Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Onesmo Merdson Mnkondya (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwanza kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu jioni ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pengine ni siku ndefu kwangu au kwa sababu nitazungumza dakika karibu kumi, nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mungu aliyenipa uzima na kunipa nguvu za kuweza kunifikisha siku ya leo ili niweze kuchangia. Pia ninawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Mbozi walioamua kunichagua na kunifikisha hapa Bungeni ili niweze kuwasemea, kuwawakilisha niseme tu nitawakilisha uwezo ninao, nguvu ninayo na nia ninayo, nitafanya kazi usiku na mchana kwa ajili ya wananchi wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wengi tumemshukuru na ni kweli Rais wetu inawezekana hasemi sana, lakini kazi zake zinaonekana. Kazi zinaonekana anazozifanya Mheshimiwa Rais, Majimboni mwetu ni mashahidi wote Wabunge wanaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru Waziri Mkuu ameanza ziara na kwangu ameshafika amefanya kazi kubwa na ile ndiyo ambayo tunataka hata kule chini kwa watendaji, kule chini wote wacheze mpira mmoja. Sina shaka na hilo Mawaziri wapo hapo watamsaidia Waziri Mkuu, watamsaidia Rais, sisi tutawakimbilia wao usiku tutakwenda kwao, mchana tutakwenda kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia Chipando anasema amefika mpaka nyumbani kwa Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu Profesa Shemdoe, kama mambo hayaendi, mimi nitakwenda. Ninawashukuru Wabunge pia wamefika hapa kwa kweli wamefanya kazi kubwa, hongera sana Wabunge kwa kuchaguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie, wakati ninagombea nafasi hii, wakati ninaomba ridhaa kwa wananchi niliwaahidi jambo moja na wao walinituma kwa jambo kubwa moja ambalo limekuwa ni mfupa kwa Jimbo langu la Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni suala la barabara. Barabara zetu za Mkoa wa Songwe za Jimbo langu hasa Jimbo langu nikianza na Barabara ya Mlowo – Kamsamba. Hii barabara imekuwa na shida miaka nenda rudi, ninaweza nikasema toka uhuru hii barabara, tunaomba ijengwe kwa kiwango cha lami, kilometa 130 toka uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amevunja rekodi na alipokuja nilimwambia Mama umevunja rekodi endelea kushikilia hapo hapo. Tumesaini barabara ile kwa kiwango cha lami kilometa tano kutoka Jimbo langu na kilometa tano kutoka kwenye Jimbo la mwenzangu Condester Sichalwe, Jimbo la Momba ili mkandarasi aanze Momba na mwingine aanze Mlowo wakutane katikati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajiuliza kilometa tano, kilometa 10 barabara yenye kilometa 130 tutamaliza lini? Ni zaidi ya miaka 13 tukienda kwa mtindo huo, miaka 13 tunajenga tu. Sasa niiombe Serikali kwa kuwa barabara hii mimi kama Mbunge nilishawaambia wananchi wangu wanielewe kabisa, nitapambana na mambo mengine, lakini Barabara ya Mlowo – Kamsamba ndicho kitakachokuwa kipaumbele chetu kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka hii mitano tunaomba barabara hii ianze kujengwa ili iweze kuisha na wananchi waondokane na adha wanayoipata kilometa 130, tuipe mkakati siyo kilometa tano hizi, ninashukuru sana kwa hizi kilometa tano, lakini naomba sasa watupe kilometa za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu ni kilometa 65, Jimbo la mwenzangu ni kilometa 65 jumla 130, barabara hii Waziri wangu na rafiki yangu kutoka kule Mheshimiwa Deus Sangu, yeye anajua barabara hii tunakutana naye kule, Wabunge hapa hakuna Mbunge hajala mchele wa kule Kamsamba, unatoka kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge hapa wanajua kabisa tuna dhahabu ya kahawa inatoka barabara hiyo, tuna mahindi yanatoka barabara hiyo, tunayo maharage na kila kitu, hilo ndiyo ombi langu tu nimesimama kuomba barabara hii, kaka yangu Naibu Waziri Kasekenya na Waziri Ulega wanaona ninavyowafuatafuata ofisini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge waliotangulia kwenye Jimbo lile kila mmoja alipiga kelele barabara ile, sasa sijui