Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lutengano George Mwalwiba (2 total)

MHE. TIMIDA M. FYANDOMO K.n.y. MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchumi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. ENG. MUSHAMU A. MUNDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lutengano George Mwalwiba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni swali No. 1,425. Kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Lutengano kwa kuwapambania sana wananchi wake wa Jimbo la Busekelo, na kwa namna anavyowasimamia. Pia ninafahamu Mheshimiwa Lutengano amekuwa akiwatetea sana vijana hata wakati akiwa anahudumu kwenye nafasi ya ukurugenzi kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo tulikuwa wote huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatekeleza mikakati mbalimbali ya kikodi inayolenga kukuza biashara ndogo ndogo, hususan za vijana, na kuhamasisha uingiaji wao katika uchumi rasmi. Miongoni mwa mikakati hiyo, ni utekelezaji wa Mfumo wa Kodi ya Makadirio (Presumptive Tax Scheme) unaolenga walipakodi wadogo wasiokuwa na kumbukumbu sahihi za mapato au vitabu vya hesabu, ambapo masharti yake ni mepesi na yanatabirika ili kuwahamasisha wafanyabiashara kusajili biashara zao na kuanza kulipa kodi kwa hiari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha utaratibu wa kipindi cha neema (grace period) kinachowaruhusu wafanyabiashara wapya kufanya biashara bila kulipa kodi kwa muda wa miezi sita tangu kuanza biashara. Hatua hizi zinalenga kuwapa wajasiriamali nafasi ya kukuza biashara zao bila mzigo wa kodi katika hatua za awali. Hii itaongeza ubunifu, kuvutia wafanyabiashara wa sekta isiyo rasmi kuingia kwenye mfumo rasmi, na hatimaye kuongeza mapato ya Serikali kwa njia endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa vivutio maalumu vya kikodi kwa vijana ili kuchochea uanzishaji wa biashara na ajira, ikiwemo msamaha wa kodi na viwango pungufu, huku ikiendelea kufanya tathmini ya athari zake ili kuhakikisha usawa, ufanisi wa sera, na uendelevu wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 na maboresho yake ya mwaka 2024, Serikali pia inatoa ahirisho la kodi ya mapato (Corporate Income Tax) kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwa biashara mpya (start-ups), hatua inayolenga kusaidia biashara changa kukua na hatimaye kuwa walipakodi wakubwa na endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. LUTENGANO G. MWALWIBA aliuliza: -

Je, lini Serikali itafanya mapitio ya miradi ya maji Busokelo ili kubaini changamoto kwa baadhi ya miradi kutofanya kazi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Lutengano George Mwalwiba, Mbunge wa Jimbo la Busokelo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha mapitio ya awali ya skimu zote 35 zilizopo Jimbo la Busokelo, ambapo skimu 19 zinatoa huduma ya maji ipasavyo wakati skimu 16 zinahitaji ukarabati kutokana na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha uendelevu wa huduma ya maji, Serikali imekamilisha ukarabati wa skimu za maji 12 kati ya 16 zilizobainika kuwa na changamoto ambazo ni Kandete, Lwangwa, Kisegese, Kifunda, Ntapisi, Nswigala, Ikanu, Ipelo, Kalinga, Nyandege, Malyasi na Mpombo ambapo kwa pamoja zimegharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kupitia bajeti ya 2025/2026 Serikali inaendelea na ukarabati wa skimu ya Kabembe sambamba na upanuzi wa skimu ya Ikanu kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 580.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya mapitio na kukarabati miradi yote yenye changamoto ya uchakavu wa miundombinu nchini ikiwemo ya Jimbo la Busokelo kadiri fedha zinavyopatikana.