Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Said Ibrahim Mzimba (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SAID IBRAHIM MZIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu, ninaomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kunifikisha hapa kwa sababu hakuna jambo lolote chini ya jua linalowezekana bila idhini ya Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nikishukuru chama changu cha ACT-Wazalendo kwa kuniamini na kunipa heshima ya kuwatumikia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Said Ibrahim Mzimba kwa mujibu wa kanuni zetu, hutakiwi kusoma, unatakiwa kufanya rejea tu kwenye hiyo document, lakini siyo unasoma, endelea.
MHE. SAID IBRAHIM MZIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Mtambile kwa imani walionionesha kwa kunichagua kwa kura nyingi. Ninaahidi mbele ya Bunge hili na mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia kuhusu Baraza la Vijana Tanzania. Kuna umuhimu mkubwa wa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana Tanzania. Ninafurahi kwa kuwa nilimsikia Waziri akizungumzia jambo hili, lakini ninataka nimwambie, hakuna wakati ambao Tanzania inapenda kuwa na Baraza la Vijana kama wakati huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna wakati ambao vijana wa Tanzania wanapenda kuwa na Baraza la Vijana kama wakati huu. Kwa hiyo, ninaomba, kuweka msisitizo, na katika baraza hilo ninaomba katika uundwaji wake kusiwe na pingamizi ya siasa, kidini, wapi unatoka, au jinsia. Baraza hili liwe chombo cha kuwaunganisha Watanzania na vijana wetu wote kwa sababu sisi ndio tuliowazaa, na tuliowalea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wanahitaji umoja wetu na mshikamano wetu ili kuliendeleza Taifa kwa hivi sasa, maana yake tumezoea kuwaita vijana ni Taifa la kesho, lakini kwa hivi sasa, kwa wakati huu vijana ni Taifa la hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba nichangie kuhusu shilingi bilioni 200 zilizowekwa na Rais wa Tanzania. Ninaunga mkono hii hoja ya Rais wetu kuweka fedha hizi, lakini sasa utekelezaji wake una changamoto kubwa kwa sababu hizi fedha zimetawanywa kwenye Wizara mbalimbali: Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara. Sasa usimamizi wa hizi fedha sijui utakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, hizi fedha zikusanywe, zirudi kwenye Wizara ya Vijana kwa sababu Waziri wa Vijana ndiye aliyekabidhiwa bango la lile hundi. Kwa hiyo, vijana wote wa Tanzania fedha hizi wanajua kuwa anazo Waziri wa Vijana. Kwa hiyo, zirudi hapa ili ziweze kudhibitiwa, kwa sababu zikiwekwa kwenye Wizara ya Mifugo, au Wizara ya Biashara, nani atakayekuwa mdhibiti wa fedha hizi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoomba, Waziri wa Vijana ndio awe msimamizi wa fedha hizi, zikigaiwa kwenye sehemu mbalimbali, uwezekano mkubwa wa matumizi yasiyo na tija yatapatikana, pia ugumu wa ufuatiliaji wa matokeo utapatikana. Ninapendekeza fedha hizi zirudi kwenye Wizara ya Vijana na masharti ya mikopo siku zote jamani, anayetaka kusaidiwa ni yule aliyekuwa hana kitu. Utamsaidiaje mtu ambaye ana chanzo, umwache mtu ambaye hana kitu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba haya masharti ya kuwa lazima uwe na mtaji ndiyo uweze kupata mkopo huu, yaondolewe kwa sababu tutawafungia milango wale wahusika ambao walitakiwa kupata fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli tuseme, vijana wetu wa Tanzania wengi hawana ajira, na wengi hawajapata mwendelezo wa kibiashara. Kwa hiyo, unapozuia ukasema lazima wenye mitaji ndio wapewe fedha hizi, tutakuwa hatuwatendei haki wale ambao ndio wanajikusanya hivi sasa waanze kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wengi wa Tanzania ni wale ambao wanajitafutia riziki ya kula leo, kesho atoke. Kwa hiyo, ninaomba hili tulizingatie kwa mapana makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa sababu ya ufinyu wa muda, ninaomba, sisi ACT – Wazalendo, tumefanya uchambuzi mkubwa sana wa hoja hii ya vijana. Kwa hiyo, tutawasilisha kwa maandishi kwenye Ofisi ya Waziri ya Vijana na Maendeleo ya Vijana, ahsante.