Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Patali Shida Patali (1 total)

MHE. PATALI S. PATALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga soko la uhakika la mazao Mbeya Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Patali Shida Patali, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na soko la uhakika la mazao ili kuboresha sekta ya nyama na lishe katika Jimbo la Mbeya Vijijini, imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 14.3 kiwanja namba 26 kitalu 13A katika Kata ya Utengule Usongwe kwa ajili ya kuchakata mazao ya nyama kwa kujenga kiwanda kikubwa cha kisasa. Eneo hilo limekabidhiwa kwa taasisi ya Serikali inayosimamia masuala ya uwekezaji (TISEZA) tarehe 26/02/2026 ili kupata mwekezaji wa kujenga kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, eneo kwa ajili ya kujenga soko kubwa la mazao la kisasa limetengwa katika Kata ya Nsalala Kiwanja Na. 831 Kitalu 13F chenye ukubwa wa ekari 6.1. Taratibu za kuandaa maandiko ya miradi na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo zinaendelea, ambapo shilingi milioni 20 zimetengwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi hayo.