Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Rahma Riyadh Kisuo (2 total)

MHE. DKT. REGINA C. MALIMA aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuongeza ajira kwa wahitimu wa
vyuo kupitia miradi ya kimkakati, viwanda vidogo, vya kati na
programu za ubunifu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA
MAHUSIANO (MHE. RAHMA R. KISUO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa nafasi hii.
Awali ya yote, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mlezi
kwa siku ya leo na siku zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, ninapenda kumshukuru
Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani isiyo kifani kwangu
kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kazi, Ajira, na Mahusiano. Nimwahidi kwa uwezo wa Mwenyezi
Mungu Mkuu nitafanya kazi hii kwa dhati, ari na uthabiti ili kuleta
matokeo bila kusahau ushirikiano mzuri sana na Bunge hili.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujibu swali zuri la
Mheshimiwa Dkt. Regina Christopher Malima kwa niaba ya
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, na
Mahusiano, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahakikisha wahitimu
mbalimbali wa vyuo wanapata nafasi za ajira kupitia miradi ya
kimkakati inayotekelezwa nchini kwa miaka ya hivi karibuni,
ambapo zaidi ya ajira 35,000 zilizalishwa katika ujenzi wa Reli ya
SGR, zaidi ya ajira 10,000 katika Mradi wa Ujenzi wa Bomba la
Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki, zaidi ya ajira 10,000 katika Ujenzi
wa Bwawa la Mwalimu Nyerere la Kuzalisha Umeme, zaidi ya ajira
1,500 katika Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Msalato, Dodoma, zaidi ya ajira 1,500 katika Ujenzi wa Daraja la
JPM (Kigongo – Busisi), na zaidi ya ajira 3,000 katika upanuzi wa
Bandari Dar es Salaam.
2
30 JANUARI, 2026
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali imetoa mafunzo ya
uzoefu wa kazi maarufu kama Internship kwa wahitimu 29,902 wa
ngazi mbalimbali za elimu pamoja na kuongeza ujuzi kwa
wafanyakazi 19,075 katika sekta za hoteli, madini, usafirishaji,
kilimo na usindikaji wa mazao ya kilimo kupitia Programu ya Taifa
ya Kukuza Ujuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hii inalenga kuwapatia
walengwa ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira. Vilevile,
Serikali imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Mafunzo kwa Vitendo
kwa Wahitimu kwa lengo la kuweka utaratibu wa utoaji wa
mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu ambao unatumika
waajiri wote (Sekta ya Umma na Sekta Binafsi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali imeandaa
Mwongozo wa Kujitolea katika Utumishi wa Umma wa Mwaka
2025 ili kuweka utaratibu rasmi wa kuwapata na kuwasimamia
vijana wanaojitolea katika Taasisi za Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati mingine iliyochukuliwa na
Serikali inajumuisha, kutoa mikopo yenye masharti nafuu na ruzuku
kupitia mifuko ya uwezeshaji kwa wahitimu wanaoanzisha
biashara, na kutoa mafunzo ya ujasiriamali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. CHACHA M. WAMBURA aliuliza:-

Je, upi mkakati wa kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kupitia miradi ya uzalishaji na ujasiriamali ili kupunguza utegemezi wa sekta ya madini – Geita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA MAHUSIANO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, ninapenda kujibu swali zuri la Mheshimiwa Engineer Chacha Mwita Wambura, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mkakati wa kuunda ajira na kukuza uchumi wa vijana kwa kuwawezesha kushiriki katika miradi ya uzalishaji na ujasiriamali, sambamba na kupunguza utegemezi wa sekta ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (MBT), vijana 5,983 wamewezeshwa kwa kupatiwa leseni, mafunzo na mitaji, huku wachimbaji wadogo 658 wakipatiwa mafunzo kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi katika mikoa ya kimadini ya Geita, Mbogwe na Chunya.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatekeleza mikakati jumuishi ikiwemo uratibu wa utekelezaji wa Sera ya Ajira ya Mwaka 2008 pamoja na sera nyingine za kisekta. Vilevile, utekelezaji wa programu za kuwawezesha vijana kama BBT na BBT-LIFE, pamoja na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kupitia Halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kukuza ujuzi wa vijana, kuratibu fursa za ajira ndani na nje ya nchi, na kuhakikisha masuala ya ajira yanajumuishwa katika mipango ya maendeleo, hatua zinazolenga kukuza fursa za ajira na kuimarisha uchumi wa vijana kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuwasilisha.