MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi. Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo Mkoani Mtwara ni miongoni mwa viwanja ambavyo vinaingiza mapato makubwa sana mechi inapofanyika: Je, Serikali kwa kushirikiana na mmiliki wa uwanja huu ina mpango gani wa kufanya ukarabati mkubwa uwanja huu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru na nimshukuru Mheshimiwa Chikota kwa swali zuri la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Nangwanda Sijaona haumilikiwi moja kwa moja na Serikali, ni uwanja wa miongoni mwa wadau wetu, Chama Cha Mapinduzi. Kama ambavyo nilishajibu mara kadhaa hapa, tunayo mazungumzo na Chama Cha Mapinduzi kuona namna ambavyo tunaweza kuhakikisha tunaweza kuvifanyia ukarabati kwa utaratibu unaofaa viwanja vingi ambavyo vinamilikiwa na taasisi hii na kuona namna ambavyo mapato yatafanyiwa mgawanyo baada ya uendeshaji kati ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali ambayo itakuwa imefanya ukarabati wa viwanja hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Uwanja wa Nangwanda Sijaona ni miongoni mwa viwanja ambavyo vipo katika fikra zetu. Tutakapokubaliana na wamiliki wa kiwanja hiki ambao ni Chama Cha Mapinduzi tutakwenda kukifanyia ukarabati na kuhakikisha kinakuwa katika hali nzuri kwa ajili ya kufanya shughuli za michezo