Answers to supplementary Questions by Hon. Laurent Deogratius Luswetula (12 total)
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Naibu Waziri kijana kabisa. Nina maswali ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kutambua umuhimu wa sekta ya fedha, Serikali imeandaa au kusimamia miongozo ipi ya kuhakikisha wananchi hususan wanawake na vijana wanapata elimu ya fedha ili kuchochea jitihada za ukuaji wa kiuchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali imechukua gani sasa kwa hao watu ambao wamejinufaisha sana kwa mikopo hii yenye riba kubwa? Waingereza wanasema Predatory Loans, lakini sisi tumeitafsiri kama ‘Mikopo ya Kausha Damu’. Kwa maana kwa namna walivyofanya wameweza kabisa wenyewe kujinufaisha na kupunguza kabisa jitihada ya Serikali ya kuwakwamua wananchi kiuchumi hususan wanawake na vijana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Neema Peter. Kwanza ninakushukuru kwa maswali mawili ya nyongeza, maswali mazuri, lakini hii inamaanisha kwamba wanawake wa Dodoma hawakukosea kukuchagua. Kweli Ph.D kichwani ipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo sasa, niseme tu kwamba, Serikali imeendelea kuandaa na kusimamia miongozo na utekelezaji wa sekta ya fedha ili kuchochea uchumi wa wananchi, hasa vijana pamoja na wanawake. Serikali imekuja na mkakati maalum ambao unaitwa Programu ya Elimu ya fedha ya mwaka 2020/2021 – 2025/2026, ikiwa ni mpango maalum wa kutoa elimu kwa wananchi (wanawake wanaume na makundi mengine) ambayo inalenga zaidi kuwawezesha Watanzania kupata uelewa, maarifa na kuwajengea kujiamini katika kusimamia mapato na matumizi na kufanya maamuzi sahihi katika kutumia huduma rasmi za kifedha.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, ninyi mnaweza mkawa ni mashahidi ya kwamba kama Wizara ya Fedha tumekuwa kila mwaka tukiadhimisha maadhimisho ya Huduma ya Wiki ya Kifedha; ambapo tumeanza mwaka 2021 – 2026 (ambapo yamefanyika rasmi tarehe 21 mwezi huu, 2026). Mimi binafsi nikimwakilisha Waziri wa Fedha nimeenda kufungua rasmi maadhimisho hayo ambayo yamefanyikia nchini (Tanga) ili wananchi waweze kupata elimu ya kifedha. Kweli wananchi wa Tanga waliyapokea kwa hali ya juu, walikuwa ni wengi. Hii ni mikakati maalum ya Wizara ya Fedha kuhakikisha ya kwamba wananchi wanapata elimu ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, maadhimisho haya yameanza muda kidogo, tangu mwaka 2021. Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na mikoa mingine imeendelea kunufaika na elimu hii.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, zaidi ya mikoa 16 mpaka sasa hivi tumeweza kufikisha huduma hiyo ya fedha, kuwapa elimu ambapo zaidi ya wananchi 64,000 ikiwemo wanawake 40,000 na wanaume 24,000 wamepata elimu hii kuhusu elimu ya fedha. Vilevile, zaidi ya halmashauri 94 nazo tumepita kuhakikisha kwamba wanapata elimu ya fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika uwekezaji wao, katika uwekezaji na kuingia sasa kuwekeza kwenye mambo yetu ya kifedha ikiwemo uwekaji akiba, mikopo, uwekezaji, bima, Bima-amana, kodi, hati fungani na mengineyo mengi, kwa sababu sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga ipasavyo. (Makofi)
SPIKA: Ahsante!