wanataka nifanyaje? Nitahakikisha ninagombana nao, anisaidie barabara ile kaka yangu Kasekenya. Rais alishaagiza ijengwe yote kwenye kampeni, Waziri Mkuu amekuja pale ameagiza mkandarasi alipwe fedha za kianzio bilioni 3.8 mpaka sasa hayajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tupo kwenye Bunge la Bajeti, ninaomba kabla hatujarudi mkandarasi ashuke pale site aanze kufanya kazi wananchi wanatusubiri, watatusubiri mpaka lini? Tutakuwa tunawaambia itajengwa itajengwa, sasa safari hii nimekuja Mbunge kijana. Nimeahidi kuchapa kazi, sijaahidi siasa ninataka tukafanye kazi barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo pia barabara nyingine hasa hii ipo TARURA na nimeiombea Barabara ya Mlowo – Mpito – Isansa ina kilometa 13.6 iko chini ya TARURA. Kwa kweli, kwa upande wa TARURA tuombe sana waongezewe fedha za kutosha ikiwezekana kipindi hiki cha mvua Mawaziri wangefanya ziara kwenye Majimbo ndipo watatambua shida tulizonazo na barabara hizi za TARURA, tuna shida mno. Niiombe barabara hii tuipandishe hadhi kutoka TARURA iende TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki mvua zinanyesha kule kuna hospitali, kuna kituo cha afya kimejengwa na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan lakini barabara haipitiki. Wananchi wataendaje kutibiwa kule? Akina mama wajawazito wataendaje kule? Niombe sana kipindi hiki tuhakikishe tunaipa TARURA fedha za dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawauliza jamani vipi? Wanasema hakuna fedha za dharura tunafanyaje, hivi hapa ninawaza Ijumaa nirudi kwenda angalau nitafute hata chochote mfukoni mwangu nikaweze kurekebisha rekebisha mashimo kule, hivi kweli? Niombe tuziangalie hizi barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zingine za TARURA ni Barabara ya Itepula – Shasya – Halungu iangaliwe barabara hii. Sisi ni wakulima tunataka tusafirishe mazao yetu kutoka vijijini kuja mjini barabara hamna, tunaomba sana tuangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wa Msanyira wananisikia hapa barabara yenu nimekuja juzi haipitiki, niko hapa kuhakikisha ninaiomba Serikali iweze kupitika. Watu wa Intentula, watu wa Isani, watu wa Isela barabara ile na yenyewe itakuja kupitika nitamfuata rafiki yangu, kaka yangu Profesa Shemdoe analifahamu, yeye ndiye mlezi wangu, ninaomba anisaidie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kelele pekee sasa hivi kule ni barabara. Watu wa Mwanjelwa wamenipigia simu wanataka Barabara yao ya Mwanjelwa kwenda kule Shitungulu. Nitampeleka Waziri apafahamu, lakini nazo barabara nyingi na muda wangu umeniishia, ila kilio changu kwa miaka hii mitano ni Barabara ya Mlowo – Kamsamba ninahitaji ijengwe sasa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nichukue nafasi hii kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ambayo imewasilishwa na Wizara ya Nishati na Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na ninakiri kupokea umeme kwangu kule vitongoji 39, japo nina vitongoji 80 vimebaki, lakini kwa mpango wa Serikali nina uhakika kuelekea mwaka 2030 kama ambavyo Ilani ya chama chetu inasema vitakuwa vimekamilika. Kwa hiyo, sina shaka na Mheshimiwa Waziri, nimeona mipango yake kwenye Wizara kwamba vitongoji vyote vinakwenda kufikiwa na umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama leo hii kwanza kwa sababu kuu ambayo inatupata sisi watu wa Songwe. Watu wa Songwe hatuna umeme wa uhakika. Hivi nilivyosimama hivi leo umeme Mkoa wa Songwe ni mara nyingi sana unakatika katika na umekuwa ni maarufu kwa Mkoa wetu wa Songwe. Yaani unaweza ukasema tuko gizani sasa. Hili jambo sisi kama Wabunge kwa kweli limeleta shida sana kwa mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumewaambia wananchi wetu kwamba muwe na subira. Sisi ni wawakilishi wenu tutakwenda Bungeni kuwasemea na ikiwezekana hivi nimesimama Mheshimiwa Waziri, unapokwenda kuwasilisha hotuba yako (kumaliza) ninakuomba tu; kwa namna ambavyo tuna tatizo Mkoa wa Songwe la katikakatika ya umeme. Hii inatokana na kwamba sisi watu wa Songwe tunachukua umeme kutoka pale Mbeya. Kuna kituo kimoja kinaitwa