Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Festo John Dugange (3 total)
MHE. SARA M. ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingi zimekuwa zikiharibika kwenye Jimbo la Mvomero hasa maeneo wanayofanya shughuli za uchimbaji wa madini; kama Kata ya Mvomero, Kata ya Lubungo na maeneo mengine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza bajeti kwenye maeneo hayo ya barabara ili ziweze kupitika kipindi chote cha shughuli za wananchi wanapofanya shughuli zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 mpaka sasa imeongeza bajeti ya TARURA kwa zaidi ya takribani mara nne na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba barabara zetu zote za vijijini na mijini zinapitika ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha bidhaa zao kwa ufanisi mkubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nikuhakikishie Mheshimiwa Sara Msafiri, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, kwamba Serikali inatambua changamoto na hususani ya Mvomero kwa hali ya hewa mvua nyingi mafuriko na shughuli nyingine za kiuchumi ambazo zinapelekea barabara nyingi kuharibika na majimbo mengine yenye sura ya aina ya Mvomero, Serikali imeweka mpango madhubuti kuhakikisha kwamba barabara hizo zinajengwa na kupitika vizuri. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kuniona. Barabara inayotuunganisha kati ya Shirati – Minigo na Kata ya Nyamtinga Rung’enye imeharibika kwa muda mrefu na haipitiki kwa sasa. Ninataka kujua Serikali ina mpango gani juu ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha changarawe, pamoja na makalavati yanayozunguka barabarani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mbunge wa Rorya, Mheshimiwa Wambura Chege kwamba, Serikali hivi sasa inafanya tathmini ya barabara zote zilizokatika kufuatia mafuriko na mvua nyingi. Tutatoa kipaumbele kwenye barabara hiyo katika Jimbo la Rorya, kwanza, kupata taarifa za tathmini na mahitaji ya gharama mapema. Pili, kutenga fedha, kwa ajili ya matengenezo, ili barabara iweze kupitika wakati tunaendelea kupanga mipango ya muda wa kati na muda mrefu, kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa kadiri itakavyoonekana inafaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ninamhakikishia kwamba, suala hilo tumelichukua, tunalifanyia kazi. Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Rorya wakamilishe tathmini ya barabara hiyo mapema iwezekanavyo na kuiwasilisha Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI kwa sababu, tupo hatua za mwisho za ku-comply yale mahitaji ya kupeleka fedha, kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo. Ahsante sana.
MHE. MWANTATU M. KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ningependa kumwuliza swali lenye kipengele (a) na (b) la nyongeza:-
(a) Kuna mpango gani wa Serikali katika kuhakikisha shule za wasichana zinazojengwa mikoani zinapatiwa vifaa vya maabara vya kutosha pamoja na watu wa maabara?
(b) Kwa kuwa Serikali inaendelea kujenga majengo ya shule za sekondari, je, ni upi mkakati wa Serikali katika kuhakikisha changamoto hii inapatiwa mwarobaini wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali kwanza imeweka kipaumbele cha hali ya juu katika ujenzi wa shule za masomo ya sayansi, na katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imejenga shule za sayansi za mikoa 26 kwa kila mkoa ambazo ziligharimu takribani shilingi bilioni 4.6 kila shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule zile zimejengewa miundombinu yote kwa maana ya maabara za Fizikia, Kemia na Biolojia, na zimepelekewa vifaa vya maabara na wataalamu wa maabara ili kuwezesha masomo ya sayansi yaweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kutenga fedha. Hivi sasa tuko kwenye taratibu za manunuzi ya vifaa vya maabara vya zaidi ya shilingi bilioni 13.97 ili kuhakikisha shule zetu zote za wasichana, shule za wavulana na shule mchanganyiko zinapata vifaa vya kutosha vya maabara ili wanafunzi wetu waweze kusoma vizuri na kwa ufanisi zaidi. Ahsante.