Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SALEHE M. MHANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Kilimo kwa siku ya leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia nianze kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi makubwa ambayo anaendelea nayo katika sekta hii ya kilimo hapa nchini. Hili halina ubishi, uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi inaonekana na mambo yanaendelea kwa kiwango ambacho kinaleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Geodfrey Chokolo akisaidiwa kwa umahiri mkubwa na Naibu Waziri ndugu yangu Mheshimiwa Silinde, Katibu Mkuu pamoja na timu nzima ya Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuunga mkono hoja ya hotuba ya Wizara ya Kilimo na ninaunga mkono kwa maana kwamba katika Taifa letu na katika nchi yetu tumekubaliana kwamba kilimo ni uti, na Mheshimiwa Waziri ameboresha siyo uti wa mgongo, utii wa mgongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo ni kwamba, hapa leo tunazungumzia hatima ya maisha ya Watanzania, na hatima ya uchumi wa Taifa letu. Kwa maana kwenye kilimo kule ndiko kunakofanya tunaweza kuishi, kupata chakula, utoshelevu wa chakula, usalama wa chakula, halikadhalika, kilimo sasa hivi ni biashara. Kwa hiyo, hapa tunazungumzia uchumi wa wananchi wetu kwa mtu mmoja mmoja, Taifa na tunazungumzia suala la uchumi katika pato letu la Taifa kwa maana ya kuweza kuuza nje ya nchi na kupata fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muktadha huu, ninaomba nichangie hotuba hii katika eneo muhimu sana ambalo limeelezwa na Waziri katika hotuba yake ya bajeti, lakini kwa msisitizo mkubwa nimeisikiliza sana hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge. Eneo ambalo tunatakiwa kuliwekea uzito sana katika suala la kilimo, mapinduzi ya kilimo, ni suala la umwagiliaji. Kilimo tunahitaji tutoke kwenye kilimo cha msimu twende kwenye kilimo cha mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hakuna njia nyingine zaidi ya uwekezaji kwenye miundombinu ya umwagiliaji. Katika miundombinu ya umwagiliaji, kwanza tukubaliane kwamba kupanga ni kuchagua, lazima fedha itoke iende kwenye eneo hilo. Miradi mingi tumeelezwa hapa, kwanza tuwe na miradi ya kimkakati tusipunguze miradi mingi, tukubaliane twende na miradi kadhaa ambayo tunaitekeleza mpaka ilete matokeo twende hatua nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, kuna miradi kadhaa ambayo leo imeelezwa hapa, ukienda huwezi ukakuta kuna mradi ambao sasa hivi unazalisha mara mbili kwa msimu, haupo. Kwa hiyo, bado safari ni ndefu. Hapa, nilikuwa niombe na kuishauri Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, mamlaka, na Wizara ya Fedha; kati ya jambo ambalo tunatakiwa kwenda kumwachia alama Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye nchi hii ni kwenda kuitoa Tanzania kutoka kwenye kilimo cha msimu wa mvua kwenda kwenye kilimo cha msimu wa muda wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fursa ya kuilisha Afrika, tuna fursa ya kuilisha dunia, na hata yanayoendelea duniani haya kwa upande mwingine kwa Tanzania sisi hii ni fursa. Leo hata hii miradi inayotekelezwa, tunatekeleza miradi ya kukinga maji ya mvua, baada ya mvua, ikiondoka, miradi ile na yenyewe haifanyi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri tuchague miradi. Kuna mabonde ambayo unajua kabisa ukisema Usangu, ukisema kule Mwamburu - Katavi, ukisema kule Morogoro, una hakika kwamba tukitengeneza miradi, Kilindi kule Tamota, miradi ambayo ukaweka miundombinu ya mabwawa, maji yakatengenezewa miundombinu ya umwagiliaji, tukazalisha kipindi cha mvua na kipindi cha kiangazi, haya ndiyo maana halisi ya miradi ya umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba hapa niweke msisitizo kwamba kilimo ni maji. Hakuna msamiati mwingine kwamba tutazalisha bila kuwa na maji. Kilimo ni maji na hili ninaomba niliwekee msisitizo kabisa kwamba hata nikiishia leo kuchangia hapa, nitakuwa nimesaidia Taifa letu kwamba kilimo ni maji na bahati mbaya sana tunapoteza maji. Mvua zinanyesha, tunalalamika hapa. Kuna jambo halijakaa sawa sawa kwenye mipango na kwenye utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende tukatumie hii baraka ya Mwenyezi