Supplementary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (3 total)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa majibu yaliyotolewa na Serikali kutambua umuhimu wa jambo hilo, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutenga maeneo ni jambo moja na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanapata hivyo viwanda ni jambo la pili. Sasa Serikali haioni umuhimu, kwa sababu maeneo mengi yaliyotengwa wanajenga viwanda Dar es Salaam, Pwani na maeneo ya mijini. Serikali haioni umuhimu wa kutenga vivutio mahususi kwenye maeneo ya vijijini ambako kule ndiko kwenye ajira kubwa, katika muktadha wa business as usual ambayo Wizara hii ndiyo imejirasimu nao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kwanza kwa kuwatetea wananchi wa Njombe Mjini. Mheshimiwa Mwanyika, amekuwa akifuatilia sana suala la uwekezaji kwenye mazao ya misitu nasi kama Wizara tunamuahidi kumpa ushirikiano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba huko nyuma viwanda vingi vili-concentrate upande wa Pwani, Mikoa ya Pwani Dar es Salaam na Tanga, ndiyo maana katika mpango wa miaka mitano wa Serikali tumekuja na mkakati wa ku-decentralize viwanda vyetu kupeleka kila maeneo. Kwa kupitia hilo tumeanzisha mpango wa maeneo maalum ya uwekezaji na ndiyo maana upande wa Njombe tunaenda kuanzisha maeneo maalum ya uwekezaji wa misitu, upande wa Bunda tunaenda kuanzisha Bunda SEZ ambapo tunaenda kuanzisha maeneo maalum kwa ajili ya mazao ya blue economy, vilevile Kigoma upande wa michikichi na mihogo na hapa Dodoma tuna eneo maalum kwa ajili uchenjuaji wa madini ambayo ni adimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kupitia hii nina uhakika sasa, ile adha kwamba viwanda vyote vime-concentrate ukanda moja inaenda kwisha na ninaomba nimtoe mashaka Mbunge kwamba tunaenda kutekeleza hili katika Mkoa wa Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Halmashauri ya Mji Njombe tuna mradi wa Igombwi umekaa zaidi ya miaka sita bila kukamilika, uko 85%. Ninaomba uhakika ni lini mradi huu utakamilika? Je, umetengwa kwenye bajeti ya sasa?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali hili. Huo ni mradi wa kimkakati, na ni moja ya agenda katika jimbo lake. Tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 30 kwa ajili ya malipo ya wakandarasi. Tutatoa fedha kuhakikisha mradi unakamilika na wananchi hawa waweze kupata huduma ya majisafi na salama.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Mji Njombe ni eneo linalokua kiuwekezaji, lakini haliwezi kuendelea na kupata wawekezaji wengi kama hatuna substation. Ni lini Serikali itajenga substation kubwa itakayovutia uwekezaji Njombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeshafanya tathmini ya mahitaji ya umeme katika nchi nzima na ni katika azma hiyo Serikali imeweza kufikisha umeme katika vijiji vyote vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maeneo yote yanayohitaji kuongezewa nguvu ya umeme, transfoma, na vituo vya kupoza umeme. Pia vinazingatia ikiwa ni pamoja na eneo lake. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba Serikali ipo kazini kuhakikisha kwamba atafikishiwa umeme wanaouhitaji.