Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Patali Shida Patali (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nishukuru kwa nafasi hii uliyonipa. Mchango wangu kimsingi ninaomba ujikite kwenye maeneo, hasa eneo kubwa la mbolea. Ninaomba nifikishe salamu za Wanambeya Vijijini kwa kuwasemea maeneo mawili kwa haraka. Kwanza ni kuhusu pareto. Mbeya Vijijini ni moja ya wilaya ambayo inaongoza kwa kilimo cha pareto nchini, kwa mujibu wa taarifa za Bodi ya Pareto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kuna jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kwa ajili ya kuboresha biashara ya zao hili. Hivi karibuni na kwa kupitia Taarifa iliyowasilishwa, kuna mpango wa ujenzi wa haya makaushio 150 na sisi Mbeya vijijini tunayo 40. Tuiombe Serikali ituharakishie ujenzi huu wa haya makaushio kwa ajili ya kuboresha hili zao la pareto Mbeya Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie bei; moja ya changamoto kubwa kwenye zao hili la pareto ni kuwa na vishoka wengi ambao wanadidimiza jitihada za makusudi za wakulima. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Chongolo wawaangazie macho hawa vishoka ambao wanaingilia kati kwenye hizi bei za hili zao la pareto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nizungumzie mazao. Jimbo la Mbeya Vijijini tunazalisha zaidi ya tani laki sita za mazao ya chakula lakini mahitaji yetu ni takribani tani laki moja na tisini hadi laki mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia katika Bunge hili, tusipoliangalia vyema hili suala la masoko nchini, tunaenda kuzalisha mazao mengi na tukakosa masoko kwa kwenda kuyauza. Cha kwanza, ninaomba nisisitize kuboresha masoko ya ndani, ikiwa ni pamoja na kujenga masoko kwenye kila wilaya ambazo zinaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza ukawaza hizi tani 400,000 sisi Mbeya Vijijini ambazo tunazalisha ziada ya chakula dhidi ya mahitaji yetu tutazipeleka wapi endapo hatutaboresha au kuchukua hatua za makusudi kujenga masoko?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ninatamani kujikita ni suala la mbolea; na hapa ninaomba nichangie haraka haraka kwa sababu ya muda mfupi. Nchi yetu hii inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 tutakuwa na takribani ya wastani ya watu wasiopungua milioni 77.55. Watu hawa wote wanahitaji ardhi kwa ajili ya kilimo ili kuelekea ule uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050 kama Dira yetu ya Taifa inavyoeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo chetu kiwe na tija ni lazima tuangalie uwezekano na kuchukua jitihada za makusudi katika kuimarisha upatikanaji wa mbolea nchini. Hali ilivyo sasa, tunapata mbolea ya ruzuku na hapa ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais; lakini bado kuna changamoto ya kuchelewesha mbolea na pia kuingiliwa na walanguzi wanaoficha mbolea. Wakati mwingine zinaadimika sokoni na kuwalazimisha wakulima wazitafute kwa njia nyingine. Ni kwa sababu mkulima anakosa option, kwa hiyo inabidi awatafute walanguzi. Niiombe Wizara ya Kilimo kupitia TFRA, ninatambua wanafanya kazi nzuri sana, lakini waboreshe eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, ili kutatua hii adha ni kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani tunavipa nguvu katika maana ya uwekezaji. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema tuna takribani viwanda 48 vya uzalishaji wa mbolea, lakini viwanda viwili tu; INTRACOM na Minjingu ndivyo at least vinazalisha, vinabeba viwanda vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa kumalizia, tutafute uwezekano wa kuwekeza kwenye viwanda hivi ili kuongeza tija ya upatikanaji wa mbolea na kuwarahisishia wakulima ili kupata mbolea na kilimo ambacho wanalima kiwe na tija na cha uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba muhimu ya Wizara hii nyeti ya Maji. Awali ya yote, niungane na Wabunge wote waliotoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji kutoka shilingi 898,000,000,000 mpaka shilingi trilioni 1.1, hili ni jambo kubwa, ni jambo la kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nichukue fursa hii adhimu niwashukuru na kuwapongeza timu nzima ya Wizara ya Maji ikiongozwa na Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso, lakini pia Naibu Waziri wake, kaka yangu Mheshimiwa Mathew Kundo, Katibu Mkuu Engineer