Mungu kutupa mvua kwa ajili ya faida ya uzalishaji wa mara mbili mara tatu kwa msimu tuwe sisi ndiyo ghala la chakula kama inavyoelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka kulichangia leo ni suala zima la zana za kilimo. Eneo la zana la kilimo nalo hili ni eneo muhimu sana katika kuleta mapinduzi ya kilimo hapa nchini, na nipongeze sana jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara husika ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ninaomba sana Jimbo la Kilindi, Wilaya ya Kilindi, lile ndiyo eneo la uzalishaji kwenye ukanda wa kaskazini likiungana na wenzake wa Kiteto. Ninaomba sana katika ule mpango wa kusambaza matrekta, power tiller maeneo haya yapewe kipaumbele kwa sababu ndiyo yanayolisha ukanda mzima wa kaskazini na nchi jirani ya Kenya na maeneo mengine. Ninaomba tulitumie hili eneo kuwekeza katika miundombinu au vitendea kazi kama matrekta, power tiller kwa wakulima wetu ili tuhakikishe kwamba tunakwenda kuongeza tija, kuongeza uzalishaji na mwisho wa siku kuinua pato la wananchi wetu na pato la Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe rai na nitoe ushauri kwamba pia katika eneo hili twende kwa maeneo tuangalie vipaumbele vya maeneo. Ninaomba tukubaliane, tukiamua kwenda kwa utaratibu wa kwamba hivi vitu tunatapanya, peleka huku kimoja peleka huku viwili, havitoi matokeo, hatupati tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tukubaliane, tunaposema tunapeleka hapa, tupeleke kitu kilete matokeo, na yale matokeo yatoe tija, tuhamie sehemu nyingine. Tutafika kwenye maeneo yote, lakini kwa kwenda kwa utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la masoko, na hapa nilikuwa ninaomba kuzungumzia NFRA. Moja ya chombo ambacho kinaweza kikaleta na kikachachusha masoko ya ndani ni kupitia NFRA. Changamoto ya NFRA; mfumo wa upatikanaji wa fedha kwenye NFRA unabishana na masuala ya masoko kwa wakulima kule kwenye maeneo yetu. Ukipeleka fedha mwezi wa Tisa, hiyo fedha haimnufaishi mkulima. Kuna watu wamekusanya, wameweka kwenye store ndio wanaonufaika na fedha zile za NFRA, lakini mkulima ambaye amehangaika amejishughulisha na kilimo kwa miezi yote ile, anajikuta ameangukia kwenye walanguzi, amepata hela ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku unapokuja kupeleka NFRA fedha, zinakwenda kunufaisha watu ambao hatujakusudia. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anakusudia kwenda kupeleka tabasamu kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa upatikanaji wa fedha za NFRA utazamwe, ikibidi apewe fedha mwezi wa Pili, au wa Tatu tayari kwa maandalizi. Mavuno yanaanza mwezi wa Tano na wa Sita, wawe wameshajiipanga, wahakikishe kwamba ule utaratibu tuliouweka wa kupeleka mifumo ya ukaushaji mazao tukawasaidie wakulima ili tuiwezeshe NFRA inunue mazao ambayo yamekaushwa vizuri, yanahifadhika, na pia kuweza kuwapa wananchi soko la uhakika na kuleta ushindani kwa wanunuzi binafsi kwa kipindi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuchangia hayo, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. SALEHE M. MHANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa Hotuba ya Makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninaomba kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali kusimama katika Bunge lako Tukufu kuchangia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pongezi kwa viongozi wetu Wakuu wa Nchi yetu wakiongozwa na Jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sambamba na Mheshimiwa Makamu wa Rais na pia Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema, “Kusema sana si hoja, kutenda ndiyo hoja”, hii ndiyo dhima ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunashuhudia namna siku 100 tu katika awamu hii ya pili ya kipindi chake cha pili anachomaliza, ahadi alizozitoa na utekelezaji wake huhitaji hata kutafuta kwa tochi. Unaona kwa vitendo na kwa matokeo na haya ndiyo ambayo Watanzania wanampenda na wanamtumainia sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa na mimi kujielekeza kwenye kuchangia hoja ya Hotuba ya Waziri Mkuu. Katika kuchangia hoja hii, mimi nimejipa muda mwingi sana wa kupitia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini ikiongozwa na