Mwakibete cha kupozea umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukimuuliza hata mtoto mdogo leo ukimuuliza Mwakibete ni nini, atakuambia ndiye anayetukatia umeme. Yaani hiki kituo cha kupozea umeme kimekuwa ni maarufu mno. Kwetu imekuwa ni kero. Matangazo yote yanayokuja na watu wa TANESCO, tatizo Mwakibete. Ni kweli, sasa kama mtu mwingine anatu-control sisi Watu wa Songwe, tutashindwaje kukosa umeme? Control zote zipo kwao, wakiwa na jambo lao lolote lile watakata tu umeme Mkoa wa Songwe tunakosa umeme. Laini yote tunakosa umeme, tena siyo Mbozi tu peke yangu, wilaya zote za Mkoa wa Songwe majimbo yote ya Mkoa wa Songwe, Wabunge wako hapa wanajua hilo, kwamba kelele ni umeme Mkoa wa Songwe. Tunakosa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wakulima kuna uzalishaji wa hali ya juu kule. Wafanyabiashara, viwanda vidogovidogo haviendelei wajasirimali wadogo hawawezi kufanya kazi kwa sababu umeme haupo, siyo wa uhakika. Ninaamini atakuja na mpango wa dharura wa kutusaidia watu wa Songwe wakati tunasubiri huu Mradi wa TAZA unaokwenda kukamilika. Kwa kweli umeme Mkoa wa Songwe hauridhishi. Hatuko salama kwenye umeme. Ninaomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili na atusaidie tupe majibu. Hivi wananchi wa Mkoa wa Songwe wanasubiri Serikali inakwenda kusemaje. Sina shaka na Waziri anakwenda kuwajibu na kutuma wataalam huko wakatuangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana ndiyo, toka tuchukue hii laini mpaka sasa, wakati tunaanza na hii laini ya kutoka Mbeya kuja Songwe ilikuwa na watumiaji 68,000. Sasa watumiaji wameongezeka kwenda 144,000. Ni pongezi kwa Serikali kuongeza watumiaji, ndiyo hivyo vitongoji vimeshapata umeme na ongezeko ni watu 80,000. Sasa, bado tunatumia laini ile ile na miundominu ile ile. Hapana, Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo ninataka nishauri sasa, kupitia mradi ambao unaelekea kutukomboa sisi watu wa Songwe wa TAZA. Mradi huu ni mzuri, ni mpango mzuri wa Serikali, lakini mradi huu ulikuwa umepangwa ukamilike tarehe 21 Mei, 2026, bado mwezi mmoja. Hivi ni kweli unakwenda kukamilika? Tatizo linakuja kwa wakandarasi wanaotekeleza huu mradi. Inawezekana hawawasimamii vizuri. Sasa, Mheshimiwa Waziri hawa wakandarasi wasimamiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe Waziri mfano wa wakandarasi hawa; mkandarasi kutoka Iringa kuja Kisada amekamilika hana tatizo. Mkandarasi kuja hapa Kisada sijui panaitwa Sasada, kuja Mbeya…

MBUNGE FULANI: Kisada.

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Kisada yes, kuja Mbeya yuko slow mno, yuko taratibu sana. Mpaka hivi ninavyozungumza, kati ya nguzo 495 amesimamisha nguzo 199, bado nguzo 296, atamaliza? Huyu ndiye atakayechelewesha. Mpango mahsusi uende kwa huyu mkandarasi, kama ni kusimamiwa asimamiwe. Atatuchelewesha sisi watu wa Songwe kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitoka hapo mkandarasi wa kutoka Mbeya kuja kwetu Songwe hadi Nkangamo, Kituo cha Kupozea Umeme yuko vizuri, bado nguzo sita tu. Huyo hatuna shaka naye.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine litakalochelewesha mradi huu ni kile Kituo cha Kupozea Umeme Nkangamo, mpaka sasa mkandarasi hajaanza kusafirisha zile transformer kutoka bandarini kwenda Songwe na tunajua zile transformer zilivyo na uzito, sidhani kama ana gari za kwenda kusafirisha zile transformer kwa wakati. Ninaamini hatakuwa na uwezo huo. Sasa, nini cha kufanya ili kumsaidia na transformer moja ya kusafiri ni kati ya siku 28 na kuendelea? Ili kumsaidia Serikali yetu, ninaamini ina uwezo mkubwa tu, ipeleke gari zenye uwezo wa kubeba mizani mizito ili aweze kusaidiwa huyu mkandarasi, aweze kuleta transformer akamilishe mradi wake pale Nkangamo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye uwasilishaji wa Mheshimiwa Waziri, kwa kweli ninampongeza sana. Wakati ninaendelea kutafakari namna gani tutakavyopokea huu umeme sisi Watu wa Songwe, kama sasa tuna changamoto na Kituo cha Kupooza Umeme cha Mwakibete Mbeya na sasa wameturuka vilevile kituo cha kupooza umeme kutoka Mbeya kimeenda mpaka wapi? Nkangamo!

