MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameendelea kuyatoa. Pia nilikuwa ninaomba wananchi wa Jimbo la Seregenti wanaomba kufahamu, ni lini Serikali itaanza kutoa fidia stahiki inayoendana na hasara wanazopata wananchi wanaoathirika na Wanyamapori? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi hawa wataendelea kupata fidia ambazo wanastahiki, na kwa sasa hakuna mtu yeyote ambaye atakosa haki yake ya msingi.
MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa juhudi zote ambazo zimekuwa zikifanyika kutokana na changamoto ya wanyamapori hao, hasa Simba. Hata hivyo, nilikuwa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, kutokana na takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, ambazo zinatamka wazi kwamba, wananchi wanaopatikana katika Hifadhi ya Serengeti ndiyo ambao wanaathiriwa zaidi na wanyamapori kuliko hifadhi nyingine zote, ukizingatia tuna Ikorongo Game Reserve, Grumeti, Ilona pamoja na Serapa, je, kwa sasa hivi ambavyo nyumbu wanaanza sasa kurudi huku kutoka Maasai Mara, Wizara imejiandaaje kutusaidia magari ya Sepali maana tembo wale wote huwa hawapendi ule mlio wa wale nyumbu na wanaanza kurudi kwenye makazi ya wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu namba mbili. Kumekuwa na ucheleweshwaji wa malipo ya fedha za open area, ambapo Vijiji vya Makundusi pamoja na Robanda havijapewa fedha hizo za malipo ya open area kuanzia Julai, 2025 mpaka hivi sasa tunavyozungumza. Hii inasababisha wananchi kutaka kurudushiwa maeneo yao ili waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi, hali ambayo inaweza ikazoofisha shughuli zetu za uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anaenda kulijibu swali hili kwamba…
MWENYEKITI: Mheshimiwa swali, umeshauliza maswali.
MHE. MARY D. SURATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini wananchi hawa wanakwenda kulipwa fedha hizo? Ninaomba akumbuke Hifadhi ya Serengeti…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mary, maana salamu yake siku zote ni ufuatiliaji wa suala hili. Kwa hiyo, ninampongeza sana kwa ufuatiliaji wake. Mara zote basi yeye unamkuta yupo Ofisini kwa ajili ya kufuatilia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaomba nikiri kuwa ni kweli kwa alichokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hii imechelewa kwa kipindi fulani. Ninaomba nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge, fedha hii kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha inaenda kulipwa na Serikali ndani ya mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu uhaba wa vitendea kazi ambao ameuzungumza, Serikali imeanzisha juhudi mbalimbali. Hivi ninavyozungumza, Serikali imenunua gari maalum ambalo linajulikana kama Mobile Veterinary Clinic. Gari hilo litapelekwa katika sehemu zote ikiwemo eneo la Serengeti. Vilevile tutaongeza idadi ya ndege nyuki ili kuhakikisha kwamba wale wanyama wakali na waharibifu wanarejeshwa katika sehemu yao ya hifadhi.