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, lililenga zaidi kwamba sasa sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga kwa namna gani kuhakikisha kwamba wale wanaokiuka taratibu zilizowekwa sasa wanaweka riba kubwa ili kujinufaisha wao.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, katika mkakati ambao tumesema kwamba tumeandaa rasimu ya kusimamia mikopo ya kidijiti ambayo inatarajiwa kuanza mwaka 2026 na 2027, sisi kama Wizara ya Fedha tumejipanga kuhakikisha ya kwamba taasisi zote zinazotoa mikopo zinafuata taratibu zote. Yeyote anayekiuka tayari tumeshaanza msako huo kuhakikisha kwamba tunasitisha leseni na kufunga kabisa, kwa sababu anakiuka taratibu ambazo Serikali imeziweka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nyongeza tu kwa niaba ya Waziri wa Fedha, tunaiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuendelea kuongeza juhudi zaidi katika udhibiti wa mikopo hii, kuhakikisha kwamba wananchi hawa ambao sasa wanatuamini na Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita wanapata mikopo ambayo sasa inawanufaisha na wala si ile wanayoiita ‘Kausha Damu’ na sisi tumejipanga kuhakikisha kwamba tuko pamoja kuwasaidia wananchi kwa sababu ndiyo wananchi wetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, maboresho ya bandari zetu za Dar es Salaam pamoja na bandari nyingine ambazo shehena zake nyingi zinategemea kwenda nchi za SADC hususani kwa kupitia nchi ya Zambia ambapo ndiyo mlango mkubwa. Maboresho haya yameonekana kuwa na tija sana kiasi kwamba shehena kuongezeka na mpaka magari mengi kupungua kwa ajili ya kubeba mizigo, sidhani kama itakuwa ni sahihi tukiwa tunaendelea kuboresha tu bandari zetu na hatuboreshi mahali ambapo mzigo unakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na maboresho ya bandari kumeleta tija, ni upi mkakati wa Serikali kuona kwamba kituo cha forodha peke yake cha Tunduma hakitoshei kusafirisha mizigo hiyo, hivyo kufanya mrundikano mkubwa sana wa magari pale Tunduma na upotevu mkubwa sana wa mapato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika majibu yake ya msingi amesema ni lazima kuwe na mawasiliano na nchi ya pili, nilitaka kufahamu wameshaanza kuwashirikisha wenzetu wa Zambia kuona pale tulipoenda kumuonesha Waziri wa Fedha kipindi hicho ambaye ni Waziri Mkuu wa sasa. Je, wameshaparidhia kwamba panafaa kujenga kituo cha forodha katika Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mbunge wa Jimbo la Momba kwa kuendelea kuaminiwa na wananchi wake, unapokuwa unaaminiwa ni dhahiri ya kwamba unafanya ambayo ni matarajio ya wananchi, nikupongeze sana, lakini kwenye maswali ya nyongeza ninaomba nijibu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikutoe hofu kabisa Mheshimiwa Mbunge kwamba mazungumzo baina ya nchi hizi mbili yanaendelea vizuri na yana matumaini makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali la pili la nyongeza, ni kweli kabisa Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na maboresho ya vituo vyetu vyote vya forodha kuhakikisha kwamba tunapokea mizigo mingi na kuipeleka sehemu ambayo inahitajika kwenye nchi jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo kwenye kituo chetu cha forodha cha Momba tumeendelea na kuboresha miundombinu kuhakikisha kwamba shehena nyingi na mizigo mingi inapita kuelekea kwenye hizo nchi jirani za SADC na kwa sababu hiyo nikuhakikishie kwamba sisi tumejipanga kuboresha miundombinu hiyo kuhakikisha meli zetu nyingi zinapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nimuagize Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwanza kuwarithisha tathmini hii ambayo ipo mwishoni kabisa na akishajiridhisha kwamba kuna ulazima wa haraka kabisa kuweza kujenga Kituo cha Forodha cha Kakozi basi nimwelekeze ujenzi huo uanze mara moja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. THOMAS M. KITIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa dira hii inasema kwamba itawahusisha wananchi wote, kwa maana uchumi jumuishi na tunapoenda kuianza tarehe 01 Julai, 2026. Wananchi watahusikaje kwa sababu hakuna elimu ambayo imetolewa kwa umma ambayo itawafanya wawe sehemu ya mpango huu na sio wasindikizaji. Je, ni lini Serikali itatoa elimu kwa wananchi wote kabla hatujaanza kutekeleza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni kwa namna gani miradi ambayo itatumika kama benchmark ama miradi ya kielelezo tunapoanza kuitekeleza dira hii tutaanza nayo mwezi Julai, ili wakati tunaendelea basi tuwe tunafanyiana assessment kupitia hiyo miradi ambayo tunaenda kuanza kuitekeleza tutakapoanza kutekeleza dira hii?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nipende kumpongeza sana Mbunge wa Ikungi Mashariki, Mheshimiwa Thomas Kitima, kwa kuendelea kupambania sana wananchi wa jimbo hilo, lakini pia kama mjumbe makini katika Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti.
Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza; niseme kabisa moja ya majukumu ya Wizara yetu ya Mipango na Uwekezaji kupitia Tume ya Taifa ya Mipango kwanza ni kuratibu na usimamizi wa uchumi, kupanga mipango ya maendeleo, pamoja na kutekeleza mipango ya maendeleo ambayo tayari imeshakwisha kuidhinishwa. Hii ni pamoja na kukusanya, kuchakata pamoja na kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo tayari imeidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, mimi niseme ni Naibu Waziri wa Fedha, na sisi kama Wizara ya Fedha, kwanza tumejidhatiti kuhakikisha kwamba Dira hii ya 2050 inatimizwa kwa 100%. Sisi tuko tayari kuhakikisha kwamba fedha ya aina yoyote ambayo inahitajika kulingana na mpango huu wa Dira ya 2050, tuko tayari kupeleka katika Wizara ya Mipango na Uwekezaji, kuhakikisha kwamba maono sasa ya mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi hii unafikia dola za Kimarekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, lakini pia wastani wa kipato cha mtu mmoja mmoja kufikia dola za Kimarekani 7,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kwa namna hiyo nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge wa Ikungi Mashariki, sisi kama Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mipango na Uwekezaji, tuko tayari kuhakikisha kwamba mipango yote ambayo imo ndani ya Dira ya 2050 inatekelezwa bila kikwazo chochote kwa ukamilifu wake.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ameuliza sasa ni kwa namna gani elimu kwa umma tunaenda kuifikisha huko. Kwanza niseme kabisa jambo hili la elimu kwa umma sio jambo la Serikali pekee yake, bali ni jukumu letu sisi kama Serikali, lakini pia na Wabunge wote ambapo tutakapokuwa tunakwenda kwenye majimbo yetu, ni lazima tuhakikishe ya kwamba tunatoa elimu kwa umma ili umma sasa uelewe kwamba Dira hii ya 2050 imebeba maono gani.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Dira ya Maendeleo ya miaka 25 kuanzia Julai 01, Dira ya Maendeleo 2050, kwanza na yenyewe kwa ukubwa wake, hatuwezi kuwakwepa sekta binafsi. Nazo tumezijumuisha kuhakikisha kwamba sekta binafsi zina-play role kubwa kutekeleza utekelezaji wa Ilani ya Dira ya Maendeleo 2050. Pia wenzetu wa Wizara ya Mipango, wana mpango mkakati mzuri sana wa kutoa elimu kwa umma kupitia platform mbalimbali ikiwemo makongamano, social media na vyombo vingine ambavyo vitahakikisha kwamba elimu ya utekelezaji wa Dira 2050 wananchi wanaielewa vizuri ili na wao waipokee kwa ajili ya utekelezaji wa dira hiyo.
Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuwasilisha
MHE. FARAJI B. NANDALA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kundi la vijana ndio kundi lengwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/2050 na Serikali imekuwa ikilielekeza kundi hili kwenda kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo pamoja na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, kundi hili limekuwa likikabiliwa sana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikiathiri shughuli hizi za kiuchumi na kurudisha jitihada za vijana hawa.
