Supplementary Questions from Hon. Paschal Inyasi Chinyele (4 total)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Mitaa hii mitano na siyo Kata, Mitaa hii mitano ilipimwa kama vijiji mwaka 1973. Je, ni hatua gani Serikali inachukua kuwanusuru wakazi wa Kata hii ya Mbalawala wapatao takriban 12,000 ambao wanategemea ardhi hii kwa maisha yao ya kila siku? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wakati Serikali inajiandaa kutwaa Bonde la Mzakwe iliwafidia wakazi wa vilivyokuwa vijiji vya Mzakwe na Mchemwa, baadhi kuwahamishia katika Kata ya Chahwa ambayo sasa hivi iko kwenye Jimbo la Mtumba. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafidia wakazi wa mitaa hii ya Kata ya Mbalawala ili wapishe Bonde la Mto Ruvu kama ilivyowafidia waliokuwa wakazi wa Vijiji vya Mzakwe na Chahwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. JAFAR R. SEIF): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Inyasi, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na swali la pili, kwa maana kwamba sisi TAMISEMI ndiyo wamiliki wa ardhi, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona namna gani ya kuendelea kuwafidia wale ambao hawajapata kwa sababu Serikali imeendelea kutoa fidia katika maeneo mengi sana nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Ardhi kuona namna gani tunaweza tukafikisha maendeleo haya kwa wananchi wetu kwa maana ya kwamba vijiji vimeshapimwa toka mwaka 1973, tuone namna gani sahihi ya kuendeleza eneo hili. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini Serikali itatekeleza mpango wa ujenzi wa viwanda katika kongani za viwanda katika kata za Nala pamoja na Mpunguzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwa kuwatetea wananchi wa Dodoma, hususan wananchi wa Nala na wananchi wa Mpunguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wetu wa miaka minne, tume-commit kuanzisha miradi saba ya kielelezo (National Flagship Programs). Katika ile miradi saba ya kielelezo, tunakuja kuanzisha kongani ya viwanda eneo la Nala ambayo kimsingi tunaweka pale viwanda vya kuchenjua dhahabu kwenye madini ambayo ni rare na critical, kwa mfano lithium, cobalt, nickel na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo la Mpunguzi tumelitenga kama eneo la mkakati kwa sababu Mpunguzi wanazalisha sana zabibu. Kwa hiyo, ninamwondoa mashaka Mheshimiwa Chinyele, Mbunge wa Dodoma Mjini, kwamba hili lipo kwenye mpango wetu wa miaka mitano. Pia, tumeliingiza na kwenye mpango wa mwaka mmoja, tumelitengea bajeti. Ninashukuru. (Makofi)
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakazi wa Mitaa ya Kata za Chang’ombe, Nkuhungu, Mnadani pamoja na Nala, wanakabiliwa na uhaba mkubwa sana wa maji. Hii ni kutokana na kuzidiwa kwa Mfumo wa Maji wa Mzakwe. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi ya maji ya Nzuguni, Nala pamoja na Zuzu ili kuepusha uhaba huo wa maji? Katika kata hizi, vipo vituo vya afya kama Chang’ombe pamoja na Zuzu, lakini havina maji. Ni lini Serikali itashughulikia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jiji la Dodoma ambapo nikiri kabisa kwamba hata ofisini kwetu ameshakuja mara kadhaa, ili kuendelea kuwasemea wananchi wa Jimbo la Dodoma Mjini, wakiwemo Wabunge wanaoishi katika Jiji la Dodoma. Mheshimiwa Chinyele, kwenye suala la miradi yetu, tunao mradi wa Nzuguni, Serikali imewekeza zaidi ya shilingi 9,000,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, Nzuguni One ambapo mradi huo umefikia 98% bado tu kidogo ukamilike. Pia tuna Nzuguni Two ambao unaendelea. Tuna mradi wa Nala ambao pia Serikali imewekeza shilingi 4,000,000,000, tunao Mradi wa Zuzu ambao tumeweka shilingi 7,000,000,000 ambapo kwa ujumla wake huo, mahitaji ya Jiji la Dodoma ni lita 160,000,000 mpaka sasa uzalishaji wetu ni lita 80,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi hii mitatu yote itakapokamilika tutaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita 80,000,000 mpaka lita 120,000,000. Maana yake ni kwamba tutakuwa tumefikia zaidi ya 80% ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea na michakato ya miradi hii, na ipo katika hatua nzuri kabisa. Miradi hii itakapokamilika wananchi wa Jiji la Dodoma pamoja na Jimbo la Mtumba itakuwa ina uhakika wa kupata majisafi na salama, wakiwemo Wabunge wanaoishi katika Jiji hili la Dodoma.
MHE. PASCHAL I. CHINYELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi (Dodoma Polytechnic College) katika Mtaa wa Lugala, Kata ya Mbalawala. Je, ni lini Serikali itaanza kuchukua wanafunzi katika chuo hicho ambacho kiko ndani ya Jiji la Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chinyele, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imekamilisha kwa kiasi fulani ujenzi wa Dodoma Polytechnic, na kama Mheshimiwa Mbunge anakumbuka vizuri tulifanya ziara pamoja katika chuo kile na hatua iliyofikia ni nzuri. Kwa hiyo, tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaenda kumalizia ukamilishaji wa chuo kile na matarajio ya mafunzo ni kuanza mwaka huu wa 2026/2027. (Makofi)