Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (2 total)

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kata ya Seed Farm, Manispaa ya Songea, haina sekondari ya kata. Je, ni lini Serikali itajenga sekondari ya kata katika kata hiyo ya Seed Farm?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Songea Mjini, kaka yangu Ndumbaro, amefuatilia mara kadhaa suala la ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata ya Seed Farm, Manispaa ya Songea. Ninaomba nimhakikishie tu kwamba, tuko hatua za mwisho. Tulikubaliana na wataalamu wafanye tathmini ya vigezo na baada ya hapo tuhakikishe tunapeleka fedha, kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutahakikisha baada ya kupokea vigezo hivyo na kufanya tathmini, tutatoa kipaumbele kinachotakiwa kupitia mapato ya ndani ya Manispaa ya Songea na Serikali Kuu, ili tuweze kujenga shule hiyo ikiwa vigezo vitakuwa vimefikiwa.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya mchepuko, kilomita 16, ndani ya Jimbo la Songea Mjini wananchi bado hawajalipwa fidia. Je, ni lini Serikali italipa fidia, ili ujenzi wa barabara hiyo uweze kuanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna barabara ya kilomita 16 ambayo sisi tunasema ni Songea Bypass. Barabara hii inajengwa na Serikali ya Tanzania kwa kusaidiana na World Bank. Tayari tumeshafanya uthamini wa wananchi ambao watapisha mradi huo ambao ni zaidi kidogo ya shilingi bilioni Nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Ndumbaro pamoja na wananchi wa Songea kwamba tunategemea Serikali kulipa fidia hiyo ambayo tayari ipo Hazina ili mradi huo uanze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hiyo barabara ya bypass pia mkandarasi huyo ndiye atakayejenga kutoka Songea kilometa 100 kuelekea Njombe hadi Lutukira tayari ameshaanza kazi, yuko kwenye hatua za awali kwa maana ya mobilization, atakapokuwa anaendelea, basi tukishalipa ataanza pia kujenga hicho kipande cha bypass ili magari mengi yanayopita hapo na hasa ya makaa ya mawe kwenda huko Mtwara yasiweze kupita Songea Mjini, ahsante.