Hotuba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa Ufunguzi Rasmi wa Bunge la Kumi na Tatu, Tarehe 14 Novemba, 2025
MHE. JUMA KHAMIS SADIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwanza kabisa, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kutuwezesha kufika siku hii ya leo tukiwa na hali ya uzima na afya zetu zikiwa zinaendelea kuwa nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na wewe kwa kunipatia nafasi hii. Ninawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Donge kwa kunirejesha tena kuwa Mbunge wa Jimbo la Donge kwa Awamu ya Tatu sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tutakubaliana hapa kwamba, Mama Samia, ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amedhihirisha ndani ya Bunge Tukufu hili na ulimwengu kwa ujumla kwamba, yeye ni mama bora. Mama wapo wengi, lakini sio kila mama anakuwa mama bora. Mama bora ni yule ambaye anawajali watoto wake, anayewanasihi watoto wake, anayewalea vizuri watoto wake na anayewaonesha njia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia Suluhu Hassan hotuba aliyoitoa hapa Bungeni amedhihirisha kwamba, yeye ni kiongozi bora na nina sababu, na kila mmoja ana sababu zake hapa za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukienda uki-google na wale waliokwenda vyuo vikuu, sifa za kiongozi bora mojawapo ni kuwa msikivu na nyingine ni kuwa na maarifa, hekima, busara, uvumilivu, ujasiri, uhodari na maamuzi. Zote hizi zinaelezea sifa za kiongozi bora. Ukiangalia hii speech ambayo Mama Samia ameitoa hapa amedhihirisha kwamba, yeye ni kiongozi bora. Amewahimiza watoto wake, Watanzania, na wajukuu zake juu ya umuhimu wa kusimamia amani na usalama wa nchi yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika umuhimu wa amani ndiyo kitu pekee, bila ya amani, bila ya usalama, hakuna chochote cha maendeleo kitakachofanyika. Hata hao wataalamu wa mambo ya usalama duniani, wa mambo ya ulinzi duniani, wote wametoa kipaumbele kuhusiana na suala la umuhimu wa usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano. Realists, liberals, kila mmoja hapa ana mtazamo wake katika kusimamia amani. Liberals wanaamini katika suala la umoja na mshikamano, cooperation, institution. Realist wao wanaamini katika force kusimamia amani. Realists, akina Hans Morgenthau, wanaamini katika kusimamia amani hakuna mbadala, wao wanaamini force ndiyo approach pekee ya kusimamia amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia, Rais wetu amekuja Bungeni akatuhutubia akawaasa vijana na watoto wake, Watanzania kwamba, changamoto ni wataalamu wanaamini conflict is unavoidable. Changamoto hizi na migogoro ni mambo ambayo hayawezi kuepukika. Je, tunatumia approach gani katika kutatua migogoro yetu na matatizo yetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama Samia approach pekee ambayo amewaasa watoto wake katika kutatua changamoto zetu tutumie diplomatic means, ndiyo njia pekee itakayotusaidia. Ndiyo maana akawaambia Mawaziri wake atakaowateua na wengine ambao tayari amewateua kwamba, Waziri yeyote lazima awe kiongozi shirikishi, vijana wa Tanzania washirikishwe katika maeneo mbalimbali. Nawapongeza sana Mawaziri walioteuliwa, ni kweli wanamtendea haki mama, wanafanya kama alivyowaagiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naseme vijana wenzangu, wengine kwenye ujana tunaondoka huko sasa. Nawaambia vijana, nchi hii ni ya kwenu nyie, usikubali kushawishiwa, ukashawishika kuiharibu nchi yako. Mama anajionesha kwamba, yeye ni mzalendo wa Taifa lake na kila mzalendo wa Taifa lake, mwenye akili timamu, atakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Rais kwamba, lolote liwalo, tusione kwamba, leo sisi Tanzania tuna amani. Wenyewe wanasema ukiona kimeundwa kinaelea, ujue kinafanyaje? Yupo muundaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu huko hawalali kwa kuitunza amani hii. Hii ndiyo value ya nchi yetu, kwa hiyo, nimesema nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anawaasa watoto wake wanasimamia amani, umoja na mshikamano wa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni suala la umuhimu wa muungano. Ni ukweli usiopingika, mimi bahati nzuri ninatokea upande wa pili wa Muungano wa Zanzibar, upande wa Zanzibar wote tunakubaliana kwamba, muungano wetu huu unafaida kubwa kwetu na njia pekee ya kutatua changamoto zile za muungano ni kama Mawaziri wetu wanavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia muungano huu, na niseme ukweli, hata ukienda duniani huko kuna nchi nyingi ziliungana, wanatamani na walishindwa ule muungano wao kudumu. Tanzania pekee mpaka leo hii ndiyo tunaongoza katika muungano wetu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine aliloligusia Mheshimiwa Rais ni suala la kusambaza huduma za jamii, ikiwemo mambo ya ujenzi. Tukubaliane, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dodoma ya mwaka 2010 mpaka 2020 ni tofauti na Dodoma ya Mama Samia leo. Huo ndiyo ukweli. Dar es Salaam ya mwaka 2010, mimi nilikuwa Mbunge hapa toka 2010 mpaka 2020, mimi juzi nimepotea Kisasa. Pale Kisasa nikazungukazunguka wee, naitafuta Martin Luther, ile njia ya Waziri Mkuu, nikazungukazunguka maana ilikuwa usiku. Ni kwa sababu, mabadiliko makubwa ambayo alimeyafanya Mama Samia kwa kipindi cha muda mfupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukitembea barabarani huko utakuta barabara ya lami mgongo wa ndizi. Natoa mfano, barabara za namna hii unazikuta maeneo machache sana, ni Tanzania na Zanzibar. Mama Samia na Dkt. Husseni Ali Mwinyi wamekuja kufanya mabadiliko makubwa na nikwambie ukweli, unajua watu walivyokuwa wanamwangalia Mama Samia hawakutarajia atakuja kufanya mambo makubwa kama haya ambayo ameyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mama amedhihirishia umma, ameudhihirisha ulimwengu kwamba, mama ni mama. Mama ana maamuzi, ndiyo maana hata ukifuatilia katika statement zake unajua hasa huyu ni kiongozi wa aina gani? Huyu ni Amiri Jeshi Mkuu. Huyu ni Mkuu wa Nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri mimi nimewahi kuwa mwanajeshi. Nataka niseme siyo kila kiongozi huwa ana maamuzi. Mimi nimekaa na viongozi wengi, sitaki kuwataja majina hapa, wengine tulifikia stage tukawa tunagombana kwenye vikao, tukaonekana hatuna adabu. Ni kwa sababu, unamkuta hana maamuzi, unamshauri hili hawezi. Mama huyu amekuja kuonesha yeye ni kiongozi wa namna gani? Nataka nikwambie kupata ujasiri wa kutamka lile neno, who are you? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kila mmoja ana ujasiri wa kuja kulitamka lile neno, tena hadharani, yes, kwa sababu, kuna watu wamejiona kwamba wao ndio wababe wa dunia kwamba, wanachokitaka wao ndicho hicho hicho. Mama amekuja, ametuonesha mwanga wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)