MHE. SALEHE M. MHANDO aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka fedha za awamu ya pili kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vya Vuju, Mswaki na Negero katika Jimbo la Kilindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salehe Mbwana Mhando, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya vya katika kata za kimkakati kote nchini. Katika kipindi cha miaka mitano Serikali imejenga jumla ya vituo vya afya 487 vikiwemo Vituo vya Afya vya Vuju, Mswaki na Negero katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya tathmini na kuainisha jumla ya vituo vya afya 364 vyenye upungufu wa miundombinu muhimu. Aidha, vituo 111 vimetengewa bajeti ya shilingi bilioni 23.37 katika mwaka 2026/2027 kwa ajili ya ukamilishaji ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ambayo imetengewa shilingi milioni 200 kukamilisha Vituo vya Afya Vuju na Mswaki. Aidha, Kituo cha Afya Negero ni kati ya Vituo vya Afya 120 vya kimkakati vilivyopokea shilingi milioni 250 kupitia bejeti ya nyongeza ya mwaka wa fedha 2024/2025. Ujenzi umehusisha jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), choo cha nje na kichomea taka na ujenzi upo hatua ya ukamilishaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa awamu na kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya vituo vya afya ili viweze kutoa huduma muhimu ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura kwa akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.