MHE. SALEHE M. MHANDO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na majibu hayo naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kupitia mapato yake ya ndani imeanza ujenzi wa vituo vya afya katika Kata ya Kilindi Asilia, Kata ya Masagalu pamoja na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya cha Kwedibomu.
Je, Wizara ina mpango gani wa kupeleka fedha kwa ajili ya kwenda kuunga mkono jitihada za Halmashauri ya Kilindi ili kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ili viweze kutoa huduma kwa wananchi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka wa fedha 2021 Kituo cha Afya cha Vuju, Kata ya Tunguli kilipokea jumla ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu; jengo la wagonjwa wa nje, jengo la wodi ya mama na mtoto, pamoja na jengo la upasuaji. Changamoto iliyopo kwenye utekelezaji wa mradi ule ni jengo moja tu la wagonjwa wa nje liliweza kukamilika na majengo mawili; jengo la mama na mtoto pamoja na jengo la upasuaji hayajakamilika mpaka hivi tunavyoongea zaidi ya miaka mitano hayafanyi kazi kabisa. Hali kadhalika Kituo cha Afya Kwediboma kilipelekewa jumla ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa majengo matatu na majengo hayo hayajakamilika mpaka hivi tunavyoongea.
Mheshimiwa Spika, je, Wizara ina utaratibu gani wa ufuatiliaji na uchukuaji wa hatua kwa miradi na vituo vya afya vinavyopelekewa fedha na majengo yake kutokukamilika kwa muda mrefu kiasi hiki na inaonekana kuna sababu za ubadhirifu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Mhando, Mbunge wa Jimbo la Kilindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni utaratibu wa halmashauri kutenga fedha mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea kujenga miundombinu katika vituo vyetu vya afya, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI itaendelea kutenga bajeti ili kuhakikisha vile vituo ambavyo tayari halmashauri imevianzisha kuweza kuvisaidia kuweza kukamilisha vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la pili la hatua ya ufuatiliaji katika vile vituo vya afya ambavyo tayari Serikali ilielekeza fedha.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa ufuatiliaji upo Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, tuna timu Kitengo Maalum cha Ufuatiliaji na nimuelekeze Mkurugenzi wa Halmashauri aweze kufuatilia vituo hivyo ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevianisha hapa na atuletee taarifa Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI ili tuweze kuchukua hatua stahiki.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ushirikiano dhati ili kuhakikisha huduma lengwa za kuwahudumia watu wetu katika Jimbo la Kilindi zinafikiwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.