataaluma ili kuhakikisha kwamba mifumo hii inafanya kazi pamoja na kuwasomesha watumishi hawa wasio wanataaluma ili kuhakikisha mifumo ya TEHAMA inakwenda kufanya kazi sawasawa na kwenye vyuo vyetu. Ninakushukuru sana.
MHE. SULEIMAN MOHAMED RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pamoja na majibu hayo nina swali la nyongeza. Serikali haioni haja kuandaa mwongozo wa dharura wa uboreshaji ambao utaweza kuzingatia kulipwa kwa posho ya kujikimu pamoja na posho maalum kwa walimu ambao wanasahihisha mitihani hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiboresha maslahi ya walimu wanaosahihisha mitihani kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo pamoja na posho wanazolipwa Serikali pia hulipa malazi, chakula, matibabu wakati wote wa kazi. Hata hivyo, ushauri wa Mheshimiwa Mbunge tumeupokea. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshuruku Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa Wanakaragwe, ninaamini ombi langu kutokana na umbali wa tarafa hizi mbili kwenda kwenye Kituo cha VETA Kayanga Mjini, Wizara itaendelea kulifanyia kazi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Chuo cha VETA pale Kayanga Mjini kipo katikati ya mji na hakina uzio. Je, ni lini Serikali itatujengea uzio?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Chuo kina uwezo wa ku-accommodate wasichana 52, lakini hivi sasa chuo kina wasichana 125. Je, Serikali itatujengea lini bweni lenye uwezo wa kuwa-accommodate wasichana wote? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ninaomba nijibu swali la Mheshimiwa Bashungwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza kwa kufuatilia mambo yanayohusiana na jimbo lake, lakini Serikali inatambua kwamba, uhitaji wa uzio kwa Vyuo vya VETA ni kwa vyote vile ambavyo vimejengwa vya wilaya. Serikali inafanyia kazi kwa awamu suala hili ambapo Chuo cha VETA cha Kayanga ni miongoni mwa vyuo ambavyo vipo katika mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili; ninakubaliana na yeye kwamba, bweni lile ambalo lipo sasa hivi la wasichana halitoshi, lakini hatua za dharura zimechukuliwa. Kuna jengo moja la Chuo cha Kayanga limefanyiwa ukarabati, kwa ajili ya kuwaweka wasichana wetu na ujenzi umeshakamilika. Fedha ya kupeleka furniture imetengwa kwa hiyo, muda wowote furniture zitapelekwa na watoto wataanza kutumia bweni hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua wasichana 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeweka mpango wa muda mrefu wa kujenga jengo la wasichana ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua wasichana 200. Kwa hiyo, naamini wasichana wa Wilaya ya Karagwe watakuwa wapo salama na watapata mafunzo ipasavyo.
MHE. THOMAS K. MAGANGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kulingana na umuhimu wa chuo hiki, je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha ujenzi huo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kabla sijaja Bungeni, nilitembelea mradi huo wa ujenzi, mradi huo hauridhishi. Je, Waziri yuko tayari kwenda kujionea halisi ya mradi na kutoa msukumo ili mradi ukamilike kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako ninaomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa ufuatiliaji wake juu ya maendeleo ya Chuo hiki cha Mlele, lakini pia nimpongeze nimepata taarifa kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Wabunge wapya katika Bunge hili. Kwa hiyo nimpongeze kwa nafasi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya awali, kwamba kati ya bilioni 1.6 ambazo zilizotengwa, bilioni 1.032 tayari zimeshatumika. Kwa hiyo bakaa iliyobaki siyo kubwa sana na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kumalizia vyuo hivi na kuanza ujenzi pia wa vyuo vingine. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Maganga kwamba, fedha zitaenda na chuo hicho kitamalizika katika awamu ya pili. Ahsante
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, niko tayari kwenda na kuangalia maendeleo ya chuo hiki.