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninawaza hivi umeme huu utatoka Nkangamo uanze kurudi tena Songwe. Makao Makuu ya Songwe jamani yako Mbozi. Tunapaswa kuwa na substation mahali hapa tu-control wenyewe ule umeme. Sasa uende kule urudi huku, hivi inawezekana? Itakuwa ni hali ile ile. Kitakachotokea kule Nkangamo ndicho kitakachotuathiri huku. Mpaka tuje tu-solve hilo tatizo muda ushakwenda. Ninamwomba Mheshimiwa Waziri, kutoka Mbeya tatizo lilikuwa lile lile. Waje watuwekee substation Mbozi Makao Makuu pale, watu wa-control pale ili tusipate shida ambayo tunaipata sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua kule Nkangamo ni mahsusi kwa ajili ya Zambia, ni mahsusi kwa ajili ya wenzetu wa Rukwa na kuendelea, lakini kwetu hatutapata manufaa. Wakati kengele ya kwanza inagonga, ninaomba nimalizie kwa kusema kwanza ninampongeza sana Meneja wa TANESCO Mkoa, ni kijana mzuri, kijana mdogo kama mimi tu. Kazi anayoifanya, pamoja na kukatikakatika umeme ni nzuri, anaitwa Engineer Chonya. Anafanya kazi nzuri usiku wote, kwanza anatoa ushirikiano mzuri, ila anazidiwa na wenzetu wa kule kwenye kituo ambacho kinatuletea shida hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huyu Meneja, Mkoa wetu wa Songwe hatuna Ofisi ya TANESCO. Hivi ninavyozungumza anatoka kwenye nyumba ya kupanga ndio ofisi, jengo la kupanga ndio ofisi. Kweli kwa mkoa wenye hadhi kabisa, kesho kutwa tu tunaenda kupata Manispaa, tuendelee kutumia ofisi ya kupanga, kweli? Hawa watu wana kiwanja. Mheshimiwa Waziri wajengee ofisi, ili kuwanusuru na wenyewe angalau wawe na uwezo wa kufanya kazi, wawe na ofisi yao badala ya kupanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, meneja huyu ndiye anayefanya kazi pia, kama meneja wa wilaya yetu, lakini kazi yake ni nzuri, wamjengee ofisi. Ninaomba sana Serikali ichukue jambo hili la umeme kukatikakatika kwa Mkoa wetu wa Songwe, kama jambo la dharura kwa Wanasongwe tuondokane na giza ambalo tuponalo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa nafasi ambayo umenipa na mchango ambao nimeutoa kwa rafiki yangu Mheshimiwa Waziri. Ninaamini Wanasongwe wanakwenda kunufaika kuanzia kesho na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa nafasi ambayo umenipa ili niweze kuzungumza na Wizara yetu ya Kilimo, ambayo ina Waziri bora kabisa na Naibu Waziri. Ninawapongeza kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kwenye Wizara yetu ya Kilimo, ninaweza nikasema ndiyo Wizara pekee ambayo imeajiri watu wengi kwenye Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumza kwa niaba ya Wanambozi ambao wamenituma na leo nifikishe ujumbe huu kwenye Wizara yangu muhimu kabisa hii, kwa Jimbo langu la Mbozi peke yake, waliojiajiri kwenye kilimo ni 80%. Maana yake nini, ni kwamba kilimo ndiyo ajira kwa Jimbo langu la Mbozi, tunategemea kilimo kwa asilimia hizo zote ambazo nimezisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, wao walichoniagiza kwenu Mawaziri wangu, mwaka jana walipata shida ya changamoto ya mbolea, wamepata changamoto ya mbegu, wamepata changamoto ya madawa, lakini asilimia kubwa wamepata changamoto ya mbolea aina ya DAP. Sasa Mheshimiwa Waziri, tunapomaliza msimu huu wa kilimo, tunaanza msimu mpya mwingine. Tunaelekea kumaliza msimu lakini tunaunganisha msimu kwa jimbo langu, msimu wote tunalima sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwaka jana changamoto ile kidogo imeleta tafaruku kwa jimbo langu. Wananchi wamelalamika kama nilivyowahi kuuliza swali hapa, wameingia hasara na hakuna mtu wa kuwafidia, ni nani wa kwenda kuwafidia na kwenda kuwaomba kwa msimu huu unaoanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji mbolea iwahi kwa wakati, tunahitaji mbolea ya kupandia iwahi kwa wakati, tunahitaji tena mbolea ambayo ni bora, hakuna mbolea feki. Tunahitaji madawa bora, tunahitaji mbegu bora ili tumlinde mkulima. Ili tumlinde nani, mkulima. Bila kufanya hivyo tunahatarisha uchumi wa Wanambozi, uchumi wa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo mbolea zinapokuja tumeruhusu watu kuuza mbolea feki, hatumlindi mkulima, unajiuliza TFRA wako wapi, unajiuliza wako wapi walinzi hawa, wasimamizi wa bei, lakini wasimamizi wa ubora wa mbolea wako wapi? Hawapo! Wabunge tunaanza kuhangaika madukani siyo sawa, watu wa TOSCI wako wapi kwenye mbegu, watu wa TIFA wako wapi kwenye madawa hawasimamii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza mbolea Jimbo la Mbozi inauzwa shilingi 100,000 hadi shilingi 90,000, hivi ndivyo bei ya mbolea ya ruzuku ambayo Rais Samia ametupatia ndiyo bei hiyo. Kwa nini wasitoke tamko marufuku kuuza mbolea kwa bei ya juu, twende tuuze mbolea kwa bei elekezi na bei elekezi ipo wazi. Niombe tumlinde mkulima, tuwalinde wakulima wetu, tuwalinde baba zetu, tuwalinde vijana wetu ambao wanakimbilia kujiajiri wanapokuta mbolea shilingi 100,000 watajiajirije? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda ninaomba nishauri lifuatalo: Mwaka jana kwenye huu msimu kampuni ya TFC imekuwa mkombozi mkubwa sana, kampuni hii ndiyo kampuni pekee imetuagizia mbolea ya DAP tani 50,000 pekee yake, kampuni zote zilinyamaza. Ninaomba wakakae na kampuni hizi nyingine pia, wakazungumze kilimo, wakazungumze biashara wakazungumze maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huohuo hii kampuni, ninaomba nishauri kwa Mheshimiwa Waziri, waendelee kuisimamia na kama kuna ruzuku waliyosambaza mbolea hawajalipwa, walipwe waagize mbolea mapema kwa ajili ya wakulima wa Mbozi na Watanzania, lakini niombe ikiwezekana wawa-support, wawape mtaji wawawezeshe, kwa sababu wana uwezo wa kufanya kazi ya kutuletea mbolea bora kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, TFC wanapoagiza mbolea tunahitaji mbolea iwahi, wawahi kuagiza na wakulima wawahi kuipata mbolea. Kuna mlolongo mkubwa kwenye uagizaji wa mbolea, taratibu za manunuzi na mlolongo wa manunuzi kwenye Taifa letu yanaeleweka, watu hawa wanaponunua mbolea wananunua kwenye Mataifa mengine....

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Naibu Spika, wananunua kwa wafanyabiashara wakubwa, ninaomba nimalizie sekunde.

NAIBU SPIKA: Malizia sentensi yako ya mwisho.
MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Naibu Spika, wanaagiza kwa wafanyabiashara wakubwa, wale wafanyabiashara wakubwa hawazijui taratibu zetu, ninachokiomba wawape fedha wawaondolee mlolongo mrefu wa kuagiza mbolea, habari za NeST aachane nazo kwenye suala la mbolea tu ikiwezekana wakaagize mbolea kwa faida ya Watanzania kwa faida ya Wanambozi ili tupate mbolea kwa wakati. Wakati wanasubirisubiri mbolea huwa inapanda.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana.

MHE. ONESMO M. MNKONDYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja lakini dakika ni chache. (Makofi)