Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. PASCAL L. LUTANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ambayo ninaipenda. Maisha yangu, suti yangu hata tai niliyoivaa ni kwa sababu ninachimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru sana Waziri wa Madini, kaka yangu Mheshimiwa Mavunde (Wakili Msomi) kwa kazi nzuri ambayo ameifanya tangu aingie kwenye hii Wizara na Katibu wake ndugu yangu, kaka yangu Samamba na wasaidizi wao wote mikoani huko RMOs kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Kwa niaba ya wachimbaji wenzangu ambao walinituma niwe sauti yao humu ndani, ninamshukuru sana Waziri na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ninataka niseme neno moja katika Mithali 31 lile fungu la 29, Selemani alisema neno hili: “Binti za watu wengi wamefanya mema mengi, lakini wewe umewapita wote.” Kwa nini nimetumia hili fungu, kama leo Biblia ingeliandikwa, inawezekana ingeandika hivi “Marais wengi wamefanya kazi nzuri, lakini wewe Mheshimiwa Dkt. Samia umefanya vizuri zaidi.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kuamini Mheshimiwa Dkt. Samia, huwa ninataka tu niulize sijui ni Mungu tu alituletea, ninapopiga picha Waheshimiwa Wabunge alipoingia Awamu ya Tano akiwa Makamu, Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, akiwa Rais alikuja kutusikiliza sisi wachimbaji. Rais Bina wa wachimbaji alikuwepo, tuliitwa tukaenda Dar es Salaam ndiyo mara ya kwanza sisi wachimbaji kwenda kukaa ukumbi mzuri pale unaitwa Nyerere nini, mtamalizia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wote walifurahi. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu, Rais alimpa jukumu la kutusikiliza wachimbaji ambao tulikuwa tumeenda tukiwa na kero 31. Zote alizipokea pamoja na Rais wa Awamu ya Tano wakasema hizi kero zote tunazimaliza. Kwa kweli hakuna Rais kama huyu mama mwenye huruma kwa wachimbaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka niwaombe Wabunge wenzangu hata wasipokubali leo ipo siku kwa sababu maneno yangu yanaingia kwenye Hansard, watakubali kwamba Rais wa Awamu ya Sita amefanya mengi kuwapita wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Waheshimiwa Wabunge niwape picha tu, mama huyu ndiyo ametoa leseni nyingi kuliko Marais wote. Waziri huyu Mheshimiwa Mavunde (Wakili Msomi) ndiyo ametoa leseni nyingi kwa wachimbaji kupita Mawaziri wote. Hilo halitoshi, Rais huyu ndiyo ameanzisha Benki ya Tanzania kuwa na dhahabu. Tuna subiri jambo likwame tumalizane nalo, ni Rais Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mama huyu nimtaje vipi? Niseme huyu Rais msikivu na mnyenyekevu. Watu wamekuwa wakihangaika juu ya utafiti, wachimbaji wanakata kuku, wengine wanakwambia nimeoteshwa hapa kuna dhahabu, unakuta na wewe unamwambia ana moko na koleo nimeoteshwa, anaenda kuchimba hajui anaenda kuchimba nini. Huyu mama amekuja na suluhusho, Waziri na wataalam wamekuja na suluhisho, wanakwenda kufanya utafiti nchi nzima ili sisi wachimbaji tuendelee kuwa mabilionea. Nani kama Samia. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Pascal, ahsante sana muda umekwisha.
MHE. PASCAL L. LUTANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimalizie kwa dakika moja.
NAIBU SPIKA: Malizia sekunde 30.
MHE. PASCAL L. LUTANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja tu. Ndugu zangu ninataka kusema mazuri yaliyofanywa tusiyafumbe kwa mabaya. Nimwombe Waziri, kule Geita bado tuna changamoto ya mrabaha wa mawe, umebaki mkoa mmoja ninaomba aondoe haraka. Hii technical support Wabunge wote huku wamesema, sisi kwa niaba ya hawa wachimbaji tunasema hatuitaki, ninaomba akalimalize. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)