MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Je, lini changamoto ya Mawasiliano Jimbo la Tabora Mjini Kata za Ikomwa, Ndevelwa, Ntalikwa, Kabila, Kalunde na Itetemia itamalizika?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Jimbo la Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kupitia UCSAF na watoa huduma wa Mawasiliano ilifikisha huduma za mawasiliano katika Kata husika kama ifuatavyo: Kata ya Ikomwa (Airtel, Vodacom na Halotel), Kata ya Ndevelwa (Halotel), Kata ya Ntalikwa (Airtel), Kata ya Kabila (Honora, Airtel na Halotel), Kata ya Kalunde (Honora, Vodacom, Airtel na Halotel) na Kata ya Itetemia (Halotel).
Mheshimiwa Spika, Kata zote sita zimefikiwa na watoa huduma za mawasiliano kama nilivyotangulia kuwataja kwa kuzijengea minara ambayo imekamilika na inafanya kazi. Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali lake kwa kuonyesha kuna tatizo la Mawasiliano, Wizara kwa kushirikiana na UCSAF na Watoa Huduma wa Mawasiliano itatuma wataalam katika Jimbo la Tabora Mjini ili kufanya tathmini ya kina ya hali ya mawasiliano kwa lengo la kujua tatizo lililopo.
Mheshimiwa Spika, upo uwezekano wa kutokea tatizo la kupatikana kwa mawasiliano ya uhakika katika baadhi ya maeneo hata kama minara ya mawasiliano ilishajengwa katika maeneo hayo kwa sababu kama vile ongezeko la watu, kukua kwa shughuli za kiuchumi pamoja na jiografia ya eneo husika. Pia, sababu nyingine ni kuanzishwa kwa makazi mapya katika maeneo ambayo awali hayakuwa na wakazi, hivyo kuongeza uhitaji wa kujengwa minara zaidi au kuboreshwa kwa minara iliyopo.
Mheshimiwa Spika, tathmini itakayofanyika itatoa suluhisho sahihi, kama ni kuongeza nguvu ya mitambo katika minara iliyopo au kujenga minara mipya. Iwapo suluhisho ni ujenzi wa minara mipya, Kata husika zitajumuishwa katika miradi itakayotekelezwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Aidha, kupitia Mradi wa Awamu ya 11 utakaotangazwa mwishoni mwa mwezi Februari, Kata ya Ndevelwa, Kijiji cha Itulu utajengwa mnara wa mawasiliano.