Mwajuma, CEOs na MDs wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji. Kipekee salamu zangu za pongezi ziwaendee maafisa wanaosimamia huduma za maji Mkoa wa Mbeya. Mimi jimbo langu linahudumiwa na taasisi mbili: Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mbeya CPA. Gilbert Kayange pamoja na Engineer Hancy Patrick kwa upande wa RUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nijielekeze kwa kusema mambo mawili; hatuwapongezi kwa sababu wapo Wizara ya Maji, tunawapongeza kwa sababu ya kupandisha utoaji wa huduma ya maji kufikia zaidi ya 92.5% mijini na 85.2% vijijini. Pia, tunawapongeza kwa sababu ya kupunguza malalamiko ya wateja kwenye sekta ya maji, jambo ambalo lilikuwa limekithiri miaka ya nyuma. Tunawapongeza kwa sababu ya kuja na mpango mkakati wa Gridi ya Taifa kutatua changamoto ya maji nchi nzima na tunaamini suala hili lilikamilika linaenda kuwa mwarobaini wa changamoto za maji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza kwa sababu wanatupa uthabiti na matumaini ya Watanzania wote kwa kuwa na uhakika wa huduma ya maji kwa sababu maji ndiyo huduma pekee ambayo haina mbadala. Tunawapongeza kwa sababu wanatii maandiko. Ukisoma Kitabu cha Waebrania 13:17 kinasema; “Watiini viongozi wenu, na kushika amri zao, wao huchunga roho zenu usiku na mchana na watatoa ripoti ya utumishi wao mbele ya Mungu, kama mkiwatii watafanya kazi zao kwa furaha la sivyo watazifanya kwa huzuni.” Wao ndiyo wanampa furaha Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sababu hana stress, wanaisimamia vyema Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa pamoja na salamu zangu niseme mambo machache: Mbeya Vijijini, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetuletea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Hata hivyo, ninaomba nimwombe Waziri, Mheshimiwa Aweso tuna miradi saba inayoendelea, hii miradi inasuasua tunaomba fedha ili wakandarasi warudi site kwa ajili ya kutekeleza mradi. Mathalani Mradi wa Izyra ambao upo 55%; Mbagala Iyunga, Mwakasita upo 50%; Mradi wa Masoko upo 40%; Ilea - Ihango upo 80%; Iwalanje-Tembela 75%; na Isuto kisima pale kipo 95%, tunaomba fedha ili miradi hii ikatekelezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, ninaomba nijikite na nijielekeze kwenye ushauri. Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha uliopita ilikuwa inadai taasisi za Serikali shilingi bilioni 61. Mkoa wa Mbeya tuna Mradi wa Maji wa Mto Kiwira una takribani zaidi ya shilingi bilioni 119. Mradi huu unaendelea vyema lakini tunaamini hizi fedha ambazo tunadai kwenye taasisi zingepatikana leo hii Wanambeya wote na huu mradi unaenda Mbeya Vijijini kwenye kata tano: unapita Swaya, Utengule Usongwe, Nsalala, Kata ya Bonde la Songwe, Iwindi na baadhi ya maeneo ya karibu ya Mshewe. Zikilipwa hizi fedha miradi kama hii ingemalizika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tukubaliane kuiunga mkono Wizara ya Maji na sisi tumwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kama Mtendaji Mkuu wa Serikali aziandikie taasisi hizi ziweze kulipa madeni haya ili miradi mingine iendelee kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuna utaratibu lazima tukubaliane, umewasilisha na saa hizi tunaelekea kuweka ushirikiano mkubwa na sekta binafsi. Sekta binafsi haijalishi ni mtu mmoja au watu sita, kuna utaratibu kupitia Sheria ya Maji inayosimamia rasilimali za maji Namba 11 ya Mwaka 2009, kwa wateja kuchimba visima. Utaratibu huu umekuwa na malalamiko kidogo na muda mwingine taasisi kukinzana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mteja anatakiwa aombe kibali cha kuchimba kisima kwenye Bodi za Mabonde, lakini waliokasimiwa kisheria ya kutoa huduma hasa mijini ni Mamlaka za Maji. Sasa Sheria ile inaeleza, mteja apewe kibali mahali ambapo mtandao haujapita. Mheshimiwa Waziri, ninaomba sana uliangalie hili, watekelezaji wa kutoa kibali cha uchimbaji wa kisima wapewe Mamlaka za Maji. Wao ndiyo wanajua wapi hakuna maji, wapi tutapeleka maji na lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimalizie. Hii itaondoa migongano, lakini pia itaondoa migongano ya taasisi kwa taasisi lakini pamoja pia na wateja kupata huduma kwa haraka kwa kuondoa bureaucracy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ninaomba kwa heshima sana kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)