Mheshimiwa Spika, swali langu, ni upi mpango wa Serikali kupanga bajeti maalum kwa ajili ya kundi la vijana ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo na uvuvi ambao wanapata changamoto sana za mabadiliko ya tabianchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge; kwanza nimpongeze sana kwa namna anavyoendelea kuwatumikia wananchi wa jimbo lake. Ni ukweli kwamba Serikali kwanza imeendelea kuwawezesha vijana kupitia mifuko mingi ya vijana ikiwemo hata juzi mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwenda kwenye Wizara ya Vijana. Hii yote ni kujali kwamba vijana wanafanya kazi na wanapata mitaji ya kuendesha biashara zao.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tuseme tumejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba kundi hili la vijana tunaliwezesha kwa kiasi kikubwa ili lisitetereke kwa namna yoyote, waweze kujiinua kiuchumi kupitia shughuli zao wanazozifanya za kila siku.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. NEEMA P. MAJULE: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa tunatamani kushiriki kwenye huu uchumi jumuishi. Ni kwa jinsi gani Serikali imejipanga kuweza kushirikisha watu kutoka vijijini, wanawake, lakini vijana watakavyoshiriki kwenye huu uchumi shirikishi. Tukizingatia sana viashiria ambavyo vitawekwa kupima kwamba makundi haya maalumu nayo yameshiriki, hasa kupitia kutafutiwa masoko, lakini utumiaji teknolojia mpya, umilikishwaji wa ardhi, siyo hivyo tu, ikiwepo upatikanaji wa ajira zikiwepo ajira zilizo rasmi na ajira ambazo siyo rasmi, ili huu uchumi jumuishi ambao utatokea, usitokee kutoka kwa wawekezaji wakubwa, lakini na sisi watu wa chini ikiwepo wanawake tuwe tumeshirikishwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimshukuru sana Dkt. Neema Majule kwa swali lake la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza swali hili ni lazima kidogo turejee katika Dira ya Maendeleo ya miaka 25 ambayo imepita ambayo kwa kiasi kikubwa kwanza imefanya vizuri sana. Ambapo mpaka kufikia mwaka 2024, wastani wa pato la mtu mmoja mmoja limeweza kukua zaidi ya mara tatu, kutoka dola za Kimarekani 453 mpaka dola za Kimarekani 1,227 lakini pia umri wa kuishi nao umeongezeka kutoka wastani wa miaka 51 mpaka miaka 68.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo sasa dira hii ya miaka 25 mingine inayokuja, tumejipanga kuhakikisha kwamba makundi yote ya wanawake, vijana, wafanyabiashara, wawekezaji nao wanaenda kuguswa na dira hii ya miaka 25 ambayo tunaenda kuanza nayo tarehe 01 Julai, 2026 mpaka mwaka 2050.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nimhakikishie kabisa Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tumejipanga vya kutosha kuhakikisha kwamba makundi hayo ambayo ameyataja, tunaenda kuyagusa kwa kiasi kikubwa na kuyawezesha kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba wanatekeleza shughuli zao za kila siku, ahsante sana.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa Bunge lako hili ndilo Bunge ambalo litaanza kutekeleza Mpango wa Dira ya Taifa 2050 kwa bajeti hii.
Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inaweka Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kwa kuwa malengo ya dira hii ni makubwa kuliko dira tuliyomaliza kuitekeleza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA) K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Hokororo kwa swali lake nzuri la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama Serikali imejipanga vya kutosha na ndiyo maana imekuja na mpango wa e-Delivery, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, ambao ni mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa mipango na miradi ya maendeleo, hii ni kama database ambayo sasa yenyewe itakuwa inafuatilia. Kwanza miradi yote ya maendeleo ambayo iko katika dira hii, ndio imehifadhiwa hapo, ambayo sasa itakuwa inafuatilia utekelezaji; mradi upi umekamilika, mradi upi umefikia asilimia ngapi, mradi upi unahitaji kitu gani. Ufuatiliaji kwa maana ya planning, monitoring and evaluation, mfumo huu ndio unaenda kumaliza kabisa changamoto hizo.
