Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mary Daniel Surati (1 total)

MHE. MARY D. SURATI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fidia kwa wakati kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikilipa kifuta jasho na kifuta machozi kama mkono wa pole au faraja kwa wananchi wanaopata madhara kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu, kwa lengo la kuimarisha mtazamo chanya kwa wananchi juu ya shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori nchini. Malipo hayo yamekuwa yakifanyika kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za Mwaka 2011 na marekebisho yake ya mwaka 2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha utaratibu wa kushughulikia masuala ya wanyamapori wakali na waharibifu, Serikali imeanza kutumia mfumo wa kielektroniki wa PAIS (Problem Animal Information System), ambao utawezesha kurahisisha ukusanyaji na uwasilishaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa wakati, kuongeza kasi ya uchakataji na uhakiki wa taarifa zinazowasilishwa, kuwezesha malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kufanyika kwa wakati, na kupunguza udanganyifu wa taarifa zinazowasilishwa.