MHE. ATHUMIN O. MAPALILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, mikopo hii ni muhimu sana kwa wananchi wetu, na walio wengi hawawezi kutumia mifumo hii ya ukopeshaji, hasa wale walioko kijijini, je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuwatumia Maafisa Watendaji wa Vijiji ili waweze kuwasaidia, hasa kundi la wanawake, kuweza kufikia fursa hizi za mikopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mtwara, kwamba Serikali inatambua changamoto hiyo, pamoja na kwamba, mfumo huu wa WEZESHA unatumika na simu yoyote; simu janja na simu za kawaida, lakini bado kuna changamoto ya uelewa kwa baadhi ya wanufaika au walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa maelekezo kwamba, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Maendeleo katika ngazi za kata na Maafisa Ustawi wa Jamii wawe sehemu ya kuwezesha kutoa elimu na hamasa kwa walengwa, ili waweze kupata elimu na ku-access mikopo hii kupitia maeneo yao. Kwa hiyo, suala hili linafanyika na tutaendelea kuliboresha zaidi ili watendaji waweze kuwasaidia vikundi hivi wapate nafuu na uwezo mzuri zaidi wa kupata mikopo hiyo.
MHE. ATHUMIN O. MAPALILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Wanawake wa Mkoa wa Mtwara hujihusisha zaidi na kilimo cha kunde, njugu na karanga, je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza mazao haya katika Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili tuwe na uhakika wa soko? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimpongeze vilevile Mheshimiwa Mbunge kwa swali la msingi. Ni kweli stakabathi za ghala imekuwa na faida kubwa kwa wananchi, na tumekuwa tukiingiza zao moja baada ya linguine, maana yake hatuwezi kuingiza mazao yote kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaangalia vilevile na ukubwa wa biashara ya hayo mazao, lakini na upatikanaji wake kwa urahisi, na biashara ya soko husika. Kwa hiyo, tutalifanyia tathmini zao la kunde ili tufanye haraka iwezekanavyo kuingiza katika Mfumo wa Stakabadhi ya Ghala.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili maana yake tunafanya sisi Wizara ya Kilimo tukishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara ambao ndiyo wasimamizi wa Bodi ya WRRB wale wasimamizi wa stakabadhi ya ghala.