Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (2 total)

MHE. JONAS W. MBUNDA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kutekeleza Mradi wa TACTIC katika Jimbo la Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas William Mbunda.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia imeanza utekelezaji wa Mradi wa TACTIC katika Jimbo la Mbinga Mjini, ambapo sasa Mradi huu upo hatua ya usanifu chini ya Mhandisi Mshauri aitwaye Bosphorus Technical Consulting Corporation ikishirikiana na Building Design Authority Limited pamoja na Masterpiece Consult Limited. Mara baada ya kukamilika usanifu huo ujenzi utaanza mara moja. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Shule ya Sekondari Sanzate na Tirina - Bunda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI ninaomba uridhie kwamba majibu nitakayoyasoma hapa ndiyo yachukuliwe kama majibu rasmi ya Serikali yale yaliyokuwa tumeyatanguliza yana marekebisho kidogo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitoa Shilingi Milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa manne, jengo la utawala, maktaba, maabara tatu, chumba cha TEHAMA, matundu ya vyoo ishirini na matenki ya kuvuna maji ya mvua, katika shule mpya ya Tirina. Pia, Serikali imetoa Shilingi Milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne, ofisi moja na matundu nane ya vyoo, ukamilishaji wa madarasa matatu na ofisi moja katika Shule ya Sekondari Sanzate.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miundombinu yote iliyobaki kwenye shule hizi mbili za Tirina na Sanzate.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kuwasilisha. (Makofi)