MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nitoe pongezi zangu kwa Serikali kwa juhudi kubwa inayofanya kuhakikisha mawasiliano yanapatikana, na hasa ninampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumeona juzi tu, tarehe 10 Aprili, 2026 alizindua minara 785 kwa ajili ya mawasiliano nchini. Pongezi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa mawasiliano yanaendelea kuimarika, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa urahisi hasa ukizingatia wafanyabiashara wengi wanatumia mitandao kwa ajili ya kufanya biashara zao wakiwemo wanawake?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninamshukuru kwa pongezi kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa kuaminika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwenye jibu lake kwamba Wizara yetu ina mpango mkakati mkubwa wa miaka mitano ya kuhakikisha kwamba nchi hii yote inakuwa na mtandao wa mawasiliano wa kuaminika na katika hilo, hii itatoa kipaumbele kikubwa kwa makundi maalum yakiwemo akina mama, vijana, wenye ulemavu na watu wengine wote walio katika makundi hayo kama wazee na watu wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kuhakikisha, ndani ya miaka hii mitano, kila mwananchi na kila kundi maalum litakuwa na uso wa furaha katika sekta hii ya mawasiliano.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni kwa kiasi gani mfuko huu umewanufaisha wanawake tangu umeanzishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kusimamia marejesho kwa wakopaji wa mfuko huu?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Tamima kwa maswali mazuri. Hadi sasa sisi kama Wizara ni zaidi ya shilingi 1,400,000,000, tayari wanawake wameweza kunufaika na masharti ni nafuu. Kuhusu kusimamia marejesho, hii ni kazi yetu sisi sote viongozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kutoa elimu kwa wenzetu ambao tunawasemea, na vilevile kabla ya kupewa fedha wanapewa elimu ya fedha, lipa kwa hekima na vilevile rejesha kwa wakati. Kwa hiyo, tunaendelea kuona kwamba wapewe ndani ya mfuko ukiwa ndani ya Wizara kwa masharti nafuu, kabla hawajaendelea na usumbufu wa marejesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukapeleka hili kwenye vyombo vyetu vya fedha, kule ambako mpaka sasa wengi wetu tumeona kwamba wanalalamika masharti ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, sisi kwa umoja wetu Waheshimiwa Wabunge, kila mmoja ana kundi kubwa nyuma yake, kila mmoja akiweza kusisitiza mtu akope na kulipa kwa wakati, basi wengi wataweza kurejesha ili wengi waweze kukopa.