dhima ile ya Dira ya Maendeleo ya Taifa letu ya 2050 ambayo Bunge hili na bajeti hii ambayo tunaanza kuijadili leo, inatuanzishia safari hiyo chini ya Mpango wa Nne wa 2026/2027 na 2030/2031 yenye maudhui yanayosema: “Mageuzi katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutafsiri dhima hii ya mageuzi katika kukuza uchumi, moja kwa moja kwa mawazo yangu na kwa fikra zangu, nimeyatafsiri maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa miaka mitano iliyopita. Huu ni mwendelezo, kazi ilishaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, ninataka kufungamanisha, kwa mfano tu, mageuzi makubwa yaliyofanyika katika uwekezaji wa bandari zetu, Bandari ya Tanga, Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Mtwara, tayari ni safari ambayo imeanzishwa katika kutekeleza Mpango huu wa Nne wa Dira ya Maendeleo wa 2050.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mageuzi yale yaliyofanywa ndiyo yanayokuja kuunganishwa na jambo linalozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani. Mapinduzi makubwa ya bandari na mimi kama Mheshimiwa Mbunge ninayewakilisha wananchi wa Jimbo la Kilindi kutoka Mkoa wa Tanga na Tanga tuliguswa na uwekezaji mkubwa wa zaidi ya shilingi 400,000,000,000 kwenye uwekezaji wa Bandari ya Tanga ambayo sasa inatoa matokeo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema, kiunganishi kikubwa katika zoezi hili, hatua hii ni uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya barabara. Pengine niseme tulichelewa, ilibidi wakati ule hatua ya uwekezaji kwenye bandari ilitakiwa iende sambamba na uwekezaji mkubwa kwenye barabara zetu hasa hizi za TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuzungumzia Barabara ya kimkakati ambayo inaanzisha kuunganisha Bandari ya Tanga kutoka Tanga – Segera, Segera – Korogwe, Korogwe – Handeni na hatimaye kutoka Handeni – Kibirashi - Kiteto – Chemba – Kwa Mtoro, Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii korido ambayo ilikuwa inatakiwa ipokee makontena, mizigo kwa njia rahisi kabisa, ilitakiwa iwe hii Barabara ya lami ambayo kipande chake kilichobaki ni kutoka Handeni – Kibirashi – Kiteto – Chemba – Kwa Mtoro. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara aliyofanya katika Jimbo letu la Kilindi na akajionea kwa macho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaanzisha kwa maono hayo akiwa anaangalia uwekezaji mkubwa wa bandari, akaanzisha ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Handeni – Kibirashi – Chemba na akaanza na kilometa 20 mwaka 2023 kutoka Handeni – Mafuleta, hatimaye akaagiza tena zijengwe kilometa 30 kutoka pale Mafuleta kwenda Kileguru kilometa 30, jumla ni kilometa 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali, twende tukatekeleze maono haya ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumechelewa, hivi tunavyozungumza, katika zile kilometa 20, kilometa 10 tu zimekamilika kwa miaka minne. Ninaomba sana, katika kutafsiri mageuzi katika kukuza uchumi, barabara hii ni ya muhimu, ni ya kimkakati na katika bajeti hii inayoanza katika kutekeleza Dira ya 2050 na huu Mpango wa Nne wa dira hii. Hii barabara iwe kipaumbele katika mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inaondoa sasa hivi mizigo inayoshuka Bandari ya Tanga inalazimika tena kurudishwa Dar es Salaam kwenye mizigo mingi inayopokelewa kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Huu ni mgogoro, lakini njia rahisi ambayo ilikuwa tungekuwa tumeanza mapema na sasa hivi hatujachelewa, tukiamua tunaweza tukaenda kwa speed, tukaitoa Barabara ile mpaka Kibirashi, Kibirashi ikaendelea kwenda Kiteto, Kiteto kwenda Chemba kule Kwa Mtoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pale Singida ianzishwe Bandari ya Kwala namba mbili, ipokee mizigo pale iingie kwenye SGR, iendelee na safari kwenda mikoa mbalimbali na nje ya nchi kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na barabara hii kwa kiwango cha lami kwa Wanakilindi bado tuna uhitaji na hii wilaya ina changamoto kubwa sana za barabara hizi hizi za TANROADS kutoka pale Songe kwenda Gairo, lakini kutoka Songe kwenda kwa Lugulu, barabara hizi hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe ushauri twende na mipango na