Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya (3 total)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawashukuru. Barabara ya kutoka Omugakorongo – Kituntu – Rwambaizi – Igurwa – Murongo ipo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, imekuwa kwenye manunuzi kwa muda mrefu, ni barabara muhimu kwani inaunganisha nchi yetu na nchi za Afrika Mashariki; na kujengwa kwa kiwango cha lami kutainua uchumi wa Kagera pamoja na Taifa letu. Je, ni lini barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni kati ya zile barabara zetu kuu, inaunganisha Uganda na Tanzania kupitia Daraja la Murongo. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba hii barabara ilikuwa imetangazwa na tulipata mkandarasi, lakini tukashindwana naye kimkataba. Hivyo, hii barabara imetangazwa tena, iko kwenye hatua za manunuzi kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Tunaanzia Murongo kuja Omugakorongo. Ahsante. (Makofi)
MHE. EDIBILY K. KINYOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Barabara ya Uvinza – Kasulu kwa kiwango cha lami, ikizingatiwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli Barabara ya Uvinza kwenda Kasulu ina kama kilometa 60 hadi 62. Tumeshakamilisha usanifu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kipaumbele. Sisi kama Wizara ya Ujenzi na TANROADS tumeichukulia hii barabara kwa kipaumbele kikubwa sana, kwa sababu ndiyo barabara ambayo inatoka Tunduma – Sumbawanga – Mpanda – Uvinza – Kasulu – Kibondo hadi Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninavyoongea sasa hivi, hicho kipande ndicho pekee ambacho kitakuwa kimebaki hakijajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatafuta fedha ili kuhakikisha kwamba hicho kipande tumekikamilisha ili tuweze kukamilisha hiyo barabara yote ambayo ni T9.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya mchepuko, kilomita 16, ndani ya Jimbo la Songea Mjini wananchi bado hawajalipwa fidia. Je, ni lini Serikali italipa fidia, ili ujenzi wa barabara hiyo uweze kuanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna barabara ya kilomita 16 ambayo sisi tunasema ni Songea Bypass. Barabara hii inajengwa na Serikali ya Tanzania kwa kusaidiana na World Bank. Tayari tumeshafanya uthamini wa wananchi ambao watapisha mradi huo ambao ni zaidi kidogo ya shilingi bilioni Nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamhakikishia Mheshimiwa Ndumbaro pamoja na wananchi wa Songea kwamba tunategemea Serikali kulipa fidia hiyo ambayo tayari ipo Hazina ili mradi huo uanze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hiyo barabara ya bypass pia mkandarasi huyo ndiye atakayejenga kutoka Songea kilometa 100 kuelekea Njombe hadi Lutukira tayari ameshaanza kazi, yuko kwenye hatua za awali kwa maana ya mobilization, atakapokuwa anaendelea, basi tukishalipa ataanza pia kujenga hicho kipande cha bypass ili magari mengi yanayopita hapo na hasa ya makaa ya mawe kwenda huko Mtwara yasiweze kupita Songea Mjini, ahsante.