Mheshimiwa Spika, Wabunge hapa kipindi cha nyuma tulikuwa tunalalamika kidogo kwamba kuna mipango mingine na miradi mingine ambayo inaingizwa kwenye utekelezaji bila mpangilio maalumu. Sasa suluhisho ni mfumo huu wa e-Delivery, ambao unaenda kuhakikisha kwamba miradi yote iliyoidhinishwa ndio inakuwepo hapa. Hiyo mipango yote ikishawekwa italuwa-locked na hakuna mtu ambaye anaweza kuifungua. Lengo na madhumuni tusipate mradi mpya ambao haujaidhinishwa kuweza kuingiwa kwenye mpango kazi wa miradi ambayo tayari imekwisha idhinishwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KAFITI W. KAFITI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na sasa naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na umeajiri wananchi wengi katika nchi yetu ya Tanzania, kwa hiyo suala la kinga ya bima kwao ni ulinzi mkubwa juu ya kilimo wanachokifanya, na kwa kuwa suala hili limeshachukua muda mrefu, sasa nini kauli ya Serikali juu ya ukamilishwaji wa kanuni hizi ili ziweze kusaidia wananchi wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nikiri, ni kweli kabisa kilimo ndicho kimeajiri Watanzania wengi sana ambao wanajipatia kipato na kulingana na umuhimu wake na ndiyo maana kiukweli tumechukua muda mrefu ili kujiridhisha kwamba hizi kanuni zitakuwa rafiki kwa wakulima na Watanzania wote ambao wanajihusisha na kilimo. Kwa maana hiyo, kama ambavyo nimeweza kujibu kwenye jibu langu la msingi, mwaka huu wa fedha utakaonza 2026/2027 ndipo tunaenda kukamilisha utafiti huu na kanuni hizo zitaanza kutumika. Naomba kuwasilisha.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na nia njema ya Serikali ya kutaka kuleta bima katika sekta ya kilimo na mifugo, lakini nataka niulize, kwenye suala zima la mifugo; ni masuala gani makubwa ambayo, kwanza yanaleta tatizo kubwa la kutopata bima ili kabla ya kufikiria kutengeneza kanuni mmeyaona mrekebishe ili kwamba hata mtu akitaka kupata bima isiwe na risk kubwa zaidi katika suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza, kuja na kanuni hizi maana yake hata sisi wenyewe kama Wizara, kuja na hii bima ya kilimo tumeona kabisa kwamba kuna umuhimu wake. Ndiyo maana kabla ya kuingia, kwa maana ya kuleta kanuni, tukasema tufanye utafiti kwa kushirikiana na wadau ili tuweze kupata maoni yao nabaada sasa ya kupata maoni yao, tukishakamilisha, ili tuje sasa na bima ambayo, sasa itakuwa na utekelezaji ambao ni imara.
Mheshimiwa Spika, kwa namna hiyo, nipende tu kumhakikishia Mbunge ya kwamba hapo awali hatukuwa na bima hizo, lakini baada ya kuona sasa kuna umuhimu wa kuwa na bima hizo za kilimo ikiwemo ufugaji na ndiyo maana tukasema kwa haraka na kuchukua jukumu la haraka kufanya utafiti na kwa sababu tuko mwishoni, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba baada tu ya kumaliza, tutafanya mipango mingine na kwa kukaribisha maoni mengine ya wadau, ili kama pengine kanuni zile zina mapungufu, basi tuweze kuzirekebisha kulingana na maoni mengine mapya ya wadau.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.
MHE. FADHILI F. NGAJILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuuliza kwamba, kwenye hizi kanuni ambazo zitaundwa kwa ajili ya bima ya mifugo na kilimo; je, wakulima wadogo au wafugaji wadogo wameshashirikishwa kwa namna gani, kwa sababu tuna tatizo kwenye ufugaji, wafugaji wetu wanapoteza sana mifugo yao kutokana na magonjwa na ajali ambazo zinatokea. Je, sasa wanaingizwa vipi katika mfumo huo wa kupata hizo bima ili tuokoe mitaji hii ya wafugaji wadogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimhakikishie Mbunge kwamba wakulima hawa wadogo ambao anawazungumzia na wao pia ni miongoni mwa wadau ambao tayari tumekwishawashirikisha kuhusu bima hii ya kilimo. Wao wametoa maoni yao na kwa kipindi chote ambacho sisi kama Wizara ya Fedha tumekuwa tukitembea kwenye halmashauri mbalimbali kutoa elimu ya kifedha, moja ya ajenda pia ambayo tunaibeba ni hii bima ya kilimo.
Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba, hata maoni ya wadau na wakulima wadogo haya, nayo yamezingatiwa na kanuni hizi ambazo sasa zitaanza kutumika katika mwaka huu wa fedha 2026/2027. Ahsante.
