Supplementary Questions from Hon. Patali Shida Patali (3 total)
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami nipate kuuliza swali la nyongeza kutoka kwenye swali la msingi Na. 138. Je, ni lini Serikali itaupandisha hadhi Mji Mdogo wa Mbalizi kuwa Mamlaka ya Mji kamili, ikizingatiwa mji huu umekidhi vigezo vyote ikiwepo idadi ya watu, uwezo wa kujiendesha wenyewe? Pia mji huu umeomba kupandishwa hadhi muda mrefu sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwa niaba ya Wanambeya Vijijini nipate majibu ya Serikali. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO): Mheshimiwa Spika, ninawaelekeza uongozi wa Mkoa, husika wakamilishe michakato yote ambayo imeainishwa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuanza mijadala kwenye ngazi ya Mitaa na Kata, Wilaya kwenye vikao vya RCC, vikao vya DCC. Watakapokamilisha wawasilishe TAMISEMI kama utaratibu unavyotaka, TAMISEMI tutatuma timu na tutafanya mapitio ya vigezo hivyo na kama vigezo vitakidhi, mamlaka itachukua hatua zinazofuata. (Makofi)
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa mwaka wa fedha uliopita na mwaka wa fedha huu unaoendelea Serikali imekuwa ikitekeleza miradi sita Jimbo la Mbeya Vijijini ambayo ni Mradi wa Maji Zira, Mbagara - Yunga Mradi wa Maji wa Masoko Mradi wa Maji wa Ilea pale Ihango, Mradi wa Maji wa Ranje, Tembela pamoja na Mradi wa Maji wa Kisima, Isuto. Miradi hii imesimama kutokana na wakandarasi kukosa fedha za kuendelea na miradi hii.
Je, ni lini Serikali itawalipa wakandarasi hawa ili wakandarasi warejee site kutekeleza miradi hii Wanambeya Vijijini wapate maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Patali Patali, Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kwamba tunamalizia miradi yote ya maji ambayo inaendelea na hivi sasa tuna miradi 1206 ambayo inaendelea kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa Mheshimiwa Patali Patali ambaye nakumbuka nikiwa katika ziara alikuja kushiriki katika mradi ule wa Kiwira ambapo tunatambua kwamba ushirikiano wa Mbeya yote na ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunaendelea kutekeleza na utekelezaji na kuanzishwa kwa miradi hii ya 1206 ni ishara tosha ya dhamira ya kweli ya Serikali ya kuhakikisha inaleta huduma ya maji safi na salama na toshelevu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wakandarasi kuendelea kulipwa tumeshakwisha weka mkakati kuanza kuwalipa awamu kwa awamu kulingana na vipaumbele vya maeneo husika, lengo ni kwamba tukitekeleza mmoja ukakamilika ukatoa matokeo basi tunakuja na mradi mwingine. Hatuwezi kuipeleka miradi yote kwa pamoja ikakamilika kwa pamoja, lazima mkakati wetu sasa Waheshimiwa Wabunge tuelewe kwamba tumekubaliana tuweke awamu kwa awamu ili Wabunge wote waweze kuguswa katika maeneo yao, tusije tukajikuta tunapeleka fedha zote katika miradi yote katika eneo moja na eneo lingine likakosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge wa Mbeya Vijijini tutakupatia vipaumbele ambavyo tumeviweka katika mkakati wetu na wewe utashiriki kushauri ili tuone namna gani tutafanya vizuri zaidi kwa ajili ya wananchi wako wa Mbeya Vijijini. Ahsante sana.
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninaiomba sana Serikali kuharakisha mchakato huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, 85% ya wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini ni wakulima na wafugaji. Mathalani kwa mwaka huu unaoisha, umezalisha zaidi ya tani 700,000 za mazao ya chakula. Wakati huo mahitaji yetu ni tani laki 200,000...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, ninaomba uulize swali.
MHE. PATALI S. PATALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi ni kuiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa hilo soko, lakini pamoja na kiwanda kilichoahidiwa kwa ajili ya uchakataji wa nyama ili wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini wapate soko, sehemu ya kwenda kuuzia mifugo yao kama mbuzi na ng'ombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Ninatambua hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia hotuba yake alikemea vikali uuzaji wa mazao uliozidi kiwango, almaarufu kwa jina la lumbesa. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuleta Muswada hapa Bungeni ili tupitishe sheria ya udhibiti wa kudumu suala hili la lumbesa ambalo limekuwa likisababisha maumivu makali sana kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini pamoja na wananchi wa Mbeya Vijijini kwamba Serikali inatambua kwamba zaidi ya 85% ya wananchi wa Mbeya Vijijini ni wakulima na wafugaji, na ndiyo maana tayari tumeshaandaa eneo kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kisasa cha nyama. Eneo hili limeshakabidhiwa kwa TISEZA kwa ajili ya kufanya utaratibu wa kupata mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili lipo, linaendelea na utaratibu wa kufanyiwa kazi na Serikali. Mara utaratibu utakapokamilika, tutapata mwekezaji ambaye atajenga kiwanda hicho ili kuboresha huduma za nyama katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, eneo la mazao ya nafaka pia limetengwa kwa ajili ya utekelezaji huo na tutakwenda kutekeleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha tunakuwa na masoko mazuri kwa ajili ya bidhaa za mifugo na mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na lumbesa, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa ya lumbesa na inaleta hasara kwa wakulima. Wizara ya Viwanda na Biashara na Serikali kwa ujumla imeendelea mara kwa mara kutoa miongozo, maelekezo na kusimamia ili kudhibiti lumbesa kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea wazo lake la kuwa na Mswada wa Sheria na sisi kama Serikali tutalifanyia kazi kuona uwezekano wake. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti lumbesa na kuleta faida kwa wakulima.