kazi zinazotoa matokeo, tutoke sasa kwenye barabara kujengwa kwa kiwango cha tope, tuwe na mpango madhubuti wa kila mwaka kwamba hizi barabara zifanyiwe matengenezo kwa kiwango cha moram au changarawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayoendelea sasa hivi ya surface grading unaondoa hata ile changarawe ya mwaka juzi, mwaka jana unaleta tope, unajaza mvua inakuja tunarudi palepale, fedha za umma zinapotea na matokeo hayaonekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatamani nione tuje na mpango kwa TANROADS tuseme sasa matengenezo ya kawaida yawe kwa kiwango cha changarawe, tuone ma-tipper yanamwaga changarawe kipindi ambacho tunatengeneza barabara ili ziweze kupitika mwaka mzima, lakini huu mpango wa surface grading tunapoteza fedha, hakuna matokeo na mwisho wa siku tunazorotesha uchumi wa wananchi wetu na uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la TARURA, Jimbo la Kilindi lina mtandao wa barabara za TARURA kilometa 1,520. Bajeti ya TARURA bilioni 2.5, jiografia ya Kilindi ni ya milima na makorongo mapana. Mimi nina madaraja nane, Daraja la Lukole, Tamota, Sambu unakwenda pale Gombero, unakwenda kule Saunyi, unakuja hapa Vunila, barabara moja limefanyiwa usanifu ni bilioni 4.3 wastani, unapokea bilioni 2.5!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kata nne zimejifunga hazifikiki; Kata za Kilwa, Lwande, Hagwi, Saunyi na changamoto yake ni madaraja. Sasa niulize kwa bajeti ya bilioni 2.5 hiki kitendawili kinakwenda kuteguliwa vipi? Kwa hiyo, ninaunga na Wabunge wenzangu wote, tuhakikishe kwamba TARURA inaongezewa na bajeti na tufanye zoezi, sasa hivi tunakwenda ku-phase out REA, ule mpango wa REA na usimamizi wake urudi kwenye barabara za TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo la barabara ninaomba niishie hapo, ninaomba sana tuchukue juhudi na tuamue, kupanga ni kuchagua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ninaomba niingie kuhusu migogoro ya ardhi ya wakulima na wafugaji. Ukurasa wa 27 umeeleza vizuri sana. Hili ninataka niwaambie miongoni mwa Wilaya zenye changamoto kubwa na Kilindi imo, lazima tukubali tatizo na ili uweze kutatua tatizo ni lazima utambue kwamba nina tatizo na hili tatizo ninaamini ni la nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo ninataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu na Mwenyekiti wa Bunge na Serikali, migogoro ya wakulima na wafugaji, lipo tatizo la msingi, lakini tu hatutaki kuli-address. Wapo wafugaji wakorofi wachache ambao wao wanaleta matatizo kwa ukorofi wao, lakini hiyo siyo hoja ya msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya msingi ni kwamba sisi tuna mifugo, tuna watu wanaojishughulisha na shughuli za ufugaji, hizi ni shughuli za kiuchumi lakini hakuna sehemu za malisho. Wote tunatoka kijijini hapa, asimame mtu aseme mifugo yetu kwenye kijiji chetu inalishiwa sehemu fulani, asimame hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonyesha hapa tuna mifugo milioni 76, mifugo maeneo rasmi ya malisho hayapo nini kinatokea? Mifugo inahudumiwa kwenye maeneo yenye matumizi mengine kama ya kilimo hifadhi na kadhalika. Sasa utakwepaje migogoro hiyo kama hali ndivyo ilivyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali hili jambo ni kubwa, ni mtambuka, linahitaji kukaliwa chini kufanya tafakari. Leo hata kule kwenye matumizi yaliyotengwa matumizi bora ya ardhi, kwenye maandishi utaona kumetengwa maeneo ya mifugo, kwenye uhalisia kule hakuna huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, lazima tukakae tutafute ufumbuzi wa eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kwa Afisa Mifugo atakupa takwimu ya mifugo na ni kweli kwenye kata hiyo mifugo ndiyo hiyo, ukienda atakupa idadi ya majosho na ukienda utayaona, ukienda atakupa idadi ya minada na ukienda utaiona, nenda kamwambie nipeleke kwenye malisho ya mifugo, hutapata jibu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Salehe…
MHE. SALEHE M. MHANDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe wito au nitoe ushauri kwa Serikali, Wizara husika TAMISEMI, Ardhi, Mifugo tukae tutafakari huu uchumi, lazima hii shughuli iwe na maeneo rasmi ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)