MHE. LUCY EDWARD MWAKYEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali kwa ajili ya uanzishwaji wa bima hii ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kilimo ndiyo suluhisho la kumkomboa Mtanzania katika ajira, wakiwemo vijana, je, Serikali inaonaje kuongeza kasi ya utafiti katika kukamilisha na kutumika bima hiyo hasa kwa upande wa bima ya mazao, mvua nyingi, ukame, wadudu kwenye mimea, pamoja na dhoruba. Matukio haya yanasababisha wananchi kupata majanga ya asili ambapo bima ikianza kwa haraka walau itampunguzia maumivu mwananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri la nyongeza, kwanza bima hii ya kilimo, nikiri kabisa kwamba imeanza kama miaka miwili au miaka mitatu huko nyuma. Kwa maana hiyo, katika hali ya kawaida kulingana na maoni ya wadau ambayo tumeendelea kuyapokea mpaka sasa hivi, jambo hili na utafiti huu ulitakiwa uchukue muda mrefu zaidi wa miaka hii miwili au mitatu ambayo sisi kama Wizara ya Fedha tunaweza kutumia.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo, yeye ameuliza kwamba kuona namna ya kuweza kuharakisha; kwanza sisi kama Wizara ya Fedha tumeharakisha na kwa sababu hiyo, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, uharakishwaji huo na ndiyo maana tunaenda kutekeleza zaidi, kanuni hizi katika mwaka wa fedha 2026/2027 kuanzia Julai 1, 2026.
MHE. TIMIDA M. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri katika nchi za Umoja wa Ulaya, taasisi zinazofanya kazi na Serikali zinapaswa kufanya malipo ya madeni ndani ya siku 30, lakini pia riba hulipwa moja kwa moja endapo malipo yatacheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali yangu ipo tayari kuandaa Prompt Payment Policy ya Taifa ili kuhakikisha wazabuni, wakandarasi, wafanyabiashara hususan vijana na SMEs wanalipwa ndani ya muda maalum unaotambulika kisheria ili kulinda mitaji ya vijana na wananchi wanaofanya biashara na Serikali? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nipongeze sana Mbunge wa Viti Maalum dada yangu Timida ambaye ni Mbaraza la Vijana wa Taifa kutokea Mkoa wa Mbeya kwa namna anavyoendelea kujenga hoja makini hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirejea kwenye swali la nyongeza, kwanza kabisa miongoni mwa vitu ambavyo hata Kamati yetu ya Bajeti imeweza kutushauri kama Wizara ya Fedha na kama Serikali imetushauri tuweze kupunguza angalau muda wa uhakiki wa madeni ya wazabuni na wakandarasi na watoa huduma mpaka kufikia siku 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi tumeweza kupokea, lakini siku hizi 21 zinaweza zikapungua au kuongezeka kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ukamilifu wa nyaraka, aina ya madeni lakini pia ushirikiano wa wadau kwa maana wadai pamoja na wadaiwa, lakini pia umri wa deni pamoja na wigo wa deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, kama ambavyo nimejibu kwenye swali langu la msingi, tumeendelea kulipa madeni ya wazabuni, wakandarasi pamoja na watoa huduma na mpaka kufikia Februari, 2026 zaidi ya shilingi bilioni 477.6 ambazo tayari wakandarasi hawa na watoa wa huduma wamekwishalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele vikubwa vya Serikali katika bajeti yetu ya mwaka 2026/2027, tumetenga na tumekubaliana kuwa na mkakati wa kutenga shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi, watoa huduma pamoja na wazabuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. MORRIS J. MAKOI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wakandarasi wa nchi hii wanadai fedha nyingi kama ambavyo ametamka Mheshimiwa Waziri, lakini wakandarasi wa ndani hawaruhusiwi kudai malipo yao pamoja na riba, kinyume na wakandarasi wa nje ambao hudai malipo ya madeni yao pamoja na riba.
Je, Waziri ana kauli gani kuhusiana na madeni ya wakandarasi wazawa wanaodai madeni yao pamoja na riba ili na wao wanufaike au waepuke hasara kama ambavyo wenzao wa nje wanavyoepuka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA (MHE. LAURENT D. LUSWETULA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nikiri kama Serikali tumeendelea kulipa madeni yakiwemo madeni ya wakandarasi wa kigeni na madeni ya wakandarasi ambao ni wazawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kusema kwenye swali langu la msingi, kwanza hakuna upendeleo wowote baina ya wakandarasi wa nje na wakandarasi wa ndani, kama Serikali tumekuwa tukishamaliza kufanya uhakiki wa madeni hayo tumekuwa tukilipa kwa wakati na hivyo Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini nipende kukuhakikishia kwamba kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba madeni yote ya wazawa na wa kigeni yanalipwa kwa wakati.