Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Edwin Enosy Swalle (4 total)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kata ya Kidegembye, hasa pale kwenye Kijiji cha Image, ambako Mheshimiwa Naibu Waziri anapafahamu, wananchi wamejengewa shule nzuri sana ya amali, lakini ipo mbali na makazi ya wananchi, kwa hivyo, hakuna nyumba za waalimu wala karakana kwa ajili ya wale wanafunzi, na hakuna bweni. Ni lini Serikali itapeleka fedha, kwa ajili ya bweni, karakana na nyumba za waalimu pale Image?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa shule hizi tulianza na awamu ya kwanza ya shilingi milioni 584 na tulijenga miundombinu ya madarasa na shule zile zimeanza kutoa huduma, kwa maana ya shule za kutwa. Awamu ya pili, tunakwenda kutenga shilingi bilioni 1,600, kwa ajili ya kujenga miundombinu inayosalia, yakiwemo mabweni, karakana na kununua vifaa vya kihandisi, ili wanafunzi wanaojifunza masuala ya kiuhandisi waweze kuwa na mazingira bora ya kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Swalle, Mbunge wa Jimbo la Lupembe, unayefanya kazi kubwa sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Lupembe, kwamba, Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua hilo, na tupo kwenye taratibu za kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha shule hizo zote 103, ili ziweze kutimiza lengo lililokusudiwa, ahsante.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Mikopo ya 10% imetoa fursa kwa watu wenye ulemavu kukopa mtu mmoja mmoja; pia imetoa fursa kwa watu kuunda vikundi vya watu watano na kuendelea, lakini wapo vijana wengi wamehitimu vyuo vikuu na vyuo vya kati wana ujuzi maalum ambao pengine kuwapata kuwa kikundi, watu wengi ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni haja sasa kuongeza kundi la nne ambalo ni la watu ambao wana ujuzi maalum waruhusiwe kukopa mtu mmoja, mmoja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Edwin Enosy Swalle, Mbunge wa Lupembe kwa wazo zuri. Serikali ipo tayari kupokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Kupitia wataalam wetu watakaa na kufanya tathmini, na tutapata majibu na kuona namna ya kuzingatia ushauri huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokea ushauri huo wa Mheshimiwa Mbunge na tutafanya tathmini kupitia taratibu za Serikali na kuona namna ya kuboresha hatua kwa hatua, kwa sababu mikopo hii itaendelea kuboreshwa siku hadi siku kulingana na mahitaji ya jamii yetu. Ahsante sana.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, wananchi wa Lupembe wanasubiri kwa hamu sana kiwanda hiki cha chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa Mahakama Kuu ilitoa amri kiwanda kirejeshwe kwa wananchi tangu mwaka 2022, lakini pia Mheshimiwa Rais kwa kuwapenda wananchi wa Lupembe na ili kuwapelekea tabasamu wananchi hawa alikwishaelekeza kiwanda hiki kirejeshwe kwa wananchi tangu 2022 akiwa pale Mtwango. Je, ni nani anayechelewesha huu mchakato mpaka leo kiwanda hakijarudi kwa wananchi wa Lupembe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wananchi wangu wa Tarafa ya Lupembe kwa maana ya Kata za Idamba, Filiga, Lupembe, Matengwe, Ukalawa pamoja na Kidegembye na Lupembe yenyewe wanalima sana chai kwenye mvua nyingi, wanakaa kwenye mabanda kwa muda mrefu, lakini bei ya chai ni 360 ambayo ni ndogo sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bei ya chai hadi shilingi 1,000 kwa kilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge Edwin Swalle kwa kupigania sana zao la chai humu Bungeni. Ninaomba nikubaliane naye kwamba kuna maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba, kiwanda hiki kinarudi kwa wakulima kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uzalishaji ili kuongeza thamani ya zao la chai, zao ambalo ni la kimkakati kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIRDO ambayo ni taasisi chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, ilishaanza zoezi hilo la tathmini mwaka 2024 ikikamilisha tathmini ya majengo na mitambo, changamoto ambayo walikumbana nayo ilikuwa ni kufanya tathmini ya ardhi. Chama cha Ushirika cha MUVYULU ilitakiwa kutoa hati hiyo ambayo kwa kuchelewesha kwao kulipelekea TIRDO kukwama na zoezi la kukamalisha zoezi la tathmini la kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kikao ambacho kilifanyika tarehe 13 Machi, 2026 chini wa Wizara ya Kilimo ambacho kilihusisha Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Viwanda na Biashara, Bodi ya Chai, Mamlaka ya Wilaya kule Njombe, Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Chama cha Ushirika chenyewe pamoja na mwekezaji, walikubaliana kwamba Chama cha Ushirika kiwasilishe hati hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafarijika kulitaarifu Bunge lako kwamba hati hiyo imeshawasilishwa tayari, wakati utawala wa mkoa na tayari ameshawasilisha kwa Bodi ya Chai. Hivyo, maelekezo yetu ni TIRDO kurudi kwa ajili ya kukamilisha tathmini hiyo ili Hazina wakamilishe malipo kwa mwekezaji, kiwanda hicho kirudi kwa wakulima na kuendelea na uzalishaji na ongezeko la thamani ya zao la chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuwasilisha.
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara ya Lupembe kwenda Ikondo, na hii barabara inapita nyumbani kwangu pale Kanikelele, yako maeneo matatu yameharibika vibaya sana hata mimi leo siwezi kufika pale kwangu nyumbani Kanikelele. Ni nini maagizo ya Meneja wa Njombe kufanya marekebisho sehemu hizo tatu watu waweze kusafiri kwenye hii barabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwakumbusha Mameneja wa TARURA katika Wilaya zetu zote na katika Mikoa yetu yote kwamba tunafahamu kuna hali ya mvua inaendelea, lakini tuna barabara muhimu sana katika maeneo yetu ambazo ni lazima ziendelee angalau kupitika wakati tunasubiri matengenezo ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika Jimbo la Lupembe ninamwelekeza Meneja wa TARURA, Mkoa wa Njombe na Wilaya ya Njombe kwenda kufanya tathmini kwenye barabara hiyo na kuona linaloweza kufanyika angalau matengenezo ya muda yafanyike, barabara iendelee kupitika, wakati tunasubiri hali ya hewa kukaa vizuri kwa ajili ya matengenezo ya kudumu. (Makofi)