Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Christina Christopher Mnzava (2 total)

MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa watumishi wetu, vijana wetu wanajitolea katika sekta ya afya pamoja na elimu wanapotuma maombi huwa wanaambatanisha ile barua ya taasisi ambayo walikuwa wanajitolea, kwa nini hawapewi kipaumbele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwisha kueleza kwenye swali letu la msingi, kwa kuzingatia Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma kwamba ajira zote kwa sasa zinatolewa kwa njia ya ushindani ili kutenda haki kwa watu wote, ili kupata usawa, hivyo basi, msisitizo unaendelea kuwekwa kwamba vijana wanapopata nafasi ya kujitolea, wajitolee ili kujijengea uzoefu na wapate ujuzi na maarifa ili yale waliyoyapata darasani waende kuyatumia katika vitendo na mwisho linapotokea suala la ajira basi washiriki katika ushindani ili waweze kuajiriwa Serikalini.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, TARURA imekuwa ikijenga barabara kwa kiwango cha lami kwa baadhi ya centre, lakini katika Halmashauri ya Shinyanga, Jimbo la Solwa hakuna Kata ambayo ina barabara ya kiwango cha lami, ni lini Serikali itatujengea angalau kwenye Makao Makuu ya Halmashauri barabara kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango wetu wa barabara za vijijini na mijini tunazo barabara za udongo, barabara za changarawe na barabara za lami, na tumeweka kipaumbele kuendelea kuongeza barabara za lami, hususan maeneo ya miji ili kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba tunapoendelea na bajeti zetu, tutatoa kipaumbele kwenye eneo la Jimbo hilo la Solwa na hizo barabara za Kata zile ambazo zinawezekana kujengwa kwa awamu, tutaanza ujenzi kwa awamu.