Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mary Daniel Surati (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027
MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuchangia bajeti ya Maendeleo ya Vijana. Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuendelea kusimama hapa nikiwa buheri wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, pia ninaendelea kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Serengeti kwa kuendelea kuniamini kijana kama mimi kuendelea kuwawakilisha Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa ni mchoyo wa fadhila kama kijana ambaye ninatokana na asasi za kiraia ambapo ninafahamu ni kwa jinsi gani kipindi hicho, hata sijajua Mungu atanibariki kuwa Mbunge, tulikuwa tunakuja mara ngapi hapa Bungeni kushawishi Wabunge kwamba sisi vijana tuweze kupewa Wizara yetu ya Vijana. Ndoto hii amekwenda kuitimiza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwa dhati ya moyo wangu ninasema ahsante kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hakukomea hapo tu, ameenda mbali, amerekebisha Sheria ya Manunuzi ya Umma, ambapo amezitaka taasisi zote kutenga 30% ya manunuzi yao kuhakikisha kwamba makundi maalum yanaweza kunufaika. Katika makundi hayo ni sambamba na vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kumekuwa na programu mbalimbali za kunufaisha vijana, kama programu ya Building a Better Tomorrow. Pia kuna mafunzo ambayo yamekuwa yanatolewa kupitia VETA na takribani vijana 8,000 wamenufaika na mafunzo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo kuna ajira ambazo zimekuwa zinatolewa na sekta mbalimbali ambapo jumla ni sekta milioni nane. Ninazidi kutoa shukurani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia ninampongeza kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Joel Arthur Nanauka, nikitambua kwamba ni Mbunge kwa mara ya kwanza, ni Waziri mara ya kwanza na Wizara pia ni mpya kwa mara ya kwanza, lakini ameonesha weledi yeye pamoja na watendaji wote anaofanya nao kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwa kuwa ni wapya, bado wapo katika kutengeneza na kuboresha system za kuweza kuwatumikia vijana. Ila amekuwa mchapakazi kweli kweli, na hata sisi vijana wenzie tunajivunia uwepo wake, na tunaona imani ambayo Rais amempatia, hajakosea. Tunashukuru sana kwa jinsi anavyotuwakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo nimeguswa nalo sana katika bajeti ambayo kaka yangu Joel, amei-present leo ni kwamba, katika bajeti ya 2024/2025 vijana tukiwa tu kama Idara, fedha ambazo tulitengewa kwa ajili ya maendeleo ya vijana ilikuwa ni shilingi bilioni moja pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ndugu yangu Waziri Joel Arthur Nanauka, ametusomea hapa inaonesha tunaenda kupewa takribani shilingi bilioni tano, ambayo ni sawa na ongezeko la 80%. Hii ni dhati Dkt. Samia Suluhu Hassan nia yake ya ukweli ya kuwezesha vijana inazidi kuthibitika siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, ukiangalia pamoja na ku-present jambo hili, pia kulikuwa na suala la kanzidata. Ni moja kati ya mambo ambayo yamekuwa yanaongelewa mara nyingi sana. Tunawezaje kupanga kusaidia vijana ikiwa hatuwatambui? Leo Waziri wa Maendeleo ya Vijana amekuja hapa na ametuhakikishia tutakuwa na kanzidata ambayo itatambua vijana wetu na itaweza kuhakikisha inawaunganisha na fursa ambazo zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye ushauri. Kulingana na hayo yote ambayo yamezungumzwa na mazuri mengi, sema tu ni muda umeisha, lakini yapo mengi ambayo natamani niendelee kuyaongelea. Kwa kuwa, nina imani na Wizara husika ninaomba sasa nishauri kwa wepesi sana na haraka mambo machache tu ambayo ninaamini yatazidi kuboresha mambo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kwamba tunayo Sheria ya Manunuzi ya Umma; pamoja na kwamba imetengwa hii 30% lakini ni ukweli usiopingika bado kuna taasisi za umma hazifikii hiyo 30%. Nimwombe Waziri wa Maendeleo ya Vijana, kwa namna ambavyo amekuwa mchakarikaji, tafadhali tushirikiane na Ndugu zetu wa VETA ili tuongeze vikundi vingi ambavyo vitakwenda kuomba fursa hiyo na kuweza kusaidia vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nimeona Ndugu yangu ameweza kuongea hoja ambayo ni agenda ya muda mrefu sana ya kuanzishwa kwa benki ya vijana, nimwombe Waziri wetu wa Maendeleo ya Vijana, hizi fedha ambazo zitakuwepo ambazo tutapatiwa shilingi bilioni tano, sambamba na hizi shilingi bilioni 200 ambazo Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeomba zirudishwe katika Wizara husika. Ninaomba zitumike pamoja na kuanzisha benki yetu ya vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hekima yangu inanituma kwamba watendaji wetu wa Wizara ya Vijana siyo bankers, siyo loan officers wao wapo pale kutengeneza mazingira rafiki ya kuwawezesha vijana kuweza kufikia malengo yao. Tunapokuwa tunajikita wao ndio wawe wakopeshaji, ndio wawe wafuatiliaji, ndio tena wabadilike wawe chombo cha fedha, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kushauri kwamba Wizara ya Vijana ibaki Wizara ya Vijana na isigeuzwe kuwa taasisi ya fedha. Hivyo, tutengeneze benki yetu ambayo itakuwa ni taasisi ya fedha, ishughulike na changamoto za vijana kama kutoa elimu ya mikopo, kuwafundisha vijana namna ya kuweka maandiko kwa ajili ya kutengeneza miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyong’ang’ana kuendelea kuwaachia na kuwatwika mzigo huu watendaji wetu, ndiyo maana tunatengeneza loan defaulters wengi. Tunaweza kuzungumza hapa fedha zitoke, zitoke, je, zinarudije? Fedha zetu zile hazitoki ili mtu aende atumie na ziwe za kwake. Ni fedha ambazo ni revolving fund, mtu anatakiwa apewe, atumie, arejeshe ili na wengine waendelee kupewa. Kwa hiyo, ninaendelea kuhimiza Waziri wetu wa Maendeleo ya Vijana, ajikite katika hii ndoto ili itimilizike, vijana tuweze kuwa na benki yetu ya vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kuongezea jambo lingine katika mitandao ya kijamii. Waziri wa Maendeleo ya Vijana, amempongeza kijana mmoja ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Leon Mendez, jina lake halisi ni Leodiga Kachebona. Kama tuna vijana ambao wanakuwa na mawazo makubwa na ya msingi kama haya wanaweza kutambulika East African Youth Award, wanaweza kutambulika Ghana Accra, kuna dhambi gani wakatambulika na sisi hapa kwetu nchini, na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akaalikwa kama mgeni rasmi ili aone juhudi zake, upendo wake na yale yote anayoyafanya kwa ajili ya vijana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana kweli tupo tayari na tunahakikisha kweli tunayafanyia kazi. Kwa hiyo, ninakuomba Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Tanzania tuanze kutoa tuzo maalumu ya kutambua mawazo bora na ya msingi ambayo vijana wetu wanayafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kumalizia japo siyo kwa umuhimu, nilikuwa ninaomba, pamoja na kwamba Serikali yetu inashughulika usiku na mchana kwa kushirikiana na sekta nyingine zote kutatua changamoto ya vijana. Ni changamoto mtambuka na Wizara ya Vijana pekee haiwezi kumaliza hilo tatizo. Tunaamini na sekta nyingine pia zinaendelea kutoa ushiriki wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Waziri wa Maendeleo ya Vijana, tuangalie namna taasisi zinazoongozwa na vijana, ambazo ni Non-Governmental Organisation wanajitolea kuweza kutoa elimu za fedha, kuweza kuunganisha vijana, kuwaelimisha katika uongozi, lakini bado hawana uwezo wa kifedha, bado hawana mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa Wizara hii iwe na mkakati maalumu wa kuangalia ni jinsi gani hizi non-governmental organisation zinazoongozwa na vijana, zinaweza walau kusaidiwa ruzuku, ama mafunzo ili ziendelee kusaidia nguvu kubwa hii ambayo tunaona Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa kuongozwa na Mheshimiwa Dkt. Joel Arthur Nanauka, inakuwa inafanya mambo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi ninaona kwamba ni jambo la heri sana tukiendelea kushirikiana kwa dhati ya mioyo yetu ...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati ya mioyo yetu kuendelea kulitengeneza Taifa letu, maana sisi ni leo, na ni kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, ninaunga mkono hoja. (Makofi)