MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Barabara Kibaha DC yenye kilometa 34 ni barabara ambayo haipitiki, siyo rafiki na ina vitu muhimu sana. Kuna Kituo cha Afya cha Halmashauri na kuna shule ya Primary yenye watoto wenye mahitaji maalum na pia kuna uwanja mkubwa sana ambao mikutano yote inafanyika hapo ya Kibaha DC, na shughuli zote ikiwemo na burudani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami? Ni lini?
MWENYEKITI: Majibu, Mheshimiwa Naibu Waziri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake nimeyaelewa, lakini barabara aliyoitaja ndiyo sijaisikia vizuri.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Asha Baraka, taja tu barabara.
MHE. ASHA R. BARAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inaitwa kwa jina maarufu Makofia – Mlandizi yenye kilometa 34 ambayo inaunganisha hospitali kubwa dispensary kubwa ambayo wanatumia watu wa Mlandizi.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Makofia – Mlandizi nadhani itakuwa ni swali la tatu ama la nne katika session hii ya Bunge kuulizwa. Barabara hii tumeijibu na tutaendelea kujibu kwamba ni barabara ambayo ni muhimu sana kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tulikuwa tumefanya tathmini ya fidia awali, lakini ikaonekana muda umepita. Tumefanya tena uthamini upya ambao jedwali la malipo ya fidia iko Hazina kwa ajili ya kuwalipa hao wananchi ambao watapisha barabara ili hii barabara iweze kujengwa, ahsante.